METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, October 30, 2016

Uzazi wa mpango unavyookoa maisha Singida

 Mkuu wa mkoa wa Singida Mheshimiwa Mhandisi Mathew John Mtigumwe
 
WAKATI leo nchi yetu inaanza Mkutano wa Kimataifa kuhusu Uzazi wa Mpango maarufu kama FP 2020, tatizo la wanawake na watoto kupoteza maisha wakati wa kujifungua bado linaendelea kujichimbia nchini. Tanzania ni moja ya nchi zilizojitahidi kutekeleza Malengo ya Milenia ambapo lengo namba tano lilitaka kupunguzwa kwa vifo, kufikia 193 kwa kila vizazi hai 100,000 kabla ya Desemba mwaka jana. Credit:Habari Leo

Hata hivyo, licha ya juhudi zilizofanyika, takwimu za hivi karibuni kutoka Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto zinaonesha kutofikiwa kwa malengo hayo kwa kuwa bado zaidi ya wanawake 430 katika kila vizazi hai 100,000, wanapoteza maisha wakati na baada ya kujifungua.

Pamoja na juhudi nyingi zinazochukuliwa kama kuboresha huduma za afya, nyingine ambayo wadau wanaamini itachangia sana kupunguza tatizo hilo nchini ni ongezeko la wanawake na wasichana wanaotumia njia za kisasa za uzazi wa mpango.

Utoaji mimba usio salama Zipo sababu mbalimbali zinazotajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa tatizo hili la vifo vya akina mama vitokanavyo na matatizo ya uzazi hapa nchini. Sababu hizo ni pamoja na utoaji mimba usio salama hasa unaofanywa na kundi la vijana wakiwemo ambao bado wapo shuleni na vyuoni.

Vifo vinavyotokana na utoaji mimba holela vinatajwa kushika nafasi ya pili (kati ya asilimia 13-15), nafasi ya kwanza ikiwa ni kutokwa na damu nyingi kunakosababisha asilimia 24 ya vifo hivyo vya uzazi.

Tafiti zilizopo zinaonesha kuwa mwanamke mmoja katika kila watano hapa nchini, angehitaji kupanga uzazi lakini hajafikiwa na huduma hizo huku wanawake milioni moja kila mwaka wakipata mimba ambazo hawakuzitarajia.

Asilimia 40, sawa na wanawake 405,000 kati yao hao huishia kutoa mimba hizo kila mwaka kwa utaratibu usio salama ambao wakati mwingine husababisha vifo au maradhi.

Ingawa kiwango cha vifo hivyo kinatofautiana kutoka eneo moja hadi lingine, Singida ni miongoni mwa mikoa ambayo inakabiliwa na tatizo hilo kwa kiasi kikubwa kutokana na sababu mbalimbali. Baadhi ya sababu zinazotajwa ni wajawazito kucheleweshwa kupelekwa vituo vya kujifungulia, kuendekeza imani potofu na umbali mrefu kwenda kwenye vituo vya kujifungulia.

Sababu zingine zinazotajwa ni kutozingatia ushauri wa watalaamu wa afya, matumizi duni ya njia za kiasa za uzazi wa mpango na uzazi katika umri mdogo au mkubwa.

Hata hivyo, sababu kubwa inayotajwa kwa mkoa wa Singida ni utoaji mimba usio salama baada ya wahusika kupata mimba ambazo hawakuzitarajia. Hii maana yake ni kwamba kama wangelipanga uzazi, vifo hivyo visingelitokea.

Takwimu kutoka Idara ya Afya Mkoani Singida zinaonesha kwamba jumla ya wanawake 97 wamepoteza maisha kutokana na matatizo mbalimbali ya uzazi katika kipindi cha Januari mwaka jana na Oktoba 10 mwaka huu.

Manispaa ya Singida ambayo ina vyuo vingi kuliko halmshauri nyingine za mkoa wa Singida, ndiyo inayoongoza kwa vifo vingi kwa kupoteza wasichana 30 katika kipindi tajwa licha ya ukweli kwamba eneo hilo ndilo pia lenye huduma bora zaidi za afya kulinganisha na maeneo mengine ya mkoa.

Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk John Mwombeki, kati ya vifo 19 vilivyotokea katika manispaa hiyo kwa mwaka jana pekee, vifo tisa ambavyo ni sawa na asilimia 47 ya vifo vyote kwa kipindi hicho vilisababishwa na vijana wa vyuo kujaribu kutoa mimba kwa njia isiyo salama.

Dawa feki za kutolea mimba Dk Mwombeki anasema kuwa wanavyuo hao wamekuwa wakinunua kiholela dawa iitwayo "Misoprostol" kutoka maduka ya dawa muhimu au zahanati bubu na kuitumia isivyo sahihi kutolea mimba.

