Na Mathias Canal, Dar es salaam
"Hivi inawezekanaje MTU akamatwe na Dawa za Kulevya halafu achekewe, Mtu akamatwe na Meno ya tembo halafu achekewe, Mtu afanye ubadhilifu wa Mali za Umma halafu achekewe, Naamini hakuna Taifa la Namna hilo....?"
Ni kauli ya Waziri wa Mambo ya ndani Mhe Mwigulu Lameck Nchemba akizungumza na Mamia ya watu waliojitokeza kwenye kusanyiko la ibada kupitia nyimbo za injili (Tamasha la Pasaka 2017).
Mhe Mwigulu alisema kuwa watanzania wamekuwa wakipotoshwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli amekuwa kiongozi mkali kuliko viongozi wote waliopita ambapo amewasihi kutambua kuwa Rais anawajibika kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na amekuwa kiongozi mwenye uchungu na Watanzania Wanyonge ambao wamekuwa wakikandamizwa na wabadhilifu wachache ambao ni wezi wa Mali za watanzania.
"Hivi naomba niulize mnapoomba kumkemea Shetani atoke huwa mnamuomba kwa unyenyekevu tena mkimbembeleza au huwa mnamkemea kwa Ukali...? Kama huwa mnamkemea shetani kwa ukali ndivyo basi hata wabadhilifu katika nchi yetu wanapaswa kukemewa kwa ukali maana hakuna kiongozi wa serikali tena nafasi ya kiongozi namba moja katika Taifa ambaye hukemea Uovu kwa upole ni lazima awe mkali" Alisema Mwigulu
Alisema Rais ametangaza mabadiliko makubwa nchini, Amerejesha nidhamu na uwajibikaji serikalini, anabana matumizi kwa manufaa ya watanzania wote hivyo mabadiliko hayo aliyoyafanya imekuwa ni Vita kubwa kwa watu wasio wema katika Taifa letu hivyo tunapaswa kumuombea kwa dhati ili dhamira yake njema iweze kufanikiwa.
Mwigulu alisema tunapaswa Kujenga nchi kwa pamoja na sio kubomoa na amewasihi baadhi ya wananchi wanaopotosha kuhusu utendaji wa serikali kuwa wanapaswa kujiridhisha kwa kupata walau taarifa kidogo kuliko kupotosha kwa makusudi ama bahati mbaya.
Alisema kuwa kumekuwa na masharti magumu ya usajili wa nyumba za ibada ilihali kuna masharti rahisi kwa wanaosajili nyumba za Starehe kama Baa na kumbi za Disko hivyo amewaagiza wasaidizi wake kusimamia urahisi wa kusajili nyumba za ibada kwa masharti rahisi ili kila MTU awe na Uhuru wa kuabudu kwa imani yake.
"Kwa bahati nzuri Wizara yangu ndio inahusika Na Taasisi za dini hivyo tunatoa Uhuru wa kuabudu kwa mujibu wa sheria lakini Uhuru huo haupaswi kuwakwaza wengine, Kuchonganisha ama kuvunja Sheria" Aliongeza Mwigulu
Akijibu risala iliyoandaliwa na Kampuni ya Msama Promotion ltd ambao ndio waandaaji wa Tamasha la Pasaka nchini iliyoelezea kuhusu wizi wa kazi za wasanii sambamba na kulipishwa gharama kubwa za kodi pale wanapowaalika wasanii kutoka nje ya nchi Mhe Mwigulu alisema kuwa Wizara yake kwa kushirikiana Na wizara inayohusika moja kwa moja Na sanaa watashughulikia ubadhilifu wote unaofanywa dhidi ya kazi za Sanaa Na kuwachukulia hatua za kisheria wezi wa kazi hizo.
Mhe Mwigulu Nchemba pia amezindua Albamu ya msanii Rose Muhando ijulikanayo kama JITENGE NA RUTHU, sambamba Na kuzindua Albamu ya NGOME ZIMEANGUKA iliyoimbwa na Kwaya ya Kinondoni Revival Choir ya kanisa la Tanzania Assemblies Of God (TAG).
Tamasha la Pasaka linaloandaliwa na Kampuni ya Msama Promotion chini ya Mwenyekiti wake Ndg Alex Msama limekuwa na mafanikio makubwa kwani wakati linaanza mwaka 2000 wahudhuriaji walikuwa 700 huku wasanii nane pekee wakitumbuiza kwenye Tamasha hilo lakini miaka 17 baadae limefikia uwezo wa kualika zaidi ya wasanii 25 huku zaidi ya wahudhuriaji 400,000 wakishuhudia Tamasha hilo kila mwaka katika kipindi cha miaka 10.
Wasanii mahiri wa nyimbo za injili barani Afrika ambao wamewahi kutumbuiza katika Tamasha la Pasaka ni Rebecca Makope, Solly Mahlangu, Sipho Makabane wa Afrika Kusini, Ephrahim Sedekia wa Zambia, Anastazia Mukabwa, Solomon Mukubwa wa Kenya, Kwetu Pazuri (Rwanda), Faraja Ntaboba wa DR Congo na wengine wengi.
Kampuni ya Msama Promotion pamoja na kuandaa Tamasha la Pasaka lakini pia inajihusisha na kutoa misaada pasina kuchagua dini Bali kwa kutazama uhitaji kwa kusaidia yatima, Wajane, Wazee na Wengine wenye uhitaji.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment