METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, March 9, 2017

MKUTANO WA LAPF WAANZA LEO JIJINI ARUSHA WAZIRI MKUU KUUZINDUA KESHO MACHI 10, 2017

 Waziri mkuu wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe Majaliwa Kassim Majaliwa
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe Mrisho Gambo (Kushoto) akizungumza na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo Ndg John Kayombo (kulia) Mara baada ya kuwasili katika ukumbi wa mkutano wa 9 wa Wadau wa Mfuko wa Pensheni LAPF uliofanyika AICC Machi 9, 2017
Naibu Waziri wa TAMISEM Mhe Suleiman Jaffo akisaini kitabu cha wageni
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe Mrisho Gambo (Kushoto), Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo Ndg John Kayomb, Mkurugenzi wa wa Halmashauri ya Wilaya ya Mlele Ndg Alex Kagunze na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Ndg Wakili Magoiga katika picha ya pamoja baada ya kuwasili katika ukumbi wa mkutano wa 9 wa Wadau wa Mfuko wa Pensheni LAPF uliofanyika AICC Machi 9, 2017

Na Mathias Canal, Arusha

MFUKO wa hifadhi ya wafanyakazi wa serikali za mitaa LAPF, umeipongeza serikali kwa kulipa malimbikizo ya madeni ambayo mfuko huo na mingine ilikuwa ikiidai kwa miaka mingi na hivyo kuathiri ustawi wa mifuko hiyo.

Meneja wa LAPF kanda ya kaskazini, Rajabu Kinande, amesema hatua ya serikali kulipa madeni hayo kumeiongezea mifuko ya hifadhi ya jamii uwezo wa kuhudumia wanachama wao kwa wakati.

Kinande ameyasema hayo kabla ya kuanza kwa kikao cha uwasilishwaji wa mada mbalimbali kwenye mkutano wa wadau wa mfuko wa LAPF ulioanza leo Jijini Arusha katika ukumbi wa AICC alipokuwa akizungumza na mtandao wa www.wazo-huru.blogspot.com kwenye kituo hicho cha mikutano ya kimataifa AICC kuelezea mkutano wa siku mbili wa mwaka wa wadau wa LAPF ulioanza rasmi hii leo Machi 9, 2017 na kutaraji kumalizika hapo kesho ambapo mgeni rasmi atakuwa Mhe Majaliwa Kassim Majaliwa..

Mkutano huo utafunguliwa na Waziri mkuu wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe Majaliwa Kassim Majaliwa Marchi 10 mwaka huu ambapo zaidi ya wanachama 1000 wa mfuko huo wanatarajiwa kuhudhuria.

Akizungumza katika semina hiyo Naibu Waziri wa TAMISEM Mhe Suleiman Jaffo amewasihi watumishi wa umma na binafsi kujiandikisha kwa wingi katika mfuko huo kwani kufanya hivyo ni njia pekee ya mafanikio ya kumuandaa mtumishi yoyote kustaafu akiwa na muelekeo mzuri.

Jaffo alisema kuwa watumishi wanapaswa kuwatumikia wananchi kwa juhudi na maarifa na kufanya kazi bila ubaguzi ili kuwanufaisha wananchi na kufurahia huduma hizo.

Akitoa salamu za mkoa wa Arusha, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe Mrisho Gambo alisema kuwa watanzania wanapaswa kujenga utamaduni wa kuthamini vitu vinavyozalishwa nchini kwani kufanya hivyo ni ustawi wa Tanzania nzima sambamba na kuwataka wananchi kuzuru katika mbuga mbalimbali za wanyama mkoani Arusha ili kuimarisha mapato ya ndani sambamba na kujifunza kuhusu mambo mbalimbali kupitia utalii wa ndani.

Rc Gambo ameupongeza mfuko huo wa LAPF kwa kazi kubwa ya kuitumikia jamii kwani tangu alipokuwa Mkuu wa Wilaya katika Wilaya mbalimbali na hatimaye kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha hajawahi kusikia malalamiko kwa wananchi kuhusu Mfuko huo.

Katika mkutano huo kumewasilishwa mada mbalimbali zikiwemo Uendeshaji wa shughuli za mfuko huo, Hesabu zilizokaguliwa na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali(CAG) za mwaka 2015/16 ambapo mfuko huo umepata hati safi ya ukaguzi wa hesabu , UKusanyaji wa michango ulipaji wa mafao kwa wanachama na uwekezaji, Utawala bora na usimamizi wa uendeshajiwa mfuko huo na Rasilimali fedha .

Nao wadau mbalimbali wa mfuko huo akiwemo Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo akizungumza na Mtandao wa www.wazo-huru.blogspot.com ameupongeza Mfuko wa Penseni wa LAPF kwa kuandaa upimaji wa figo bure kwa wanachama wote ambao unafanywa na Madaktari bingwa kwani umezingatia kuwa Machi 9 Dunia huadhimisha siku ya figo.

MD Kayombo amesema kuwa Mfuko huo wa LAPF umeanza na dhamira hiyo nzuri kwa kuwasaidia wananchi na wadau mbalimbali kupata huduma hiyo ya upimaji bure kwani itawasaidia kupata uelewa wa ugonjwa huo jambo ambalo linawapa urahisi wa kujiandaa kwa kufahamu namna ya kujihudumia na kujitibu kwa wale watakaobainika kuwa wana matatizo kwenye figo zao.

Kesho mkutano huo utafunguliwa rasmi na Waziri mkuu Kassim Majaliwa ambapo pia atazindua Program mpya ya mikopo kwa wanachama kwa kushirikiana na benki ya CRDB, program iitwayo Maisha popote ambao ni mkopo wa kwanza kutolewa na mfuko huo.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni kuibua fursa endelevu za ajira kwa maendeleo endelevu kwa watanzania.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com