METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, October 17, 2016

Watumishi TBS na TRA Waliohusika n a Upotevu wa Makontena 100 Bandarini Watakiwa Kujisalimisha Haraka kabla Hawatumbuliwa


Serikali imewataka baadhi ya wafanyakazi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) walioshirikiana na wenzao wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kupitisha  makontena zaidi ya 100 bila kukaguliwa na shirika hilo katika Bandari ya Dar es Salaam kujisalimisha haraka.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alitoa agizo hilo jana wakati akizindua baraza la wafanyakazi wa TBS.

“Nimeanza kukusanya orodha ya majina ya watu waliosaidia kupitisha makontena haya na nikija nayo hawatapona,” alisema.

Aliwataka wote wanaojijua kuhusika kujisalimisha mapema na kutubu ili wasamehewe kabla ya hatua hiyo.

Makontena hayo yalipitishwa katika Bandari ya Dar es Salaam hivi karibuni bila ya kuthibitishwa na TBS.

Pia, aliitaka TRA kuacha kutoa makontena bila ya shirika hilo kuthibitisha au kukagua ubora wa bidhaa zinazoingizwa nchini kwa sababu ndilo lenye mamlaka hayo.

Alisema watakaotubu watapaswa kusema walishiriki vipi na lini, walishirikiana na nani na kutaja sehemu yalikopelekwa ili Serikali iweze kusaidia kukomesha hali hiyo.

Mwijage alisema anaamini waliofanya hivyo katika mamlaka hiyo walifanya kwa utashi wao bila ya ushiriki wa viongozi wao na kwamba sasa wakati umefika wa kukomesha tabia hiyo.

Alilitaka baraza hilo jipya la wafanyakazi kushirikiana na menejimenti kuhakikisha matatizo yanayojitokeza yanapatiwa ufumbuzi kwa masilahi ya nchi na kwamba Serikali itahakikisha inaongeza vitendea kazi na watumishi ili kufikia malengo ya shirika.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk Egid Mubofu alisema baraza hilo lina wajumbe 48 wanaotoka katika vitengo mbalimbali na litakaa kwa muda wa miaka mitano.

“Baraza hili linaundwa kutokana na mkataba wa menejimenti na Chama cha Wafanyakazi (Raawu),” alisema Dk Mubofu.

Alisema wafanyakazi wanatakiwa kufanya kazi kwa weledi na uadilifu katika majukumu yao ya kila siku.

Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi TBS, Profesa Mekanya Maboko alilitaka baraza hilo kufanya kazi kwa kushirikiana na menejimenti na bodi kuhakikisha shughuli za udhibiti wa ubora zinafanyika kwa ufanisi.

“Bodi itaendelea kuisimamia menejimenti na kuishauri ifanye kazi kwa kuzingatia sera na sheria,” alisema.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com