MOHAMED HABIBU MNYAA AFUKUZWA UANACHAMA
Tarehe
7/2/2017 Mkutano Mkuu wa Tawi la Chanjaani, Jimbo la Mkoani wilaya ya
Mkoani-Pemba, umefanya maamuzi ya kumfukuza uanachama wa CUF Mohamed
Habibu Mnyaa kutokana na kukiuka katiba ya chama Ibara ya 12 (6)(7)(16)
kutokana na kuwa na mwenendo usiofaa wa kuwagawa wanachama, kueneza
taarifa za upotoshaji dhidi ya viongozi na Chama, kufanya vitendo vya
hujuma za kutaka kukidhoofisha Chama, kudharau na kushindwa kuhudhuria
na kutoa ushirikiano kwa tawi lake kila alipotakiwa kufanya hivyo.
Mkutano Mkuu wetu wa leo umehudhuriwa na wajumbe halali 112 kati ya
wajumbe wote halali 113.
Wajumbe
wote 112 wamepiga kura za ndio kuazimia kumfukuza uanachama kwa mujibu
na mamlaka ya kikatiba yaliyoelezwa katika katiba ya CUF ukurasa wa 29
ibara ya 18(1)(ix) kuhusu wajibu wa Mkutano Mkuu wa Tawi kama
ilivyoeleza kuwa;
“Kumchukulia
hatua za nidhamu mwanachama au kiongozi yeyote wa tawi hilo, ikiwa ni
pamoja na kumpa onyo, karipio, karipio kali, kumsimamisha uanachama au
uongozi wa Chama kwa muda, na hata kumuachisha au kumfukuza uanachama wa
Chama”
Mohamed
Habibu Mnyaa alijiunga na CUF katika tawi hilo tarehe 28 septemba mwaka
1999 na kukabidhiwa kadi yenye Namba ya usajili 029033. Mohamed ambaye
amewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Mkanyageni kwa muda wa vipindi viwili
2005-2015, amekuwa na mwenendo huo mbaya na usiofaa kwa Chama na
viongozi wake tangu alipokosa ridhaa ya wanachama na Maamuzi ya vikao
vya Chama kumpitisha kugombea kwa mara nyingine tena katika nafasi ya
ubunge mwezi August, mwaka 2015. Mohamed amefukuzwa uachachama akiwa ni
mwanachama wa kawaida wa tawi la Chanjaani asiyekuwa na wadhifa wowote
mwingine ndani ya Chama.
Kwa mujibu wa Katiba ya CUF ibara ya 108(5) kuhusu Nidhamu ya chama na Muda wa kukata Rufaa inaeleza kuwa;
“
Mwanachama au kiongozi yeyote aliyeamua kukata Rufaa kwa jambo lolote
lile, basi atafanya hivyo kwa ngazi iliyo juu ya kikao kilichotoa
maamuzi ambayo hakuridhika nayo katika kipindi kisichozidi siku kumi na
nne (14) tokea siku uliotolewa uamuzi huo” ni hiyari yake kuona kama
inafaa kukitumia kifungu hiki au kutokitumia.
Tunatoa
wito kwa wanachama wote wa tawi la Chanjaani, kuzingatia wajibu wao wa
kikatiba na kuheshimu taratibu, kanuni na kulinda nidhamu na heshima ya
Chama chetu ndani ya Chama na ndani ya jamii kwa ujumla. Uongozi wa tawi
hautasita kutekeleza matakwa ya katiba pale itakapobainika kwa
mwanachama yeyote kwenda kinyume na maamuzi na misimamo ya Chama.
HAKI SAWA KWA WOTE
KOMBO MOHAMED MAALIM
KATIBU WA TAWI LA CHANJAANI, JIMBO LA MKOANI-PEMBA
Mawasiliano: 077 815 3414
0 comments:
Post a Comment