"Kitaalamu, dawa hii hutumika kwa wajawazito ambao hushindwa kujifungua kwa njia ya kawaida na ni lazima itolewe kwa idhini ya daktari lakini vijana hawa wananunua kiholela na kuitumia pale wanapobaini wamepata mimba wasizotarajia," anafafanua Dk Mwombeki.

Anasema kuwa matumizi ya "misoprostol" bila ushauri wa daktari huleta madhara makubwa kwa mtumiaji; ikiwemo kutokwa na damu nyingi na hivyo kuweza kusababisha kifo kwa mhusika.

Anasema kukosekana kwa taarifa za kutosha kuhusu matumizi ya njia za kisasa za Uzazi wa Mpango kwa vijana wa kike katika eneo hilo kunachangia tatizo na vifo hivyo. Tamaa vyuoni.

Anasema baadhi ya wasichana walio vyuoni, hujiingiza katika mapenzi yasiyo salama kutokana na tamaa za mwili au fedha. Anasema baadhi ya wanaume wenye fedha katika manispaa hiyo pia hudhani ni salama kufanya ngono bila kinga na wanavyuo wakiamini kuwa mabinti hao hawana magonjwa, jambo ambalo si kweli pia.

Anasema mmomonyoko wa maadili kwa baadhi ya matabibu wa hospitali ya Serikali na wa vichochoroni huchangia kushamiri tatizo la utoaji mimba usio salama ambalo ni kosa la jinai kwa mujibu wa sheria zetu.

Dk Mwombeki anasema kuwa mbali na kupoteza maisha, madhara ya utoaji mimba usio salama ni pamoja na ugumba iwapo mhusika atatolewa kizazi kwa bahati mbaya wakati wa kutoa mimba.

Pia anasema kupata maambukizi ya magonjwa mbalimbali. Wadau wadhamiria kuokoa vifo Kutokana na tatizo hilo, Dk Mwombeki anasema kuwa wapo wadau ambao wameliona tatizo hilo na kuanza kuchukua hatua mbalimbali ili kupunguza vifo vinavyojitokeza.

Anasema kuwa miongoni mwa wadau hao ni Shirika lisilo la Kiserikali la Marie Stopes lenye makao yake makuu jijini Dar es Salaam ambalo limefanyakazi kubwa katika kutoa elimu ya uzazi wa mpango katika makundi mbalimbali kwa vijana mkoani humo.

Anasema Marie Stopes wamekuwa wakiandaa matamasha kwa kuwakusanya vijana na kuwapatia elimu juu ya umuhimu wa kuzingatia Uzazi wa Mpango ili kupunguza tatizo la utoaji wa mimba holela.

Muuguzi Kiongozi wa Marie Stopes anayeshughulika na utoaji Elimu ya Uzazi wa Mpango mkoa wa Singida, Flora Shirima anasema kuwa pamoja na elimu wanayotoa, bado kuna changamoto kubwa ya mimba zisizotarajiwa miongoni mwa vijana mkoani humo.

Anasema Marie Stopes lilijikita katika kutoa elimu na huduma ya Uzazi wa Mpango kwa eneo hilo huku msisitizo ukiwa kwa vijana na hasa wanavyuo na wanafunzi wa sekondari. Shirima anasema licha ya changamoto hiyo, kumekuwa na mabadiliko chanya kutokana na huduma hiyo.

"Huduma zetu zinalenga kupunguza vifo vya wajawazito wakati wa kujifungua. Katika eneo hili kwa kweli tumefanikiwa kwani vifo vimepungua kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na wakati tulipoanza," anasema Shirima na kuongeza kwamba walengwa wao pia ni wanavyuo.

Anasema kuwa wanapofika kwenye maeneo yenye watu wagumu kupokea huduma zao, mbinu mbalimbali hutumika ikiwa ni pamoja na kuwatumia watendaji wa vijiji kuitisha mikutano ya hadhara na katika mikutano hiyo Elimu ya Uzazi wa Mpango hutolewa na wataalam wa Afya.

Shirima anasema kwa vile hakuna sheria inayoruhusu utoaji mimba nchini, njia pekee ya kuepukana na adha ya utoaji mimba kiholela na usio salama kwa akina mama na vijana ni kujikita kwenye kutumoa njia za kisasa za kupanga uzazi.

Msaidizi Mratibu wa Afya ya mama na Mtoto mkoa wa Singida, Hyasinta Alute anasema kwa kipindi cha mwaka jana kulikuwa na jumla ya vifo 60 mkoani Singida, 13 kati ya vifo hivyo vilitokana na utoaji mimba usio salama.

