METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, April 30, 2017

SALA YA KUMALIZA MSIBA WA MZEE KAYOMBO YAFANYIKA KIJIJINI MISASI-MWANZA

Na Mathias Canal, Mwanza

Misa ya shukrani na kumaliza Msiba (HITMA) wa Marehemu Mzee Antony Raphael Kayombo imefanyika Jumamosi April 29, 2017 nyumbani kwa Marehemu Kijiji cha Misasi, Wilaya ya Misungwi, Mkoani Mwanza kwa kuambatana na sala ya kuwaombea marehemu wote waliofariki duniani katika ukoo huo na jamii kwa ujumla.

Marehemu Mzee Kayombo aliugua ugonjwa wa kibofu cha mkojo ambao ulianza ghafla tarehe 29/1/2017 na kupelekwa katika Hospitali ya Misasi, Baadae hospitali ya Mkoa wa Mwanza  (SEKOU TURE) na mwishowe Hospitali ya Bugando alipofanyiwa upasuaji ambapo hata hivyo hali yake iliendelea kudhoofika mpaka mauti ilipomkuta tarehe 4/2/2017 majira ya saa mbili usiku.

Zikiwa zimepita zaidi ya wiki sita Tangu Marehemu Mzee Kayombo  kuhifadhiwa katika nyumba yake ya milele (kaburini) kumekuwa na ibada na maombi mbalimbali kwa Familia, Ndugu, Jamaa na Marafiki  ya kumtakia heri na fanaka katika Maisha yake mapya ya mauti sambamba na ibada ya mwisho ya kumaliza msiba na matanga iliyofanyika Mwishoni mwa Mwezi Aprili 2017.

Akizungumza katika Ibada ya Sala ya Kumaliza Msiba (Arobaini) Padri Onesphory Lazaro Kayombo kutoka Shirika La Kidini la Precious la Jijini Dar es salaam amewataka wakristo na waamini wa dini mbalimbali kuwapenda majirani zao wanaoishi nao kila siku kwani kufanya hivyo ni njia sahihi ya kumjua na kumpenda  Mungu.

Padri Onesphory alisema kuwa binadamu wote wanapaswa kumpenda Mungu katika Roho na kweli na kutenda yaliyo mema hapa duniani ili watakapofariki waweze kuwa na safari njema katika Maisha mapya ya Mauti.

"Mzee Wetu amefariki lakini ameacha alama kubwa Duniani ambayo inapaswa kuigwa na jamii nzima, ameacha familia ikiwa katika umoja na mshikamano, hivyo mnapaswa kuendeleza upendo mlionao na kusaidiana kama mlivyofanya wakati wote wa Maisha ya Marehemu Mzee wetu mpaka alipoitwa na kuitika" Alisisitiza Padri Onesphory

Akizungumza kwa niaba ya Familia Mjukuu wa Marehemu Mzee Kayombo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo alisema kuwa anaamini katika matendo mema hapa Duniani, Babu yao ametangulia na kuacha pigo kwa familia na kwa jamii yake lakini hakuna namna kila mtu ana kila sababu ya kupokea kifo hicho kama jambo la ukamilifu wa Maisha ya Binadamu japo halizoeleki.

Alisema kuwa kwa kuwa safari ya kifo ni ya kila mmoja hivyo familia imepokea kifo hicho kama safari ya mwisho kwa Mzee wao lakini inaendelea kumuombea ili aishi maisha ya amani huko alipo.

MD Kayombo amewashukuru wananchi wote kwa kushirikina na familia katika kipindi cha kuuguza mpaka kifo cha Marehemu Mzee Kayombo.

Amewashukuru pia viongozi mbalimbali walioshirikiana na familia kumuuguza Mzee Kayombo mpaka kifo chake ambapo ni pamoja Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu  aliyeambatana na mkewe, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Mkurugenzi wa Jiji La Mwanza, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Meya wa Manispaa ya Ubungo, Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, pamoja na Viongozi mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mwanza na Taifa.

MUNGU AILAZE MAHALA PEMA PEPONI ROHO YA MAREHEMU MZEE ANTONY RAFAEL KAYOMBO. AMENI

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com