KIU ya Rehema Mwilu (16), ni kusoma na anatamani apate fursa hiyo ili atimize ndoto zake za kuwa mwalimu.
Lakini ni mwaka wa tatu sasa yuko nyumbani, akisubiri bahati yake
huenda msamaria, akajitokeza ili kumwezesha kwenda shule kusoma. Rehema
ni binti anayeishi Mtoni Kijichi, Dar es Salaam.
Alihitimu elimu ya
msingi katika Shule ya Msingi Mtoni Kijichi mwaka 2013 na kufaulu.
Alichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari
ya Kibada. Hata hivyo, hakuweza kuripoti shuleni kutokana na ugumu wa
maisha, uliosababisha aendelee kukaa nyumbani hadi leo.
Ni mtoto wa tatu kuzaliwa akiwa msichana pekee kati ya watoto watano
wa familia ya Ally Mwilu (47) na mama Hadija Makongo (39). Ndugu zake
Rehema ni Hussein Mwilu ambaye ni mtoto wa kwanza, Nashiri Mwilu wa
pili, Selemani wa nne ambaye anasoma elimu ya msingi na Baraka ni
kitinda mimba, yeye bado ni mdogo.
Kati ya ndugu zake hao wawili wakubwa, hawakuchaguliwa kuendelea na
masomo ya sekondari, baada ya kuhitimu elimu ya msingi , na hivi sasa
kila mmoja anajitegemea na kufanya shughuli ndogo zinazowasaidia
kujikimu na wakati mwingine kusaidia familia yao.
Kwa miaka yote mitatu, binti huyo amekuwa akiwaza kuwa ipo siku
atasoma, na hiyo ni moja na sababu ya yeye kukataa kuozwa na wazazi
wake, kwa kuwa bado anaamini kuwa iko siku atasoma, na elimu hiyo kuwa
mkombozi wa maisha yake.
Mkasa wa binti huyo ni funzo kwa wasichana wengine wenye kiu ya elimu
kwa sababu, pamoja na ugumu wa maisha hajakata tamaa wala kujiingiza
kwenye makundi yasiyofaa, bali ameendelea kujitunza akiamini iko siku
atasoma na kuwa mwalimu.
Sauti ya Rehema
Siku moja Nashiri, kaka yake Rehema, alimpelekea mama yake magazeti
mbalimbali ayasome, kwa kuwa hupenda kusoma magazeti. Na miongoni mwa
magazeti hayo, kulikuwa na gazeti la HabariLeo.
Baada ya Rehema kuyaona, alipekua na kubahatika kuona mawasiliano ya
viongozi wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali ya TSN, kwenye gazeti la
HabariLeo, kisha akaamua kupiga namba za simu zilizoandikwa, akiamini
kuwa kiu yake ya elimu itafanikiwa.
“Nilifungua magazeti tofauti, ila nilipofungua gazeti la HabariLeo
niliona kuna sehemu zimeandikwa namba za simu mbalimbali za viongozi,
nilipiga namba mojawapo ya Voda, ila nikakata kwa sababu nilijua
sitaweza kuongea kwa kirefu itaisha salio kwa sababu ninatumia mtandao
wa Tigo, hivyo niliamua kupiga namba nyingine ya Tigo na kufanikiwa
kuzungumza na mmoja wa viongozi”, alisema Rehema.
Baada ya kuwasiliana na mmoja wa viongozi wa Kampuni hii, Rehema
alielekezwa mahali ofisi zilipo na kufika kisha kuelezea maisha yake, na
ndipo hatua ya kutafuta ukweli wa jambo hilo, ikaanza kwa kufuatilia
kuanzia shule ya msingi aliyosoma hadi shule ya sekondari aliyopangiwa
na nyumbani kwao na hata kwenye Ofisi ya Serikali ya Mtaa wake.
Rehema alisema baada ya kuhitimu masomo mwaka 2013, alifaulu kujiunga
na kidato cha kwanza, ila hakuweza kuripoti shuleni kwa sababu ya hali
duni ya wazazi wake na huo ukawa mwanzo wa yeye kukaa nyumbani hadi leo.
“Nilimaliza elimu ya msingi mwaka 2013, nikachaguliwa kujiunga na
kidato cha kwanza ila sikuweza kwenda shule kwa sababu wazazi wangu
hawana uwezo na shule ilikuwa mbali, ila mimi nataka kusoma sitaki
kuolewa na nilikataa mchumba kwa sababu ndoto zangu ni elimu kwanza”,
alisema Rehema.
