METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, October 22, 2016

Mahiga: Nchi za SADC zipambane na ugaidi


NCHI wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) zimetakiwa kupambana na ugaidi, uhamiaji haramu, uharamia na biashara haramu za watu ili kutengeneza mazingira bora ya amani na utulivu katika nchi zao.

Mwito huo ulitolewa jana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga wakati akifungua mkutano ulioshirikisha mabalozi wa nchi za Umoja wa Ulaya (EU) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), jijini Dar es Salaam.

Alisema ni jukumu la kila nchi, kukabiliana na changamoto hizo, zinazohatarisha usalama huku akizitaka nchi mwanachama kushirikiana kikamilifu.

Balozi Mahiga alisema watu wanaojihusisha na biashara hiyo, wanafahamika na wanafahamiana na kusisitiza kuwa iwapo kila nchi itajitahidi kuwakamata, mafanikio yatapatikana.

Alitaka wahakikishe kuwa wanatumia mkutano huo, kujadili mbinu mpya za kiintelijensia zitazotumika kukabiliana na wale wote wanaojihusisha na uhalifu wa aina hiyo.

Alisema, kuwa zipo sababu zinazohatarisha usalama wa nchi za SADC na dunia nzima, ambazo hazitokani na ukosefu wa ulinzi au usalama mwingine wowote, ila zinasababishwa na mazingira, ambapo alitaka yote hayo kushughulikiwa.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com