WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali imewaagiza Makamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) nchini wahakikishe wanawakamata na kuwachukulia hatua watu wote watakaojihusisha na vitendo vya rushwa kuelekea uchaguzi mkuu.
“Watu wamezoea vitendo vya rushwa kwenye uchaguzi, Serikali tumeagiza kwa kamati za ulinzi na usalama zishirikiane kuhakikisha kwamba hakuna vitendo vya rushwa katika uchaguzi na yeyote ambaye anajihusisha na rushwa asiachwe.”
Alitoa kauli hiyo jana jioni (Jumamosi, Juni 20, 2020) wakati akizungumza na viongozi wa mkoa wa Lindi mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Nachingwea akiwa njiani kuelekea wilayani Ruangwa kwa ziara ya kikazi.
Waziri Mkuu alisema kitendo cha kutoa na kupokea rushwa ni kosa, hivyo viongozi hao wa TAKUKURU nchini hawana budi kuwachukulia hatua watu wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo.
Vilevile, Waziri Mkuu amewataka Makamanda wa TAKUKURU katika wilaya zote nchini wahakikishe wanawakamata watu wote watakaojihusisha na vitendo vya rushwa wakiwemo na wapambe ambao ndio wachochezi wa vitendo hivyo.
Waziri Mkuu alitoa maagizo hayo ili kuhakikisha uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu unakuwa huru na wa haki, hivyo kuwawezesha wananchi kuchagua viongozi wanaowahitaji na si kwa msukumo wa rushwa.
Katika hotuba yake aliyoisoma Juni 15, 2020 bungeni jijini Dodoma wakati akihitimisha mkutano wa 19 wa Bunge, Waziri Mkuu aliwataka viongozi wa vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi wazingatie katiba, sheria, kanuni na miongozo iliyopo katika uendeshaji wa shughuli za uchaguzi.
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwasihi viongozi na wanachama wa vyama vyote vya siasa na wananchi kwa ujumla waendelee kulinda amani na kuendeleza mshikamano katika kipindi hiki na wakati wa uchaguzi Mkuu.
Mapema asubuhi jana Mheshimiwa Majaliwa alikweda Zanzibar ambako alishiriki katika tukio la Kuvunja Baraza la Wawakilishi liliyofanywa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein kwenye ukumbi wa Baraza hilo. Pia tukio hilo lilihudhuliwa na Spika wa Bunge Job Ndugai.
0 comments:
Post a Comment