Mwendesha Mashataka mkuu wa ICC Fatou Bensouda
Siku
chache zilizopita Burundi na Afrika Kusini zilitangaza kujiondoa
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) na sasa Mahakama hiyo inasema ni
vyema kukawa na majadiliano ya kina juu ya hatua hiyo kuzuia wengine
kujitoa.
Siku
chache baada ya Afrika Kusini na Burundi kutangaza kujiondoa katika
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC, ya mjini The Hague, Uholanzi,
sasa Mahakama hiyo inataka mdahalo na mataifa hayo na mengine yenye azma
kama hiyo ikisema imesikitishwa na hatua hiyo huku zikiweko khofu hasa
kwa upande wa mashirika ya kutetea haki za binadamu duniani kwamba nchi
za Kiafrika huenda zikaanza kujiondowa kwa wingi kutoka ICC.
"Ni
masikitiko makubwa katika bara la Afrika" hivyo ndivyo alivyosema Rais
wa Baraza la Nchi Wanachama wa Mkataba wa Roma uliounda mahakama hiyo ya
ICC hapo jana, kufuatia uamuzi wa Burundi na Afrika Kusini kujiondoa
kwenye chombo hicho cha kimataifa cha sehria dhidi ya wahalifu wa
kivita.
Sidiki
Kaba, ambaye pia ni waziri wa sheria wa Senegal, amesema jumuiya ya
kimataifa itafanya kila iwezalo kuchukua hatua kabambe za kuhakikisha
kwamba nchi hizo mbili zinatafakari upya hatua ilizochukua, akisisitiza
kutumia njia ya majadiliano kulitatua hilo.
Jijini
New York, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon amesema naye
amesikitishwa na uamuzi wa Afrika Kusini kujiondoa ICC na kuitolea mwito
nchi hiyo kufikiria tena uamuzi wake huo kabla ya kuanza utekelezaji wa
kujiondoa kwake katika chombo hicho.
Akitoa
msimamo huo wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, msemaji wake, Stephane
Dujarric, amesema Ban Ki-moon anaaamini kwamba ICC ni chombo kikuu
duniani kinachofanya juhudi za kupambana na viongozi au watu
wasioshtakiwa kutokana na nafasi zao. "Kadhalika ni chombo kinachofanya
juhudi kubwa kukabiliana na mizozo," amesema Dujarric.
Maandamano ya kumpinga rais Nkurunzinza mwaka 2015
Mkurugenzi
Mkuu wa shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human
Rights Watch, Richard Dicker, pia ameitolea wito Afrika Kusini kuangalia
upya msimamo wake. Afrika Kusini ilitangaza siku ya Ijumaa kwamba
itajiondoa ICC, ikisema uanachama wake ndani ya chombo hicho unazuia
juhudi za kusaidia kuitatua migogoro katika bara la Afrika.
Burundi
nchi inayozongwa na mgogoro, ilipiga kura kupitia bunge kuunga mkono
kujiondoa ICC na wiki iliyopita Rais Pierre Nkurunziza akaweka saini
kwenye azimio hilo.
Baadhi ya
wachambuzi wa masuala ya kisheria na siasa katika bara la Afrika
wanahisi kwamba bara hilo linataka kuonesha ubabe wake mbele ya jumuiya
ya kimataifa kwa kuzipinga taasisi za jumuiya hiyo ili kuendeleza
ukiukaji wa haki za binadamu pamoja na kutowajibikia uhalifu wanaoufanya
dhidi ya wananchi wao.
Hata
hivyo mitazamo pia inatofautiana kuhusu dhima ya mahakama ya ICC
kuelelekea bara la Afrika na viongozi wake. Barani Afrika hisia
zilizoenea ni kwamba mahakama hiyo imekuwa ikiwaandama kionevu viongozi
wa kiafrika kuliko inavyofuatilia masuala ya mabara mengine.
DW
0 comments:
Post a Comment