MAANDALIZI YA UMISSETA YAENDELEA UBUNGO
Na Nassir Bakari
Maandalizi ya kushiriki michezo kwa shule za sekondari (UMISSETA) yameendelea katika Manispaa ya Ubungo kwa kufanyika kikao kati ya Idara ya elimu Sekondari Manispaa ya Ubungo na walimu wakuu 27 wa shule za serikali na 39 wa zisizo za serikali ( private).
Kakao hicho cha majadiliano kilifanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa shule ya Sekondari Kibamba iliyopo Kata ya Kibamba Manispaa ya Ubungo.
Wakati wa kikao hicho wakuu hao wa shule pamoja na maofisa kutoka Idara ya elimu sekondari walijadili mikakati ya kufanikisha michezo hiyo katika ngazi ya wilaya.
Akizungumza kwa niaba ya walimu wakuu wa shule za umma Mwenyekiti wa UCOSES (Ubungo Community Secondary School) Ndg. Deogratius Haule alisema changamoto ni nyingi lakini watakabiliana nazo.
"Changamoto nyingi kama vifaa vya michezo na washiriki ni wachache lakini tutakabiliana nazo kwani tumejiandaa kushinda" alisema Haule na kuendelea.
"Tunamshukuru sana Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg. John Lipesi Kayombo kwa kuwa nasi bega bega na tunamwahidi ushindi" alisema Haule.
Pia mwakilishi wa shule zisizo za serikali (private) Ndg. Erick Rwegasila alisema kwa pamoja wameazimia kushirikiana bega kwa bega na shule za umma ili kuleta ushindi katika Manispaa ya Ubungo.
0 comments:
Post a Comment