METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, July 31, 2017

CHADEMA YAENDELEA KUPOTEZA WAKATI CCM IKIVUNA.

Chama Cha Demokrasi na Maendeleo (CHADEMA) kimezidi kupoteza madiwani wake baada ya diwani wa Viti maalum (CHADEMA) kutoka wilaya ya Ngorongoro, Manda Ngoitika kujiuzulu nafasi yake hiyo ya udiwani kwa kile anachodai kuvutiwa na utendaji wa serikali.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Bwana Raphael John Siumbu amesoma barua hiyo ya diwani huyo katika kikao cha baraza la madiwani na kusema ataitaarifu Tume ya Uchaguzi kwa ajili ya utekelezaji wa mwingine.

"Najiuzulu kwa hiyari yangu nafasi ya udiwani viti maalum kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, aidha maamuzi haya nimeyachukua baada ya kuridhishwa na uongozi wa awamu ya tano na utendaji wake, kutetea na kusimamia haki na maslahi ya wanyonge", alisoma barua hiyo Raphael John Siumbu.

Hata hivyo diwani huyo wa CHADEMA alipewa nafasi ya kusema chochote ndipo aliposema kuwa atatoa ushirikiano wa kutosha kwa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi na serikali kwa ujumla.
"Nitashirikiana na kila mmoja wenu, nitashirikiana na serikali iliyopo madarakani" alisema Manda Ngoitika.

Manda Ngoitika amekuwa diwani wa kwanza kujiuzulu nafasi yake ya udiwani kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilayani Ngorongoro mkoani Arusha
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com