Akielezea jinsi alivyokataa kuozwa, Rehema alisema, baada ya kukaa
nyumbani mwa muda, alitokea mwanamume aliyezungumza na wazazi wake na
kupeleka barua ya posa na wazazi wakamtaka Rehema aridhie kuolewa kwa
sababu hana pa kwenda.
“Alikuja mtu nyumbani na wazazi wanasema kaleta barua ya posa hivyo
nikubali kuolewa, ila nilikataa na kusema ninataka kusoma, na hapo ndipo
wazazi wangu wakakasirika na kuniambia shauri yangu nitajijua mwenyewe,
ila sikukata tamaa ninajua iko siku nitasoma”, alisema Rehema.
Safari ya kuusaka ukweli
Maelezo ya Rehema yalinifanya nifunge safari pamoja na Rehema hadi
Shule ya Msingi Mtoni Kijichi na kujitambulisha, kisha kueleza lengo la
safari yangu, maelezo yaliyowaridhisha walimu na kufanikiwa kuzungumza
na Mwalimu wa Taaluma shuleni hapo, Mary Kivyiro.
Mwalimu Kivyiro alimhoji Rehema maswali machache na Rehema aliyajibu
kwa kujiamini, huku mmoja wa walimu aliyemfundisha Rehema akitokea na
kumchangamkia. Baada ya mahojiano hayo, Mwalimu Kivyiro aliangalia
kwenye kumbukumbu za shule na kuthibitisha kuwa ni kweli Rehema alisoma
shuleni hapo na alichaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari Kibada.
“Ni kweli Rehema Ally Mwilu alikuwa mwanafunzi wetu aliyemaliza mwaka
2013 na namba yake ni PS 0206054/255 alikuwa miongoni mwa wanafunzi 196
waliochaguliwa kijiunga na kidato cha kwanza mwaka 2014, sasa kama
hakwenda kuripoti shuleni sisi hatukupewa taarifa”, alisema Mwalimu
Kivyiro na kuongeza… … ila kama angerudi kusema wazazi wameshindwa
kumpeleka shule wakati ule ule alipochaguliwa, uongozi wa shule
ungemsaidia kwa kutoa taarifa kwa Ofisa Elimu, ambaye angemsaidia, ila
ndio kwanza unatuambia habari hizi leo, wenzake wako kidato cha tatu
sasa”, alisema Mwalimu Kivyiro.
Safari ya kuelekea Sekondari ya Kibada
Baada ya kuthibitishiwa hayo, safari ya kuelekea Shule ya Sekondari
Kibada ilifuata na kufanikiwa kuzungumza na Kaimu Mkuu wa Shule,
Fulgence Daudi ambaye alithibitisha kuwa Rehema Mwilu alichaguliwa
shuleni hapo, ila taarifa zinaonesha hakuripoti shuleni.
‘Ni kweli tuna jina la Rehema Ally Mwilu ambaye alipangiwa hapa
kujiunga kidato cha kwanza mwaka 2014, ila hakuripoti na kwa sababu
zisizofahamika na kwa mujibu wa taratibu kama ameshindwa kuhudhuria
ndani ya siku 90, huwa anajiondoa kuwa mwanafunzi kwa sababu hatukuwa na
taarifa zake”, alisema Mwalimu Daudi.
Hata hivyo, alisema kinachowezekana kumsaidia binti huyo ni yeye
kuandika barua kwa Mkurugenzi wa Manispaa husika, barua ipitie kwa Ofisa
Elimu Sekondari kupitia kwa mkuu wa shule alikochaguliwa, na ieleze nia
yake ya kuomba kusoma na aweke viambatanisho vya sababu iliyomzuia
awali ashindwe kusoma, na kama kuna sababu nyingine aziandike.
“Barua hiyo ipitie shuleni ili mkuu wa shule ya msingi aliyosoma,
athibitishe kuchaguliwa kwa mwanafunzi huyo na kisha itaenda ngazi
husika, na pia kama ni tatizo la kifamilia na ameshindwa kusoma mbali,
kwenye barua iandikwe na aombe shule ya karibu itakayomsaidia yeye na
changamoto za familia yake’’, alisema Mwalimu Daudi.
Changamoto za elimu
Mwalimu Daudi alisema bado kuna changamoto kwa baadhi ya wazazi na
walezi kwenye maeneo mbalimbali, yakiwemo ya Pwani, kutokuwa na mwamko
wa elimu kwa watoto wao na hupenda zaidi kuthamini sherehe za mila na
tamaduni, ambazo wakati mwingine huwalazimu wanafunzi kuacha masomo na
kuhudhuria.
