Naibu
waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhe. Suleimani Jafo akijibu
swali la Mbunge wa Kwela Mhe. Ignas Malocha (hayupo pichani) aliyehitaji
kujua ni lini kituo hicho cha afya kitapewa hadhi ya kuwa Hospitali ya
Wilaya,
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Dodoma
Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kukarabati kituo cha afya
cha Laela kilichopo mkoani Rukwa ili kikidhi vigezo vya kuwa Hospitali
ya Wilaya ikiwa ni moja ya jitihada za kupunguza adha ya wananchi
kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya zilipo.
Hayo
yamesemwa jana mjini Dodoma na Naibu waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais –
TAMISEMI, Mhe. Suleimani Jafo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kwela
Mhe. Ignas Malocha aliyehitaji kujua ni lini kituo hicho cha afya
kitapewa hadhi ya kuwa Hospitali ya Wilaya.
Mhe. Jafo
amesema kuwa ni uamuzi wa muda mrefu wa Serikali kuiweka Hospitali hiyo
kuwa ya Wilaya na ndiyo sababu ya kufanya jitihada za kukiongezea uwezo
kituo hicho kwa kujenga wodi nyingi pamoja na kutoa kibali cha kuajiri
watumishi wapya kwani kwa sasa kituo hicho kina upungufu wa watumishi .
Amefafanua
kuwa hadi sasa kuna baadhi ya majengo ambayo tayari yameshakamilika
ambayo ni jengo la upasuaji wa dharura, wodi ya wagonjwa waliofanyiwa
upasuaji pamoja na wodi ya mama wajawazito.
“Kwa sasa
kituo cha afya cha Laela hakina miundombinu inayokidhi sifa za kuwa
Hospitali ya Wilaya ila kutokana na kupanuka kwa Mji huo na kuongezeka
kwa watu wanaohitaji huduma katika kituo hicho tumeamua kukiboresha ili
kifikie hadhi ya kuwa Hospitali ya Wilaya”, amesema Jafo.
Ameongeza
kuwa kwa sasa huduma za rufaa kwa wagonjwa wanaohudumiwa katika kituo
hicho zinatolewa kupitia magari ya kawaida ya Halmashauri kutokana na
ukosefu wa gari la kubebea wagonjwa lakini Wizara ina matarajio ya
kutenga fedha ya kununulia gari hilo katika Bajeti ya mwaka 2017/2018.
Aidha,
Mhe. Jafo amethibitisha kuwa kituo hicho kimetengewa jumla ya shilingi
9,358,100 katika Bajeti ya fedha ya mwaka huu ambayo itagharamia kununua
dawa na vifaa tiba vitakavyorahisisha upatikanaji wa matibabu kwa
wananchi wa eneo hilo.
0 comments:
Post a Comment