METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, April 10, 2017

SERIKALI YA TANZANIA NA UTATA WA SUALA LA URAIA PACHA

Na Mwandishi wetu, Vijimambo Blog

Nianze kwa kukusabahi wewe msomaji wangu, nikitumaini upo mzima wa afya kwa uwezo wake Mola.

Nakukaribisha tena katika makala nyingine, na hii ya leo itazungumzia suala la uraia pacha. Hili ni suala ambalo kwa mtazamo wangu, Watanzania waliochukua uraia wa nchi nyingine wamekatishwa tamaa na namna serikali ya nchi yao inavyolipuuzia, licha ya kuwa ni suala muhimu na lenye faida kubwa kwa taifa letu.

Viongozi wengi sio kwamba hawaelewi umuhimu wake bali wanafanya jitihada za makusudi za kuwatia uoga na kukataa kuwaelimisha ndugu zetu WaTanzania juu ya faida ambazo nchi itapata kutokana na ndugu zao ambao waamehamishia maisha na kuchukua uraia nje ya nchi. Kuna sababu mbalimbali za waTanzania hawa kufikia maamuzi haya, lakini sote tunatambua kwamba sababu kuu ni moja tu, kutafuta maisha, kitu ambacho hakina tofauti na mtu aliyetoka kijijini na kuhamia mjini.

Viongozi wetu wamekua mstari wa mbele kuwaita WaTanzania wenzao waliokwenda ughaibuni kutafuata maisha, na wengine kulazimika kuchukua ukaazi wa huko kutokana na kubanwa na sheria kuwa WAMEJILIPUA, ilhali tunatambua kuwa lengo ni kuweza kurejesha matunda ya ukaazi huo nchini Tanzania.

Neno kujilipua tafsiri yake hasa ni mtu aliyejifunga bomu na baadae kujilipua ili afe. Hiyo ndio maana yake halisi na kwa viongozi wetu kufananisha mtu aliyebadili uraia na mfu, inasikitisha.
Binafsi napinga kuhusishwa kwa tafsiri hiyo na kinachofanywa na WaTanzania sisi, kwa sababu mtu aliyekufa hawezi kutoa huduma yeyote kwa jamii. Watanzania waliobadili uraia wanasaidia sana ndugu zao nyumbani na kuwakumbusha tu viongozi ni kwamba, uraia anaopewa mTanzania ni wa karatasi kamwe hautaweza kufuta nchi aliyozaliwa.

Katika uongozi wa awamu ya Nne Rais mstaafu Mhe. Jakaya Kikwete alishawahi kutamka na kutoa mwamko wa WaTanzania waliopo nje warudi nyumbani kuwekeza na hii ni kutambua umuhimu wake na sio kwamba alikua haelewi sheria inasemaje kwa mTanzania anayebadili uraia. Naamini Rais alisema vile kwa kuwa aliona umuhimu wa WaTanzania wanaoishi nje ya Tanzania na kwamba alijua wanaweza kutumia ujuzi na maarifa ya Dunia ya kwanza katika kuletea maendeleo ya nchi yetu.

Rais mstaafu Kikwete alijitahidi kukutana na WaTanzania kila nchi aliyoenda na kuwapa ujumbe wa kutosahau kuwekeza nyumbani na wakati Fulani alinukuliwa akisema " WaTanzania Diaspora na WaTanzania mliobadili uraia wote ni jamii moja, rudini nyumbani mkawekeze. Ni fedheha unakaa huku ukirudi unafikia hoteli kule ni nyumbani hata kama huna fedha nyingi za kuwekeza, jenga hata kibanda"

WaTanzania wengi waliitikia wito huo na kuanza kupeleka vitega uchumi nyumbani na wengine kujenga nyumba pasipo kufikiria ipo siku wataitwa WaTanzania waliojilipua au kuukana uraia wa nchi yao. Kwa mimi binafsi, meneno hayo hayapaswi kutumiwa kwani yanapandikiza na kujenga chembechembe za chuki na WaTanzania wengine kuona kwamba WaTanzania wenzetu kwanza hawaitaki nchi yao na sasa wanarudi kuomba uraia pacha kusudi wale huku na kule.

