METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, October 1, 2016

Amphibious Landing yaonesha uthabiti wa ulinzi JWTZ

JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limehitimisha maadhimisho ya miaka 52 ya kuasisiwa kwa jeshi hilo, kwa kuonesha zoezi la medani liitwalo ‘Amphibious Landing’ lililofanyika Bagamoyo, Pwani.

Tukio hilo lililokuwa na mvuto wa aina yake, lilifanywa juzi jioni katika kijiji cha Baatini huku likishuhudiwa na Rais John Magufuli, Rais wa Zanzibar, Dk Mohamed Shein, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi na Katibu Mkuu Kiongozi wa Zanzibar, Abdulhamid Yahaya Mzee.Katika mazoezi hayo ya wiki mbili, Jeshi lilionesha uhalisia, jinsi wanavyoweza kukomboa eneo lililotekwa.

Wakati wa zoezi hilo, Meja Patrick Sawala alikuwa akielezea mtiririko wa matukio kwa Rais Magufuli na baada ya vikosi kumaliza kazi ya kukomboa eneo lililotekwa, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali, Davis Mwamunyange alisema anajivunia kuwa kiongozi wa chombo hicho.

‘Najivunia kuwa kiongozi wa chombo hiki, kwa sababu nina askari na maofisa wazuri, wanaojituma sana, weledi, wazalendo na wako tayari kulinda watanzania na wanafanya hivyo kwa maslahi ya nchi yao, na hata nje ya nchi tunajivunia kwa sifa yetu ya nidhamu na uimara wetu,” alisema Mwamunyange.

Mwamunyange alimwambia Rais Magufuli kuwa vifaa hivyo vya kijeshi ni mali ya watanzania, vimenunuliwa na watanzania na vyote vinaendeshwa na watanzania wenye maadili na weledi na nidhamu ya hali ya juu kwa nchi yao.

Katika mazoezi hayo, jeshi lilitumia ndegevita, vifaru vyenye uwezo wa kukaa baharini na kutembea nchi kavu, melivita, boti za kasi.

Akizungumzia lengo la mafunzo na zoezi hilo lililoshirikisha kamandi ya anga, maji, nchi kavu na Jeshi la Kujenga Taifa(JKT), Mwamunyange alisema ni kuimarisha ushirikiano na utendaji kazi wa vikosi. Rais Magufuli ambaye alivalia mavazi ya kijeshi, hakuweza kuficha hisia zake baada ya kukamilika kwa zoezi hilo, alisema ameridhika na uwezo wa jeshi hilo.

“Niseme ukweli, nimeridhika, hakuna anayeweza kutuchezea, tuna jeshi imara sina mashaka niko salama na watanzania wako salama,”alisema Rais Magufuli.

Mbali ya kulisifia jeshi kwa kazi nzuri inayofanya, pia aliahidi kutatua changamoto mbalimbali zinazokabili chombo hicho na kusema fedha za mafungu ya matumizi (OC) katika vyombo vyote vya ulinzi na usalama, zitaongezwa.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com