METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, April 25, 2017

KUPATIKANA NA DAWA ZIDHANIWAZO KUWA ZA KULEVYA

Image result for jeshi la polisi
TAARIFA YA JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA KWA VYOMBO VYA HABARI “PRESS RELEASE” TAREHE 24.04.2017.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kufanya misako, operesheni na doria zenye tija katika maeneo mbalimbali ili kudhibiti uhalifu na wahalifu na limekuwa likishirikiana na wananchi na wadau wengine katika jitihada hizo za kukabiliana na uhalifu na wahalifu na kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupungua kwa matukio makubwa ya uhalifu.

Mnamo tarehe 21.04.2017 majira ya saa 21:45 usiku huko maeneo ya Mashineni – Mwanjelwa, Kata ya Mangaa, Tarafa ya Sisimba, Jiji na Mkoa wa Mbeya, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya liliendesha msako katika maeneo hayo na kufanikiwa kumkamata mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la RASHID SHABAN [35] Mkazi wa Sinde akiwa na dawa zidhaniwazo kuwa za Kulevya aina ya Heroine kete 05 ambazo mtuhumiwa alikuwa amehifadhi ndani ya mifuko ya nailoni.

Mtuhumiwa ni msambazaji na mtumiaji wa dawa hizo, upelelezi unaendelea.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya pia linaongeza jitihada za kuzuia na kupunguza ajali za barabarani kwa kuhakikisha madereva na watumiaji wengine wa barabara wanatii sheria za usalama barabarani. Aidha kumekuwa na tukio 01 la ajali ya kifo kama ifuatavyo:-

AJALI YA KIFO.

Mnamo tarehe 23.04.2017 majira ya saa 19:30 usiku huko eneo la Ntokela lililopo katika kata ya Ndanto, Tarafa ya Ukukwe, Wilaya ya Rungwe Mkoa wa Mbeya barabara kuu ya Tukuyu kuelekea Mbeya, Pikipiki yenye namba za usajili MC 762 AWN aina ya GSM iliyokuwa ikiendeshwa na dereva ambaye bado hajafahamika jina lake aliyekimbia mara baada ya ajali ilimgonga mtembea kwa miguu mtoto aitwaye PROMISE HAKIMU [05] Mkazi wa Ntokela na kumsababishia kifo chake papo hapo.

Chanzo cha ajali ni mwendo kasi wa dereva wa pikipiki. Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Igogwe. Juhudi za kumtafuta mtuhumiwa zinaendelea kwani baada ya kusababisha ajali alikimbia.


Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kukabiliana na matukio makubwa ya uhalifu pamoja na wahalifu. Jitihada zinaendelea kwa kushirikiana na wananchi kuhakikisha Mkoa wetu unakuwa mahala salama. Kumekuwa taarifa 01 ya kifo kama ifuatavyo:-

Mnamo tarehe 23.04.2017 majira ya saa 11:30 asubuhi huko Kitongoji cha Itunge kilichopo Kata ya Itunge, Tarafa ya Unyakyusa, Wilaya ya Kyela, Mkoa wa Mbeya, Mtoto mdogo mwenye umri wa mwaka mmoja aliyefahamika kwa jina la SAMIR SHOMARI jinsi ya kiume na Mkazi wa Itunge alikutwa amekufa maji baada ya kutumbukia kwenye mfereji wenye maji mengi.

Inadaiwa kuwa chanzo cha kifo ni mtoto huyo kutumbukia kwenye mfereji unaopitisha maji mengi na kusababisha kifo chake. Aidha wakati tukio hilo linatokea, marehemu alikuwa akicheza na watoto wenzake na hapakuwa na uangalizi wa mtu mzima.   

WITO:

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu Kamishina wa Polisi DHAHIRI A. KIDAVASHARI anatoa wito kwa wazazi/walezi kuweka uangalizi wa kutosha kwa watoto ili kuepuka madhara yanayoweza kuwapata watoto hasa katika msimu huu wa mvua zinazoendelea kunyesha. Aidha Kamanda KIDAVASHARI anatoa wito kwa madereva kuwa makini kwa kuzingatia na kufuata sheria na alama za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazoepukika. Aidha watumiaji wengine wa barabara kuwa makini na matumizi ya barabara ikiwa ni pamoja na kuvuka maeneo yenye vivuko vya kuvukia.

Imesainiwa na:
 [DHAHIRI A. KIDAVASHARI - DCP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA


Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com