Binafsi naamini kuna faida kubwa sana za raia wa nchi husika walio nje ya nchi kushiriki maendeleo kwa uhuru na bila hofu. Nchi kama Kenya, Sudan, Ethiopia na nyingine barani Afrika ni mfano tosha. Na naamini faida za hili ni kati ya sababu zilizopelekea nchi karibia zote jirani zinazotuzunguka kuruhusu uraia pacha. Kwanini inakuwa ngumu kwetu sisi ambao tunaungana na nchi hizo lakini tunatengana na wazawa wetu? Kwani tunaona ugumu gani?

Wenzetu Kenya wamejiwekea lengo la mwaka 2017- 2018 wakusanye kodi ya Kshs 300 bilioni ambayo ni sawa na $3 bilioni kutoka kwenye uwekezaji unaofanywa na Diaspora wa Kenya nchini humo. Serikali yetu ikiamua kufuatilia fedha zinazoingia Tanzania kutoka Diaspora na kuzitoza kodi ambayo kodi hiyo inaweza kutumika kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo.

Sasa wakati umefika kwa viongozi kuwaelimisha au kuwaambia wananchi ukweli kuhusu uraia pacha na faida zake, badala ya kuwapotosha na kuwatisha kwa kauli kama “tukiruhusu uraia pacha siku moja nchi nii itakuja kutawaliwa na Rais mzungu"?
Kwanini wananchi pia wasiambiwe “tukiruhusu uraia pacha nchini itapata Madaktari, Wahandisi, Wawekejazi WaTanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo wanamichezo wa KiTanzania watakaoamua kuja kuiwakilisha nchi yao katika mshindano ya kimataifa na hatimae kuliletea Taifa sifa”?.

Pamoja na kuchukua uraia wa nchini nchingine mbona inapotokea hitaji la misaada, WaTanzania hao hao wanaowaitwa wameukana uraia wanaipeleka Tanzania, na viongozi wanaipokea kwa mikono miwili?

Misaada mingi itolewayo na diaspora kama vile Madaktari, vifaa mbalimbali vya mahospitalini, mashuleni mitambo ya kuchimbia visima na kadha wa kadha yote ni kuonyesha mapenzi makubwa waliyonayo na nchi yao walikozaliwa.

Hizo ni faida chache mbali na fedha zinazoingizwa nchini kutoka Diaspora ambazo hazina idadi kwasababu hakuna ufuatiliaji wa fedha hizo.

Tunaomba Viongozi wetu mlifikirie upya swala hili kwa faida ya Taifa letu na kwa mwendo kasi wa Rais wetu Mhe. John Pombe Magufuli ingekua vizuri kuwashirikisha WaTanzania nje ya nchi ili kusaidiana na ndugu zetu nyumbani ili wachangie nguvu ya kuleta maendeleo ya nchi kwa kasi zaidi.

Hainingii akilini unamyang'anya uraia mTanzania mwenzako aliyechukua uraia nchi nyingine hafafu unampa uraia mwananchi wa nchi ngingine hii sio sawa hata kidogo inabdi tukae chini na kuliangalia upya swala hili. Hii sheria ilitungwa 1995 ya Immigration Act and Citizenship Act  hii ni 2017 ni zaidi ya miaka 10 tangia kutungwa kwke tunaomba iangaliwe upya iendane na muda uliopo kwa manufaa ya nchi yetu.

Kwa pamoja, walio nyumbani na ugenini, tutaijenga Tanzania njema, Tanzania bora, Tanzania ya viwanda ambayo serikali inaitaka, na wazawa wake walio nje wanaishi na kutumika vilipo viwanda

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Diaspora
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com