Kasi
ya kupambana na ujangili iliyoongezwa na Rais John Magufuli imeendelea
kuzaa matunda huku Kikosi Kazi Maalum kilichoundwa kikiripotiwa kukamata
bunduki 11 nyumbani kwa mbunge.
Kwa
mujibu wa chanzo cha gazeti la Mwananchi, Bunduki hizo zinazosadikika
kutumika katika matukio ya ujangili zilikutwa nyumbani kwa mbunge wa CCM
ambaye jina lake limehifadhiwa kwa sababu za kutoingilia unyeti wa
oparesheni hiyo.
Taarifa
hizo zimekuja ikiwa ni siku chache baada ya Rais Magufuli kufanya ziara
ya kushtukiza katika Ofisi za Maliasili na Utalii na kukipa nguvu zaidi
kikosi kazi hicho ambacho kilidaiwa kuanza kuzimwa.
Rais
Magufuli alimtaja mtu mmoja kwa jina la ’Mpemba’ anayehusishwa na
biashara haramu ya pembe za ndovu kwa muda mrefu na kueleza kuwa
angeshangaa kama asingekamatwa. Alishuhudia meno 50 ya Tembo ambayo
yalikamatwa kutokana na oparesheni hiyo, hali inayoonesha kuna tembo 25
waliuawa.
Naye
Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe juzi alieleza
kuwa tayari wameshamtia nguvuni Mpemba na kwamba wanaendelea na msako wa
wengine ambao wakikamatwa nchi itatikisika kutokana na majina yao.
”Hilo
ni jina lake analolitumia katika harakati zake za biashara ya ujangili
ili asitambulike. Yuko mwingine pia anajiita ’Mangi wa Kabila fulani’
lakini sio majina yao halisi,” alisema Profesa Maghembe na kuongeza kuwa hawaweki hadharani majina yao ili kutoharibu uchunguzi.
Profesa
Maghembe aliwahakikishia Watanzania kuwa mtandao wote wa majangili
utavurugwa na hakuna jangili atakayesalimika bila kujali jina lake.
Hivi
karibuni, Rais Magufuli alimteua Mkuu wa Majeshi wa zamani, Jenerali
George Waitara kuwa Mwenyekiti wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa),
ambaye ameahidi kuwakomesha wafanyabiashara hao haramu.
0 comments:
Post a Comment