TAARIFA zilizopo zinaonesha kwamba nchi za Asia zikiwemo Malaysia na
Singapore ambazo wakati tunapata uhuru kiwango cha maendeleo yao na sisi
kilikuwa takribani sawa, zimepiga hatua kubwa ya maendeleo kutokana na
kuwekeza vya kutosha katika elimu, afya, uzazi wa mpango na mageuzi ya
kiuchumi.
Bila shaka tumeifanya Malaysia kama nchi tunayojifunza kwake,
hususani suala zima la Matokeo Makubwa Sasa (BRN) hadi wataalamu wao
walikuja nchini kutusaidia namna ya kunyanyua uchumi wetu kwa haraka
kupitia njia hiyo. Lakini swali ambalo wengine wanajiuliza ni mbona
hatukuwaiga pia suala zima la uzazi wa mpango ambao unatajwa kuwa moja
ya kitu kilichowasaidia kupiga hatua?
Takwimu zinaonesha kwamba mwaka 1960 pato la taifa la Malaysia kwa
mwaka lilikuwa Dola za Marekani 299 huku sisi likiwa 319. Lakini mwaka
2010, pato lao lilikuwa limefikia Dola 8,754 wakati letu likiwa Dola
514.
Takwimu pia zinaonesha kwamba mwaka 1960, wastani wa kuzaa kwa kila
mwanamke wa Malaysia (fertility rate) ilikuwa watoto sita wakati sisi
ikiwa watoto saba, lakini mwaka 2010 takwimu zinaonesha kwamba wao
walikuwa na wastani wa kuzaa watoto wawili, sisi watoto 5.4 (sawa na
sita).
Kadhalika mwaka 1960, kiwango cha kujiunga na shule za sekondari kwa
Malaysia kilikuwa asilimia 35 wakati Tanzania kilikuwa 9, lakini mwaka
2010 kiwango chao kilikuwa asilimia 96 huku chetu kikiwa asilimia 27 tu.
Na kiwango cha wanafunzi kujiunga na vyuo (vikiwemo vyuo vikuu) kwa
Malaysia mwaka 1960 kilikuwa asilimia 4, huku sisi kikiwa 0.5 lakini
mwaka 2010 kiwango chao kilikuwa kimepanda hadi asilimia 37 wakati sisi
kikiwa asilimia 3.9 tu.
Kwa mantiki hiyo, wakati tunapozungumzia kuelekea uchumi wa kati
ifikapo mwaka 2025 huku tukianza kufanya mageuzi ya kiuchumi, tunaweza
tukafanikiwa haraka kama suala la uzazi wa mpango na elimu bora kwa
watoto wetu tutalitilia maanani.
Faida za uzazi wa mpango Uzazi wa mpango una faida nyingi, kuanzia
kupunguza vifo vya akina mama vinavyotokana na uzazi, kupunguza vifo vya
watoto chini ya umri wa miaka mitano na kupunguza utoaji wa mimba usio
salama (kienyeji) ambao pia huhatarisha sana maisha.
Lakini pia kuna faida nyingi za kiuchumi kutokana na uzazi wa mpango
ikiwa ni pamoja na mama kuongezea fursa za kujishughulisha kiuchumi,
familia kupata muda wa kutosha wa kuwekeza kwa watoto wao wachache
lakini pia kuna faida kwa jamii kuendana na raslimali chache zilizopo.
Wanademografia wanasema jamii zote zilizopiga hatua ya maendeleo
duniani, moja ya kitu kilichowasaidia kufika waliko leo ni kuhimiza
uzazi wa mpango kwani una mchango mkubwa ikiwemo familia na taifa kwa
ujumla kuwa na uwezo wa kuendeleza watoto kielimu.
Kwa mfano, hata kama tumehimiza vya kutosha suala la madawati mwaka
huu, kama uzazi wa mpango hautazingatiwa, tutegemee kila mwaka kuwa na
upungufu mkubwa wa madawati.
Hapo sijasemea matundu ya vyoo, vitabu, maabara, idadi ya waalimu na
kadhalika! Njia za kisasa Njia za uzazi wa mpango za kisasa
zimegawanyika katika makundi matatu, zipo za muda mfupi, muda mrefu na
zile za kufunga kabisa kizazi baada ya wanandoa kukubaliana hivyo. Njia
za muda mfupi kwa mujibu wa Dk Dismas Daniel wa Hospitali ya Marie
Stopes ni matumizi ya sindano, vidonge na kondomu.
Anafafanua kwamba, kwanza kabla ya mama kupatiwa tiba hiyo,
anafanyiwa uchunguzi na anapopewa, huwa imeshaaminika kwamba hatopata
matatizo, na kama yapo ni madogo tu.
Anasema kinachofanywa na sindano au vidonge ni kuzuia yai lisipevuke
na pia kuweka ute mzito kwenye njia ya kizazi, hatua inayozuia mbegu za
kiume kutoingia kwenye mji wa mimba.
Anasema kutokana na mabadiliko hayo yanayotokana na homoni, baadhi ya
watumiaji hupata madhara madogo, ikiwa ni pamoja kunenepa au baadaye
kutokwa na damu, lakini kinachotakiwa ni kuwaona wataalamu na tatizo
hushughulikiwa na kumalizwa.
Kuhusu kondomu anasema kuna watu ambao wanapata mzio (allergy)
wakizitumia na hao ni wachache na wakiwaona madaktari watapata ushauri
maridhawa. Njia za muda mrefu Dk Daniel anazitaka kuwa ni pamoja kitanzi
na vijiti ambazo baadhi ya watu, hususani kitanzi, wamezipa pia sifa
ambazo hazina.
"Kuna watu wanatoa madai kwamba mwanamke akiwekewa kitanzi, mara baba
atakigusa, mara kinatembea mwilini na mengine ambayo hayana ukweli.
Kuna baba wakati wa tendo la ndoa na mkewe mjamzito alishamgusa mwanae?" Anahoji Dk Daniel.
Anafafanua kwamba kitanzi huwekwa kwenye mji wa mimba ambako si
rahisi mwanamume kupagusa wala habari za kutanzi kutembea mwili hazina
ukweli wowote.
Hata njia za kufunga kabisa kizazi kwa mwanamke na mwanaume, Dk
Daniel anasema hazina madhara kama wengi 'wanavyobwabwaja' mitaani
kwamba zinasababisha saratani, au kumfanya mhusika akose raha ya tendo
la ndoa.
Mkutano wa FP 2020 Kuanzia leo, nchi yetu itakuwa mwenyeji wa mkutano
wa Kimataifa kuhusu Uzazi wa Mpango maarufu kama FP 2020). FP 2020 ni
mkutano unaojielekeza katika kutekeleza malengo ambayo dunia imejiwekea
ifikapo mwaka 2020.
Mkakati huo ni wa ushirikiano wa kimataifa unaohamasisha haki za
wanawake na wasichana za kuamua kwa uhuru ni wakati gani ambao ni
mwafaka kwao kushika mimba na hivyo kuondokana na mimba wasizozitarajia.
Ni mpango unaoshirikisha serikali, asasi za kiraia, mashirika ya
kimataifa, wafadhili, sekta binafsi, na watafiti wa maendeleo ya jamii
katika kuwawezesha wanawake na wasichana zaidi ya milioni 120 kutumia
njia za kiasa za uzazi wa mpango ifikiapo mwaka 2020.
Mkutano huo pia utashirikisha mpango wa kimataifa wa kusaidia kifedha
juhudi za nchi mbalimbali katika kuimarisha afya ya wanawake, watoto na
vijana wadogo, yaani Global Financing Facility (GFF).
Hadi mwaka 2013 wakati Tanzania inafanya mkutano wake wa Kitaifa wa
Uzazi wa Mpango (FP), idadi ya watumiaji wa njia za kisasa za uzazi wa
mpango ilikuwa asilimia 27 tu na lengo lilikuwa ni kufikia asilimia 60
hadi mwishoni mwa mwaka jana. Hata hivyo, takwimu zilizopo zinaonesha
kwamba kasi siyo kubwa kwani ni asilimia 32 tu kwa sasa ndio wanaotumia
njia za kisasa za uzazi wa mpango.
Utafiti uliofanywa Zambia unaonesha kwamba kuwekeza dola moja katika
uzazi wa mpango kunasaidia kuokoa dola nne katika masuala ya afya na
maeneo mengine ya maendeleo, ikiwa ni pamoja na afya ya uzazi, chakula,
malaria, elimu na huduma za maji. Wakati mkutano huu unafanyika nyumbani
ni vyema tuzinduke na kujipanga katika kuongeza idadi kubwa zaidi ya
matumizi ya njia za kisasa za uzazi wa mpango.
Ili hilo liwezekane tunatakiwa kuongeza elimu kuhusu faida za kupanga
uzazi na kuongeza bidhaa za uzazi wa mpango na wataalamu hadi vijijini.
Pia tunapaswa kuboresha sera na sheria zetu lakini kubwa kabisa ni
kuongeza bajeti inayokwenda kwenye uzazi wa mpango, mintarafu suala zima
la upatikanaji bidhaa zote za kupanga uzazi kisasa.
Bajeti iliyotengwa mwaka huu ni Sh bilioni 5, lakini mahitaji halisi
ni Sh bilioni 20. Si vibaya tukaongeza hadi hata Sh bilioni 8, kiwango
ambacho hatujawahi kufikia.
Sunday, October 30, 2016
KARIBU TUME YA MAENDELEO YA USHIRIKA
KARIBU TUME YA MAENDELEO YA USHIRIKA
Popular Posts
-
Kiongozi wa chama cha upinzani cha Forum for Democratic Change (FDC) nchini Uganda Kizza Besigye amekamatwa tena na maafisa wa polisi. ...
-
📌 Asema Rais, Dkt. Samia anafanya kazi kubwa ya kuwaunganisha Watanzaia 📌 Atak...
-
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea hundi ya sh. 4, 000,000,000/= kutoka kwa Meneja Mkazi (Country Manager) wa Kampuni ya Madini ya...
-
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati akifungua kikao kazi cha vyama vya ushirika kuhusu ununuzi wa mbolea k...
-
Mvua kubwa za El-Nino zilizonyesha zimeleta athari maeneo mbalimbali...
Powered by Blogger.
0 comments:
Post a Comment