NI wazi kwamba Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli
imeanza kudhihirisha kwa vitendo, kauli kwamba deni la Tanzania nje ya
nchi ni himilivu baada ya kuanza kulipa sehemu ya deni ikiwa na chini ya
mwaka mmoja madarakani.
Takwimu zilizotolewa mwishoni mwa wiki na Ofisi ya Taifa ya Takwimu
(NBS) na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu
zimebainisha hali ya uchumi kuimarika kwa kasi, hatua ambayo imewezesha
serikali kuanza kulipa madeni na kutekeleza mipango mikubwa ya
maendeleo.Akithibitisha uwezo wa serikali kuanza kulipa deni la nje na la ndani
ambalo limekuwa likipigiwa kelele nyingi na wabunge hususani wa kambi ya
upinzani kuwa halihimiliki huku serikali ikisisitiza kuwa ni himilivu,
Gavana Ndulu amesema tayari serikali imeanza kulipa madeni hayo kwa
kasi.
Gavana Ndulu alisema juzi kuwa BoT imeanza kulipa madeni yote ya ndani
na nje kwa fedha zake za ndani ambapo tayari imeshalipa kiasi cha Sh
bilioni 96 za deni la ndani huku ikilipa dola za Kimarekani milioni 90
(sawa na Sh bilioni 190) za deni lake la nje.
Alisema kufuatia serikali kulipa Sh bilioni 96 za deni la ndani, deni
hilo linasalia kiasi cha Sh trilioni 9.9 huku deni la nje linalofikia
dola milioni 620 zikiwamo fedha za mkopo kutoka Benki ya Stanbic,
likipunguzwa kwa dola milioni 90.
Ndulu aliwahakikishia wananchi kuwa, uchumi wa Tanzania uko imara,
kukiwa na akiba ya kutosha ya fedha za kigeni zinazofikia dola bilioni
4, huku ikiendelea kutumia fedha zake za ndani kuendesha shughuli za
nchi bila kutumia mkopo kutoka nje, licha ya kwamba inahitajika hususani
ile nafuu.
“Hakuna fedha hata senti kutoka nje tuliyotumia tumelipa madeni makubwa
na mnaona bado tuna kiasi kikubwa, niseme tu kwa sasa serikali
inajiendesha kwa fedha yake ya ndani,” alisema Ndulu.
Kuimarika kwa Pato Akizungumza na waandishi wa habari Alhamisi
iliyopita, Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dk Albina Chuwa alisema katika
kipindi cha robo ya pili ya mwaka huu, pato la Taifa limeendelea kukua
kwa kasi ya asilimia 7.9 ikilinganishwa na asilimia 5.8 ya robo ya pili
ya mwaka jana.
Chuwa alisema kutokana na kasi ya uchumi inavyokwenda kwa sasa, huenda
ifikapo Desemba mwaka huu, kwenye taarifa ya robo ya tatu ya mwaka pato
la Taifa likaongezeka zaidi.
Alisema kwa mujibu wa takwimu zilizopo, pato hilo la Taifa limefika
jumla ya thamani ya Sh trilioni 11.7 ikilinganishwa na Sh trilioni 10.9
katika kipindi kama hicho cha mwaka jana.
Naye Gavana Ndulu akizungumzia hali ya uchumi juzi, alisema ukuaji wa
Pato la Taifa katika nusu ya kwanza ya mwaka ya Januari hadi Juni,
umeongezeka na kufikia asilimia 6.7 kutoka asilimia 5.7 kwa nusu ya
kwanza ya mwaka 2015.
Alisema katika robo ya pili ya mwaka 2016, ukuaji wa Pato la Taifa
unakadiriwa kuongezeka kwa asilimia 7.9 ikilinganishwa na ongezeko la
asimilia 5.8 kwa kipindi kama hicho mwaka 2015.
Alisema shughuli zinazochangia ukuaji huo wa uchumi kwa kiasi kikubwa
kwa nusu ya kwanza ya mwaka 2016 ni uchukuzi na uhifadhi wa mizigo
asilimia 16.0, ujenzi asilimia 10.7 na kilimo asilimia 10.3.
Akizungumzia mafanikio hayo jana, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Profesa Benson Bana alisema hizo ni dalili za wazi kabisa kwamba
sasa serikali ina uwezo mkubwa wa kifedha kuliko ilivyokuwa huko nyuma.
“Ukiangalia takwimu za ukuaji wa uchumi na miradi mikubwa inayofanyika
ni uthibitisho tosha kwamba kauli ya Rais Magufuli kwamba serikali ina
uwezo wa kulipa madeni lakini pia kununua ndege na kutekeleza miradi
mbalimbali ya maendeleo kwa fedha za ndani, inawezekana,” alisema Bana.
Saturday, October 1, 2016
KARIBU TUME YA MAENDELEO YA USHIRIKA
Popular Posts
-
📌 Asema Rais, Dkt. Samia anafanya kazi kubwa ya kuwaunganisha Watanzaia 📌 Atak...
-
Mvua kubwa za El-Nino zilizonyesha zimeleta athari maeneo mbalimbali...
-
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa MOI, Dkt. Respicious Boniface akizungumza na Waandishi wa Habari (ha...
-
Waziri wa kilimo Mhe Japhet Hasunga akikagua ghala la kuhifadhia mbegu la Wakala wa Mbegu (ASA) katika ziara yake ya kikazi mkoani Morogo...
-
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu) Jenista Mhagama akisalimiana na baadhi ya Viongo...
Powered by Blogger.
0 comments:
Post a Comment