Hodi nyumbani kwa akina Rehema
Gazeti hili lilifika pia nyumbani kwa familia ya Rehema eneo la Mtoni
Kijichi na kuzungumza na wazazi wake, ambao walisema tatizo kubwa
lililokwamisha elimu ya binti yao ni umasikini.
“Tulipenda sana binti yetu asome, ila umasikini ndio ulinikwamisha,
ingekuwa ni kipindi hiki angeweza kusoma kwa sababu hakuna ada serikali
inagharimia , ila natamani asome na yeye anapenda ila hatuna jinsi na
mama yake ni mgonjwa , hivyo familia ya watoto sita ninaihudumia
mwenyewe kwa kuuza mkaa”, alisema baba yake Rehema, Mwilu.
Mwilu anauza mkaa, ambapo hutumia baiskeli yake kufuata gunia moja au
magunia mawili wilayani Mkuranga na kisha kurejea kuuza, ili kupata
fedha za kuendeshea familia kwa sababu mkewe ni mgonjwa wa tumbo na
hawezi kufanya kazi, kwa sababu mwili umevimba na inakuwa tabu kutembea.
Mama yake mzazi Rehema, Hadija alisema awali baada ya mtoto wake
kuchaguliwa, alifanya juhudi za kuomba uhamisho kupitia kwa ofisi ya
diwani, ila hakufanikiwa na alipofika shuleni Kibada, alifafanuliwa
gharama za ada na michango mingine inayofikia Sh 180,000.
“Baada ya kuambiwa gharama hizo, kwa kweli sikuwa na jinsi, kwa
sababu ni fedha nyingi na familia yangu haina uwezo, ilibidi tu Rehema
abaki nyumbani”, alisema Hadija, mama mzazi wa Rehema, ambaye pia
alikiri familia ilipokea barua ya posa ila binti yao alikataa. “Ni kweli
mchumba alijitokeza na binti yetu alikataa, na sisi hatukumlazimisha”,
alisema Hadija mama mzazi wa Rehema.
Posa ya Rehema
Akielezea ilivyokuwa hiyo posa, Rehema alisema yeye anataka kusoma na
kwamba wazazi wake walimtaka aolewe baada ya mchumba kuleta barua ya
posa nyumbani ambayo wazazi waliiridhia.
“Ililetwa barua ya posa na wazazi wakaridhia kwa kumtaka huyo mchumba
aje anione, na alipokuja mimi sikukubali kuolewa kwa sababu malengo
yangu ni kusoma na sio kuolewa kwa umri huu”, alisema Rehema.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa anena Naye Mwenyekiti wa Serikali ya
Mtaa wa Butiama anakoishi Rehema, Haji Mgaya alisema anamfahamu binti
huyo na aliuliza iwapo anasoma na kuambiwa anajifunza ufundi wa kushona,
ila hakuambiwa kama binti huyo alitaka kuozwa.
Msaada wako
Binti Rehema ni jasiri na kitendo cha yeye kupiga simu kuomba msaada
wa kusomeshwa, kinaonesha kiu aliyonayo ndani ya moyo wake, kwani pamoja
na yeye kupenda shule, wenzake aliomaliza nao elimu ya msingi hivi sasa
wako kidato cha tatu, na wamekuwa wakimcheka wakidhani alikataa shule,
la hasha!
Ni changamoto na umasikini wa familia yake, ndivyo vimemkwamisha.
Lakini, hajachelewa, unaweza kubadilisha maisha yake kwa kumsaidia
Rehema atimize ndoto zake za kuwa mwalimu, ili aelimishe wengi kuhusu
haki ya elimu hususan kwa mtoto wa kike. Watakaoguswa, wawasiliane na
uongozi wa gazeti hili jinsi ya kumpata Rehema.
Saturday, October 22, 2016
KARIBU TUME YA MAENDELEO YA USHIRIKA
Popular Posts
-
📌 Asema Rais, Dkt. Samia anafanya kazi kubwa ya kuwaunganisha Watanzaia 📌 Atak...
-
Mvua kubwa za El-Nino zilizonyesha zimeleta athari maeneo mbalimbali...
-
Wafanyakazi wanawake wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Dodoma, wakiwa wamejipanga tayari kwa maandamano katika maadhimisho ya S...
-
Waziri wa Kilimo Mhe Prof Adolf Mkenda akifurahia jambo pamoja na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) ...
Powered by Blogger.
0 comments:
Post a Comment