WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imeunda timu ya wataalamu ambao
watatoa ushauri juu ya suala zima la kuhamishia makao makuu Dodoma.
Ametoa
kauli hiyo jana mchana (Jumamosi, Oktoba 1, 2016) wakati akizungumza na
watumishi wa Serikali wa mkoa wa Dodoma, wazee wa mkoa huo,
wafanyabiashara pamoja na viongozi mbalimbali kwenye ukumbi wa mikutano
wa Dodoma (Dodoma Convention Centre).
“Tumeunda
timu ya watu 10 ambao ni wataalamu waliobobea kwenye masuala ya ujenzi
wa miji mikuu, hawa wana uzoefu wa kuangalia makao Makuu ya nchi
yanafananaje. Watakuja Dodoma, wapitie master plan na kisha watapita
kwenye maeneo kadhaa ya mji ili waone hali halisi ikoje ndipo watupe
maoni yao,” amesema.
“Tunataka
tusirudie kosa la Jiji la Dar es Salaam la kulazimika kubomoa makazi ya
watu kila inapolazimu kufanya uboreshaji wa miundombinu. Hawa watu
watatuambia wapi tunatakiwa tuweke njia nne au sita za magari, wapi
tuweke bustani au wapi tujenge nyumba za ghorofa moja, mbili, tatu au
zaidi,” ameongeza.
Akifafanua
kuhusu miundombinu, Waziri Mkuu amesema timu hiyo pia itatakiwa kutoa
ushauri juu ya wapi ijengwe njia ya malori tu au mahali gani
zinahitajika kujengwa barabara za juu (flyovers) ili kuepusha msongamano
katikati ya mji wa Dodoma.
Bila
kutaja majina ya wajumbe wa timu hiyo, Waziri Mkuu amesema timu hiyo
itaongezewa wataalamu kutoka China na Malaysia ambao nchi zao tayari
zina uzoefu wa kuhamisha makao makuu ya nchi zao zaidi ya mara moja.
Alitumia
fursa hiyo kuwaeleza watumishi juu ya uwepo wa Tume ya Kuboresha
Maslahi ya Wafanyakazi ambayo imekuwa ikifanya kazi tangu mwaka jana.
“Kuna vikao vimekuwa vinafanyika tangu mwaka jana baina ya Serikali na
viongozi wa vyama vya wafanyakazi kwa lengo la kujadili uboreshaji wa
maslahi ya wafanyakazi, na jambo hili linaendelea vizuri,” amesema.
Kuhusu
madeni ya watumishi wa umma, Waziri Mkuu amewasihi watumishi wawe na
imani na Serikali yao kuhusu madeni hayo na kwamba ikimaliza uhakiki
unaofanyika hivi sasa, kila mwenye stahili zake atalipwa.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu ameutaka uongozi wa Mamlaka ya Ustawishaji
Makao Makuu (CDA) ihakikishe inakamilisha upimaji wa viwanja 100,000
kama ilivyojipangia ili watumishi hao pamoja na wananchi waweze kupatiwa
viwanja haraka iwezekanavyo.
“Nimearifiwa
kuwa mna mpango wa kupima viwanja 100,000 kwa ajili ya kuwapatia
wananchi na watumishi. Kamilisheni utaratibu huo haraka ili watumishi
wapewe viwanja na waweze kujenga nyumba zao za kuishi,” amesema huku
akishangiliwa.
Natambua
kuwa mmekubaliana kuanzisha utaratibu wa kuingiza viwanja kwenye mfumo
wa kompyuta ili kuepuka double allocation. Harakisheni zoezi hilo ili
kama itawezekana, kabla ya Novemba kazi hiyo iwe tayari na watu wapatiwe
viwanja chini ya mfumo huo mpya,” amesisitiza.
Kuhusu
huduma za kijamii kama elimu, umeme, maji na masoko, Waziri Mkuu
amewahakikishia watumishi hao kwamba Serikali imeangalia kila eneo na
kuzingatia mapendekezo yaliyotolewa ili kuboresha utoaji wa huduma hizo.
Amewataka watumishi hao wabadilike na wawe tayari kuwapokea watumishi
wenzao watakaowasili kwa awamu kuanzia mwezi huu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
0 comments:
Post a Comment