Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza wakati wa mahojiano
maalum na televisheni ya Taifa (TBC) katika maadhimisho ya Siku ya
Wanawake Duniani, nyumbani kwake Makao Makuu ya Nchi Dodoma (Picha na
Ofisi ya Makamu wa Rais)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amelaani na kukemea vikali vitendo vya
ukeketaji wa wanawake na ubakaji vinavyoendelea katika jamii na
amewataka wananchi kote nchini kushirikiana katika kukabiliana na
vitendo hivyo nchini.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo tarehe 8-March-2017
wakati akizungumza katika mahojiano maalum na Shirika la Utangazaji wa
Tanzania (TBC) mjini Dodoma kuhusu maadhimisho ya siku ya wanawake
Duniani.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan
amesema vitendo hivyo vya ukeketaji wa wanawake na ubakaji vinamchukiza
sana hivyo ametoa wito maalum kwa wananchi na wadau wote bila kujadili
dini, kabila wala rangi kupambana ipasavyo na vitendo hivyo ambavyo
vinarudisha nyuma jitihada za kumkwamua mwanamke kiuchumi.
Kuhusu maadhimisho ya Siku ya Wanawake
Duniani, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amesema anafurahishwa na
hatua na jitihada zinazochukuliwa na wanawake kote nchini katika
kujikwamua kiuchumi kwa kuimarisha shughuli zao za ujasiriamali katika
kuelekea katika uchumi wa viwanda.
Amesema jukumu kubwa la serikali ya
awamu ya Tano ni kuhakikisha wanawake wanaboreshewa ipasavyo mazingira
ya kufanyia kazi hasa shughuli za ujasiriamali ili waweze kufikia
malengo waliyojiwekea.
“Inapofika katika shida zetu wanawake ni
lazima tuwe na kitu Kimoja na sauti Moja katika kulinda na kutetea haki
zetu bila kujali itikadi za kisiasa”Amesisitiza Makamu wa Rais.
Katika uundaji wa majukwaa ya
kuwawezesha wanawake kiuchumi nchini, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu
Hassan amesema kazi hiyo inaendelea vizuri na kutaka mikoa na wilaya
ambazo bado haijaunda majukwaa hayo kufanya hivyo haraka iwezekanavyo.
Ameeleza kuwa lengo la uundaji wa
majukwaa hayo katika ngazi ya wilaya na mikoa nchini ni kuwakutanisha
wanawake pamoja katika kujadili na kutafutia ufumbuzi changamoto
zinazowakabili ikiwemo tatizo la masoko za bidhaa wanazozizalisha.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan
amesisitiza kuwa majukwaa hayo ambayo yameanza kuundwa katika mikoa
mbalimbali nchini yatakuwa sio ya kisiasa.
Katika Mahojiano hayo na mtangazaji
Shaban Kissu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) mjini DODOMA,
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu ametumia sehemu ya mahojiano hayo kwa
kuwatakia heri na mafanikio wanawake wote nchini katika kuadhimisha Siku
ya wanawake Duniani.
Kauli mbiu ya mwaka huu ya siku ya wanawake Duniani ni “Tanzania ya Viwanda,Wanawake ni msingi wa mabadiliko ya Kiuchumi”.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
Dodoma.
8-Mar-2017
0 comments:
Post a Comment