METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, May 29, 2017

Mradi wamaliza migogoro ya vijijini Ulanga

VIJIJI 19 vilivyopo katika Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro vimefanikiwa kumaliza migogoro ya kugombea mipaka baada ya Mradi wa Uwezeshaji Umilikishaji Ardhi (LTSP) kupitia wataalamu wa ardhi kuweka alama za upimaji.

Vijiji hivyo vilikuwa na migogoro ya mipaka kwa zaidi ya miaka 10 kwa kijiji kimoja kuingilia kingine na kwamba baada ya kupimiwa ardhi yao, waliwekewa alama za upimaji (bikoni). Ofisa Ardhi Mteule wa Wilaya ya Ulanga, Valence Huruma alisema haya wakati akizungumzia utekelezaji wa mradi huo wa LTPS.

Alisema walibadili mfumo wa upimaji ardhi kutoka ule wa kuweka alama bikoni kila baada ya kilometa tano hadi 10, na kuweka bikoni kwa kila mita 50 ya mpaka ambazo ni ndefu zisizoweza kupoteza alama ya mpaka.

“Awali tulifanya upembuzi wa kupata taarifa za msingi kujua hali ya umiliki ardhi na baada ya mradi kuisha utasaidiaje. Tulipima vijiji 19 hivi vilikuwa na mgogoro kwa muda mrefu na baada ya kuweka mipaka hakuna migogoro tena,” alisema Huruma na kuongeza kuwa alama za upimaji wanazoweka katika mipaka ni za kisasa ambazo haziwezi kupoteza alama ya mpaka kwa hali yoyote.

Alisema kutatuliwa kwa migogoro ya mipaka kwa vijiji hivyo kumechangiwa na ushirikishwaji wa wananchi ambapo katika uwekaji wa alama za mipaka, viongozi kutoka vijiji viwili vinavyogombana husaini kwa pamoja na kuridhia kuwekewa mipaka.

Alisema hii ni tofauti na awali ambapo upande mmoja wa kijiji chenye mgogoro ndio uliosaini ili kuwekewa alama za mipaka hali iliyokuwa ikisababisha migogoro inapotokea kushindwa kutatuliwa kwa urahisi. Alisisitiza uwepo kwa migogoro hiyo unachangiwa na mfumo usiokuwa rasmi wa kuanzisha vijiji bila ya kupanga maeneo ya matumizi.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com