Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Dunia ya sasa inapigania haki sawa kwa
wanaume na wanawake ili waweze kushiriki kwa pamoja kwenye nyanja zote
za kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa ajili ya kuchangia kwenye ukuzaji wa
pato la taifa na kupelekea kukua haraka kwa maendeleo ya nchi.
Tumeshuhudia wanawake wengi nchini
wakijikita katika kufanya biashara na ujasiriamali wa bidhaa na huduma
mbalimbali ambazo zinawakomboa kiuchumi na kuwafanya waweze kujitegemea
kama walivyo wananume.
Wanawake hao waliojiamini na kuamua
kuanzisha biashara zao wameonekana kuwa na mafanikio makubwa ambayo
yanasaidia kuinua uchumi wa mtu binafsi na wa nchi kwa ujumla.
Kwa upande mwingine, baadhi ya wanawake
wamekua bado hawana ujasiri wa kuanza kufanya ujasiriamali kwa kuhofia
kuwa hawataweza kuendelea na wengine wakihofia waume zao kuwakataza.
Dhima ya kujirudisha nyuma waliyonayo
baadhi ya wanawake ndio inayorudisha nyuma hata maendeleo ya nchi hasa
kwa wakati huu ambao Serikali ya Awamu ya Tano imeamua kujikita katika
kukuza uchumi wa viwanda.
Serikali inafanya jitihada mbalimbali za
kuwahamasisha wanawake kufanya ujasiriamali hivyo kupitia Benki ya
Wanawake, Serikali imeendelea kutoa huduma za mikopo kwa wajasiriamali
wanawake nchini ili kuhakikisha wanapata mitaji ya kuanzishia shughuli
hizo ambazo baadae zinakua ni mkombozi wa maisha yao.
Katika kipindi cha 2009 hadi 2014, Benki
ya Wanawake imetoa jumla ya mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni
24.9 kwa wananchi 12,992 wakiwemo wanawake 11,350 ambayo ni sawa na
asilimia 87.
Aidha, katika kuwawezesha wanawake
kiuchumi na kuinua hali zao kimaisha, Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake
umenufaisha vikundi 3,119 vyenye jumla ya wanawake 23,769.
Idadi ya wanawake waliopata mikopo
kutoka katika Mfuko huo imeongezeka kutoka wanawake 3,008 mwaka 2005
hadi kufikia wanawake 23,769 mwaka 2014.
Pia jumla ya Mikoa 25 ya Tanzania Bara
ilipelekewa fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake kwa ajili ya
kuwakopesha wanawake, mikopo hiyo imewawezesha wajasiriamali wanawake
kujiajiri katika shughuli mbalimbali za uzalishaji na hivyo kuinua
kipato chao.
Kwa upande wake Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii ,Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anasema kuwa
jamii inatakiwa kuondokana na dhana ya mfumo dume inayomfanya mwanamke
kukaa bila kufanya shughuli yoyote ya kiuchumi hivyo kuwa mtegemezi kwa
kila kitu hali inayopelekea kushindwa kutoa maamuzi wanayoyataka na
wengine kunyanyaswa.
Hivyo, jamii inatakiwa kuhakikisha
inashirikiana na Serikali pamoja na wadau mbalimbali kuwajengea uwezo
wanawake, kuwapa elimu na kuwapa fursa wanawake kushiriki katika
shughuli za uzalishaji mali zikiwemo za kilimo na biashara mbalimbali.
Ukiondoa mchango wa Serikali katika
kuwasaidia wanawake kujikwamua, wanawake wenyewe kwa wenyewe wanatakiwa
kusaidiana hasa wale walioendelea wanatakiwa kutoa elimu na ushauri kwa
wanawake wenzao ili kila mwanamke afahamu juu ya umuhimu wa ujasiriamali
na jinsi utakavyoweza kumkomboa katika maisha yake ya kila siku.
Pia wanashauriwa kujiunga katika vikundi
vya kusaidiana ili kupeana mawazo mbalimbali ya biashara, kutiana moyo
kwa kuwa siku zote mwanzo wa kitu chochote huwa ni mgumu pamoja na
kusaidiana katika kupeana mitaji itakayowawezesha wajasiriamali kuinuka.
Kufuatia maadhimisho ya Siku ya wanawake
Duniani,wanawake wa Tanzania wamepewa jukumu la kuhakikisha wanajikita
katika ujasiriamali na kushiriki katika kuinua uchumi kupitia viwanda
kwani wanawake ndio msingi wa mabadiliko ya kiuchumi.
0 comments:
Post a Comment