WATU wanne wakiwemo raia watatu wa Burundi, wanashikiliwa na Polisi
mkoani Morogoro baada ya kukutwa na magamba ya kakakuona, yenye thamani
ya zaidi ya Sh bilioni 1.4.
Walikuwa wamehifadhi magamba hayo kwenye mifuko 67, yakisubiri
kusafirishwa kwenda nje ya nchi kuuzwa. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Morogoro, Ulrich Matei, alisema watu hao walikamatwa saa tano na nusu
usiku wa Oktoba 28, mwaka huu eneo la mtaa wa Reli, kata ya Kichangani,
Manispaa ya Morogoro.
Walinaswa ndani ya ghala moja, lenye mashine ya kukoboa na kusaga nafaka.
Alisema, askari wa jeshi hilo wakiwa katika msako, walipokea taarifa
za kiintelejensia kutoka kwa raia wema kuhusu mazingira ya watu katika
eneo hilo. Walipofika, walikuta watuhumiwa hao wanne.
Baada ya upekuzi kwenye ghala hilo, polisi walikamata magamba ya
kakakuona katika mifuko 67, baaadhi yake yakiwa tayari kwa ajili ya
kusafirishwa kwenda nje ya nchi.
Kamanda Matei aliwataja raia wa Burundi waliokamatwa kuwa ni Kibonese
Golagoza ( 35), Nuru Athuman (32) na Benjamin Gregory Luvunduka (41)
ambao pia ni wakazi wa Morogoro, wakati Mtanzania ni Shukuru Mwakalebela
(25) mkazi wa Stesheni mjini hapa.
Alisema magamba hayo, yalifungwa katika mifuko yenye kilo 50 na kisha
kutumbukizwa kwenye viroba vikubwa vya kilo 100, vilivyochanganywa na
maharage. Aidha alisema watuhumiwa raia wa Burundi, wanakabiliwa pia na
tuhuma za kuingia nchini bila kibali cha Uhamiaji.
Alisema wote wanaendelea kuhojiwa na Polisi na watafikishwa
mahakamani upelelezi utakapokamilika. Hata hivyo, Kamanda huyo alisema
ni mapema kueleza kakakuona hao wanauawa katika maeneo gani ya nchi, na
mahali liliko soko kubwa kwa vile suala hilo lipo katika uchunguzi na
utakapokamilika, taarifa itatolewa.
Ofisa Maliasili wa Mkoa wa Morogoro, Joseph Chuwa aliyekuwepo katika
upekuzi huo, alisema katika mifuko 67 iliyokamatwa, kila mmoja ulikuwa
na wastani wa magamba ya kakakuona 1,000.
Alisema kakakuona mmoja, kwa wastani anakuwa na magamba 60 hadi 100,
hatua iliyofanya kila mfuko kuwa na wastani wa kakakuona wapatao 10
waliouawa kwa ajili ya biashara hiyo haramu.
Alisema kutokana na idadi ya mifuko hiyo, wastani wa kakakuona 670
waliuawa, ambapo kilo moja ya magamba yake huuzwa kwa dola za Marekani
960, hivyo kutokana na viwango vya sasa vya thamani ya dola kwa fedha ya
Tanzania, ni sawa na Sh bilioni 1.4.
Chuwa alisema kutokana na wingi wa magamba hayo ya kakakuona,
ujangili huo hauwezi kuwa umefanyika mkoani Morogoro pekee, bali pia
katika maeneo mengine ya hapa nchini, kwa kuwa kiwango hicho ni kikubwa
na hayakupatikana kwa wakati mmoja. Alisema soko kubwa la bidhaa hiyo ni
katika Bara la Asia.
Kakakuona kwa ufupi
Kakakuona ndiye mnyama pekee duniani, ambaye mwili wake wote
umefunikwa na magamba makubwa kuliko ya viumbe wengine. Hutumia magamba
hayo, kama silaha ya kujilinda dhidi ya maadui. Jina la kakakuona
lilianzia nchi za Mashariki ya Mbali za Malaysia, Indonesia na Brunei,
likimaanisha kitu kinachojikunja.
Kwa kawaida, Kakakuona hupenda kujikunja kama mpira. Hiyo ni mbinu
anayotumia kujilinda dhidi ya maadui. Kakakuona akiona adui, hujilinda
kwa kujikunja, lakini akiona hali inakuwa mbaya zaidi, hutema sumu kali
mithili ya tindikali inayoweza kumdhuru adui.
Pia, wakati mwingine hunyoosha mkia wake na kuuzungusha na kumkamata
adui aliyekaribu yake.
Licha ya kutumia mbinu hiyo kujilinda, lakini
anapojikunja ndiyo inakuwa rahisi kwa watu kumkamata na kumbeba. Kuna
aina nane za kakakuona duniani, zilizopo duniani kwa zaidi ya miaka
milioni 80 ya mabadiliko yao.
Kati ya hizo, aina nne zinapatikana Bara la Ulaya na nyingine barani
Afrika. Kakakuona ana ulimi wenye urefu unaozidi mwili wake. Akiurefusha
kwa kuutoa nje ya kinywa, unafikia urefu wa sentimita 40. Ulimi huo
ambao pia unanata, huutumia kwa ajili ya kukusanya wadudu, ambao ndiyo
mlo wake wa pekee.
Hana mlo mwingine zaidi ya huo kutokana na kukosa meno. Baadhi ya
kakakuona huishi juu ya miti. Wengine hujichimbia ardhini na kuishi
ndani ya mashimo. Wanaoishi juu ya miti ni wenye mikia mirefu
wanaopatikana barani Afrika. Wengine huchimba mashimo marefu ardhini na
kuishi humo ili wasikutane na binadamu.
Inakadiriwa kuwa kakakuona 100,000 hukamatwa kila mwaka barani Afrika
na Ulaya na kuuzwa. China na Vietnam ndizo nchi maarufu ambazo nyama na
magamba yake huuzwa. Inakadiriwa kuwa mamilioni ya wanyama hao,
wameuawa na kuuzwa katika miaka 10 iliyopita.
Sunday, October 30, 2016
KARIBU TUME YA MAENDELEO YA USHIRIKA
KARIBU TUME YA MAENDELEO YA USHIRIKA
Popular Posts
-
Kiongozi wa chama cha upinzani cha Forum for Democratic Change (FDC) nchini Uganda Kizza Besigye amekamatwa tena na maafisa wa polisi. ...
-
📌 Asema Rais, Dkt. Samia anafanya kazi kubwa ya kuwaunganisha Watanzaia 📌 Atak...
-
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea hundi ya sh. 4, 000,000,000/= kutoka kwa Meneja Mkazi (Country Manager) wa Kampuni ya Madini ya...
-
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati akifungua kikao kazi cha vyama vya ushirika kuhusu ununuzi wa mbolea k...
-
Mvua kubwa za El-Nino zilizonyesha zimeleta athari maeneo mbalimbali...
Powered by Blogger.
0 comments:
Post a Comment