Alute anasema kuwa kati ya Januari na Oktoba 10 mwaka huu kumekuwa na jumla ya vifo 37 tu huku kukiwa hakuna kifo hata kimoja kitokanacho na utoaji mimba kiholela; hali inayoashiria dalili njema ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Kwa mujibu wa Mratibu huyo, jumla ya idadi ya vifo kwa kipindi cha Januari mwaka jana na Oktoba 10 mwaka huu ni 30 kwa Manispaa, Ikungi vifo 23, Manyoni 17, Iramba 13, Mkalama sita na Halmashauri ya Singida vifo viwili na kwamba vyote vimetokana na sababu nyinginezo na sio utoaji mimba.

Anakiri kuwa Marie Stopes ni moja ya wadau wakubwa katika suala hilo ambao wamesaidia kufikisha elimu ya Uzazi wa Mpango kikamilifu katika maeneo ya vyuo mbalimbali na shule za sekondari.

Elimu yasaidia Aidha, Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto katika Manispaa ya Singida, Cresencia Mapunda mwenye eneo ambalo hapo awali lilikuwa tete kwa utoaji mimba, anathibitisha kuwa mamlaka hiyo kwa kushirikiana na wadau wake mbalimbali, wakiwemo Marie Stopes wamekuwa wakitoa elimu hiyo mara kwa mara.

“Kwa mfano, mwaka huu tu sisi kwa kushirikiana na Marie Stopes tayari tumeshatoa huduma rafiki kwa vijana mara mara tatu (Januari, Juni, na Septemba) kwa kutembelea vyuo na shule za sekondari kwa ajili ya kutoa huduma na elimu ya Uzazi wa Mpango,” anasema Mapunda.

Mratibu huyo anasema kuwa mbali na kupunguza utoaji mimba, elimu imeongeza kiwango cha utumiaji wa njia za kisasa za Uzazi wa Mpango kwa kipindi cha mwaka jana hadi kufikia asilimia 57. Takwimu hizi anasema zinadhihirisha kwamba mwitikio wa huduma hizi umekuwa mkubwa.

Uzazi wa mpango ni nini hasa?

Uzazi wa mpango ni uhuru wa mwanamke, mwanamume, wanandoa au walio katika mahusano kuamua kutokuwa na mtoto asiyetarajiwa na pia kupanga lini kuzaa na idadi ya watoto.

Hali hiyo haiji hivi hivi isipokuwa inahusisha upatikanaji wa huduma hiyo, taarifa sahihi (elimu), sera, upatikanaji wa bidhaa yaani njia zote zinazotumika katika kupanga uzazi na watalaamu.

Tafitizi za kisayansi zilizopo zinaonesha kwamba kadri watu wengi wanapotumia uzazi wa mpango katika jamii kunakuwa na faida nyingi kama kupunguza vifo vya akina mama na watoto vitokanavyo na uzazi, kupunguza utoaji wa mimba zisizo salama, kupunguza utegemezi, kuimarisha afya ya akinana na kuwawezesha kuzalisha mali.

Ni kwa sababu hiyo uzazi wa mpango hauchukuliwi kama ‘masuala ya wanawake’ bali uchumi na maendeleo na hata mazingira.

Unahusishwa pia na haki za binadamu, usawa wa kijinsia na uwezeshwaji.

Takribani nchi zote zilizoendelea duniani zimefanya juhudi kubwa katika kupanga uzazi.

Mkutano wa FP 2020 Kuanzia leo hadi Ijumaa, nchi yetu utakuwa mwenyeji wa mkutano unalenga kuangalia hatua zilizofikiwa kuhusu malengo yaliyowekwa na wadau mwaka 2012 ili yawe yametekezwa ifikapo mwaka 2020 na ndio maana unaitwa FP 2020.

Wadu walipokutana mwaka 2012 nchini Uingereza, waliona kuna kasi ndogo ya utumiaji wa njia za kisasa za uzazi wa mpango, hali inayochangia kudumaza maendeleo.

Ikaweka malengo na matarajio kwamba ufikapo 2020, wanawake na wasichana milioni 120 wawe wanatumia njia za kisasa za uzazi wa mpango. Nchi yetu, nayo ikadhamiria kutekeleza maazimio hayo kwa kuongeza idadi ya wanaotumia njia za kisasa za uzazi wa mpango kutoka asilimia 27 wakati huo hadi asilimia 65 kufikia mwaka jana.

Lakini hadi sasa takwimu zinaonesha tuko asilimia 32 tu. Njia za kisasa za uzazi mpango ni pamoja na matumizi ya kondomu, sindano na vidonge, zinazoitwa za muda mfupi wakati za muda mrefu ni pamoja na matumizi ya vijiti na vitanzi. Njia zingine ni kufunga uzazi kwa wanawake au wanaume (vasectomy).
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com