HUU NDIO UHALISIA WA MAISHA YA UGHAIBUNI NINAO UFAHAMU MIMI
Na Mwandishi wetu, Vijmambo Blog
Kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia siku nyingine tena na nimatumaini yangu upo vizuri tu na mchaka mchaka wa kila siku.
Leo napenda nizungumze na wewe au nikumegee machache kuhusu uhalisia wa maisha ya ughaibuni ambayo kama leo utabahatika kwenda ughaibuni basi ujue huku ni kazi tu na sio kweli kwamba pesa inadondoka kutoka kwenye mti kama yalivyo mawazo ya vijana wengi wanaokimbilia nje kwa ajili ya kutafuta maisha na baadae maisha yanageukia kuwa majanga.
Mimi mwenyewe nilikua na mawazo kama ya kwako na ya vijana wengi wanavyofikiria ughaibuni ni kuku tu, ni kweli kwa wakati mwingine ikilinganisha masikini wa Dunia ya kwanza thamani ya maisha ya masikini wa Dunia ya tatu ni tofauti na jambo la kwanza ambalo ndio vijana wengi ulitizama ni mwonekano wa vijana wanaorudi likizo Tanzania akiwa ameng'aa juu mpaka chini kila kitu kipya wala hakijakanyaga vumbi
Siri kubwa ya nyuma ya pazia vitu hununuliwa mtu anapojiandaa kusafiri kuelekea Tanzania lakini anapokuwepo ughaibuni katika maisha yake ya kila siku mwonekano wake ni mtu wa kawaida hasa katikati za wiki maisha ni ya kawaida sana na hasa kwenye pamba wewe wa Bongo unang'aa zaidi yake. Na hii nazungumzia Mbongo wa ughaibuni wa hali ya kawaida sio mbongo aliyebahatika akaenda shule na kazi yake nzuri ya ofisi.
Kama kijana ukibahatika kwenda ugaibuni kwa masomo au kitu kingine kilichokuleta kwanza jua maisha ya ughaibuni ni mchakamchaka mno, ughaibuni siku, miezi hadi miaka inakimbia kupita kiasi hii ni kwa sababu maisha ni mbio mbio unakuta mtu anafanyakazi 1- mpaka 4 kutokana na uhitaji wa maisha aliyoyachagua, ukichagua kuishi kifahari maisha yako yatakua ni mateso ya kazi kwa sababu ya uweze kumudu gharama za maisha uliyojichagulia. Kama nilivyosema hapo awali kama umebahatika kuja kwa masomo au chochote kilicho kupeleka tafadhali jikite nacho mara nyingi vijana wengi wameharibu nafasi zao za masomo kutokana na kuhadaika na watu waliokutana nao au kwa lugha nyepesi waliowapokea.
Kama utapata mwenyeji mzuri atakae kujali atakuongoza vizuri lakini wakati mwingine unakutana na wenyeji wenye roho mbaya wao wameharibikiwa na wao wanataka na wewe uharibikiwe, watu kama hawa wapo sana tu ughaibuni kwa hiyo kabla hujatumbukia kichwa kichwa ongea na watu wawili watatu wengine usikie nao maoni yao ili nayo uyaweke kwenye mizani.
Dunia ya sasa imebadilika Ugaidi umebadilisha sheria nyingi ughaibuni tafauti na miaka ya iliyopita, maisha yamezidi kuwa magumu tofauti na miaka ya nyuma, ughaibuni ya zamani sio ya sasa kwa hiyo kabla hujasafiri usikurupuke kaa chini ufikirie mara mbili, jitathmini na ujiridhishe angalia maisha uliyonayo nyumbani, jiulize je nina nyumba au pakulala?, je nina gari au nauli ya kwenda kokote nakotaka?, je nina kazi au biashara?, je nina lala njaaa? kama kila kitu hapo na vitu vingine upo powa ughabuni wewe sio kwa kukimbilia labda kama umepata shule kupanua elimu hapo sitakua na kipinganizi na wewe.
Kwa wadau wa ughaibuni tusiridhike na mafanikio tuliyofikia daima tupende kujiendeleza na hii ipo tangia nyumbani tunarizika sana na maisha tuliyonayo, inabidi tuwe na wivu wa maendeleo. Unaweza kufanyakazi pamoja na makabila mengine wewe utajikuta miaka 10-15 upo pale pale mataifa mengine miaka hiyo aishapanda cheo.Kama kuna uwezekano nenda shule na jiwekee malengo kila baada ya miaka fulani unataka ufike wapi.
Michongo inapotokea jambo la maendeleo au manufaa ni vizuri kupeana fursa na mwenzako kama mataifa mengine yanavyofanya, hii ni muhimu kwa maendeleo ya familia na jumuiya zetu katika sekta mbalimbali ikiwemo nchi yetu itanufaika.
Inapotokea majanga ya misiba kwa wale wasiokua na bima, mara nyingi inakua vigumu hasa kama ulikua mtu usiyejichanganya na yote ni kwa sababu kuu moja ya hatujajiandaa kufia ughaibuni kwa sababu tumeweka kwenye fikra zetu tumekuja kuchuma na ipo siku tutarudi nyumbani. Mawazo ni mazuri lakini usisahau dhamana ya maisha yako ameishikilia Mwenyezi Mungu yeye ndiye anayejua kesho utakua wapi, tujitahidi japo uwe na bima ya maisha hii itasaidia kuondoa matatizo kwako na jamii.
Naona niishie hapo kwa leo tukutane wiki ijayo
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Diaspora.vv
0 comments:
Post a Comment