Na
Mathias Canal, WEST-Zanzibar
Serikali imetoa kiasi cha
Dola Milioni tano (USD Mil 5) kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa majengo ya
Taasisi ya Chuo cha Bahari Zanzibar ambacho ni kampasi ya Chuo Kikuu cha Dar es
salaam kilichopo katika eneo la Buyu mjini Unguja Visiwani Zanzibar.
Fedha hizo zimetolewa
ambapo UDSM imetakiwa kuhakikisha kuwa
inatekeleza kwa ufanisi mkubwa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan kuhusu usimamizi wa mradi wa Benki ya Dunia wenye
takribani Trilioni moja.
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda ameyasema hayo tarehe 9 Julai 2022 wakati akikagua
ujenzi wa Taasisi ya Sayansi za Bahari-Zanzibar iliyopo chini ya Chuo Kikuu cha
Dar es salaam wakati akiwa katika ziara ya siku moja kisiwani Unguja.
Waziri Mkenda amesema kuwa
mradi huo wa mageuzi ya kiuchumi kupitia elimu ya juu una lengo la kuboresha
mitaala na miundombinu ikiwemo kujenga kampasi mpya za vyuo vikuu pia unalenga
kutoa ujuzi unaotakiwa na soko hasa uchumi wa viwanda.
Prof Mkenda amempongeza Mkuu
wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam ambaye ni Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe Dkt Jakaya Mrisho Kikwete kwa kusimamia na kukagua mara kwa
mara ujenzi wa maabara ya muda katika
chuo hicho kutokana na maaba ya chuo hicho ikiwemo ofisi kuungua mwishoni mwa
mwaka jana katika eneo la Malindi.
Katika hatua nyingine, Waziri
Mkenda amemtaka Makamu Mkuu wa Chuo cha Ardhi ambao ni wasimamizi wa ujenzi wa
Taasisi ya Sayansi za Bahari-Zanzibar kuhakikisha anafika haraka iwezekanavyo
mjini Zanzibar ili kukagua na kuhakikisha dosari zilizopo katika ujenzi wa chuo
hicho zinapatiwa ufumbuzi wa haraka.
“Hatutaruhusu Chuo chetu
kikuu chochote ambacho kinafundisha wataalamu halafu kisimamie kazi
isiridhishe, tunataka kazi ikisimamiwa na chuo chetu chochote iweze kuakisi ule
ubora ambao tunatarajia ” Amekaririwa Waziri Mkenda
Waziri Mkenda amesema kuwa
hata kama muda wa usimamizi wa mradi umekwisha lakini mkandarasi anapaswa kuhakikisha
kuwa anakamilisha dosari zote zilizopo ikiwemo ubovu wa marumaru.
Amesema kuwa haitokuwa kazi
ngumu kwake kufumua uongozi endapo kazi haitaenda vizuri kama ilivyokusudiwa
kwa mujibu wa taratibu za ujenzi na makubaliano katika mkataba wa ujenzi.
Kadhalika Waziri Mkenda
amesisitiza kuwa wanafunzi wanaosoma kozi zinazohusu uvuvi wanapaswa
kufundishwa kwa vitendo na kupewa kazi za mara kwa mara za kwenda baharini kwa
ajili ya kujifunza uvuvi kwa vitendo.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment