KWENYE mpira wa miguu inasemwa kwamba shabiki ni mchezaji wa 12 uwanjani.
Kwa maana anavyoshangilia zile kelele zinaongeza hamasa kwa
wachezaji. Tanzania huwa kuna tatizo la ushangiliaji, mashabiki wa soka
wamezoea kushangilia pale tu linapofungwa bao au mchezaji wa timu husika
anaposhambulia lango la wapinzani. Tatizo hili lipo pote si kwenye timu
za taifa wala kwenye klabu. Tena kwenye timu ya taifa ndio kabisa
mashabiki wanaweza kuanza kusomea ama kushabikia timu pinzani kisa tu
timu yao inacheza vibaya siku hiyo.
Ilipokuja timu ya TP Mazembe kucheza na Simba kwenye michuano ya Ligi
ya Mabingwa mwaka 2011 hamasa ya ushangiliaji ilianzia pale. Mashabiki
wa Tanzania walifurahi jinsi vikundi vya ushangiliaji vilivyokuwa
vikishangilia kuanzia dakika ya kwanza ya mchezo mpaka ya mwisho.
Hawakuwa wakiwafikia wale wa Liverpool lakini angalau walikuwa
wakishangilia na kuwafanya wachezaji wao kujiona wako pamoja uwanjani.
Ndipo baadhi ya mashabiki wa soka nchini walipoamua kuanzisha kikundi
cha hamasa kwa timu za taifa ambapo kilianza mwishoni mwa mwaka jana.
Kundi hilo linalojulikana kama Taifa Stars Supporters limekuwa
likihamasishana kusafiri na timu za taifa nje ya nchi zikiwa na vigoma
vyao kwa ajili ya kuzishangilia na hakika limekuwa kundi muhimu kwa timu
za taifa kuanzia za vijana mpaka za wakubwa kwa upande wa wanawake na
wanaume.
Hata hivyo, kikundi hicho kimekuwa hakina mtu wa kukipa msaada zaidi
ya kuchangishana wenyewe kufanikisha safari za kwenda uwanjani, kupokea
timu uwanja wa ndege au kusafiri kwa nchi za karibu kama Zambia, Kenya,
Uganda. Ndipo kampuni ua Platinum Credit inayohusika na mikopo ilipoamua
kujitosa kusaidia kikundi hicho japo kwa kutoa fulana kwa ajili ya
wanachama wake.
“Tunawashukuru sana Platinum Credit kwa moyo wao wa kizalendo ambao
wamekuwa wakitusaidia ili tuweze kutimiza majukumu yetu ya kuzishangilia
timu zetu za Taifa, kama wote tunavyojua ushangiliaji ni moja ya sehemu
ya uchezaji ambao unachochea matokeo mazuri uwanjani… “Kikundi chetu
ndio kiko kwenye kujijenga nia nikurudisha uzalendo uliokuwa umepoa
kwenye michezo, hivyo wadau mbalimbali wajitokeze kuhakikisha kwamba
tunakuwa na moyo na kuzipenda timu zetu za Taifa ambazo kiukweli kila
mmoja ana jukumu la kuhakikisha zinafanya vizuri kwa maslahi ya- Taifa,”
ndivyo anavyoanza kusema Mwenyekiti wa kundi hilo Godson Karigo katika
mahojiano maalumu na gazeti hili.
Anasema ilitokea tu walikutana mashabiki wachache wa soka wakaamua
kuja na kitu hicho ili kurudisha morali ya mashabiki wa soka kwa
kushangilia timu zao na kweli jambo hilo likafanikiwa.
“Kwanza tulianza
kwenye kuunda kundi la Whatsap, humo ndipo tulipokuwa tukijadili namna
ya kufanya, kundi hilo kila mtu anayejisikia kuwa mwanakikundi anatoa
namba yake anaungwa, tulijadiliana na mwisho tukafanya mkutano wa kwanza
ambapo baadae tukatengeneza katiba na kusajili umoja wetu, kwa hiyo
tupo kihalali na tumesajiliwa,” anasema.
Sasa kikundi hicho maarufu chini ya Mwenyekiti Karigo kimekuwa
kikionesha uzalendo wa hali ya juu katika ushangiliaji wa timu za Taifa
bila kujali aina ya matokeo uwanjani. Ni wazi kwamba kuwepo kwa kikundi
hicho kimeongeza hamasa kubwa na kuibua uzalendo upya kwa wananchi na
sasa imeanza kuwa kawaida kuona watanzania wakiendelea kushangilia timu
zao mwanzo wa mchezo hadi mwisho.
Mara zote unapokuwa uwanjani kikosi hicho kimekuwa kikitoa hamasa
mwanzo wa mchezo hadi mwisho, kitu ambacho hakikuwepo kabisa katika soka
la hapa nyumbani. Akizungumza na namna wanavyoendesha kikosi hicho,
Karigo anasema mara nyingi wamekuwa wakijitolea kuhakikisha vijana
wanawezeshwa kufika katika eneo la kutoa hamasa iwe uwanjani kwa ajili
ya mechi au uwanja wa ndege kupokea timu inaporejea kutoka nje ya nchi
kushiriki michuano mbalimbali.
“Mpaka sasa bado tunaendesha kikundi kwa kuchangishana pesa kutoka
mifukoni mwetu nia yetu ni kuhakikisha timu zetu kujituma na kujua
kwamba zina deni kwa watanzania ambao tuna kiu ya kuhakikisha siku moja
tunafanikiwa sana kisoka,” anasema. “Ndio maana hata timu zinapokuwa
zinacheza mechi zake nchi za jirani tunaanza kuchangishana na
kuisindikiza timu, hii yote lengo lake ni kuhamasisha soka letu”.
“Tunaomba wadau wengine wengi wajitokeze kuunga mkono juhudi za hiki
kikundi ambacho kwa sasa kina vijana wanaozidi 400 wako tayari kutumika
kuhamasisha... “Ukifuatilia mafanikio ya vikundi vya ushangiliaji kwenye
timu za Taifa za wenzetu utaona ambavyo vimechangia kwa kiasi kikubwa
kupatikana kwa matokeo mazuri, mpira unachezwa uwanjani na wachezaji 11,
lakini jukwaani huwa kunahesabika ni mchezaji wa 12 kwani inaaminika
kabisa ushangiliaji ni chachu ya ushindi”.
Katika mapokezi ya timu ya soka ya Taifa ya wanawake iliyochukua
ubingwa wa Kombe la Chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati
iliyofanyika Jinja, Uganda, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
michezo Nape Nnauye anasisitiza wadau kujitokeza katika kuhamasisha timu
za Taifa ikiwemo ushangiliaji ambao unaongeza hamasa katika kuleta
mafanikio kwenye soka.
Nape alionyesha kuvutiwa zaidi na juhudi zinazofanywa na kikundi cha
stars Suportes kwa kujituma kuzishangilia timu za Taifa ambazo kwa
hakika mafanikio yake ni faida kwa nchi nzima. Kwa kuonesha kwamba
anaunga mkono kikundi hicho alimwahidi shabiki maarufu wa ushangiliaji
katika michuano ya Ndondo maarufu kama Chifu kwamba aandae hati ya
kusafiria ili awe anasafiri na timu za taifa ikienda nchi jirani.
Saturday, October 22, 2016
KARIBU TUME YA MAENDELEO YA USHIRIKA
Popular Posts
-
📌 Asema Rais, Dkt. Samia anafanya kazi kubwa ya kuwaunganisha Watanzaia 📌 Atak...
-
Wafanyakazi wanawake wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Dodoma, wakiwa wamejipanga tayari kwa maandamano katika maadhimisho ya S...
-
Katibu Mkuu wa Wizara ya kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma Katibu Mkuu wa Wizara ya kilim...
-
Waziri wa Kilimo Mhe Prof Adolf Mkenda akifurahia jambo pamoja na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) ...
Powered by Blogger.
0 comments:
Post a Comment