METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, October 8, 2016

BWENI LA WASICHANA MORETO SEKONDARI LA TEKETETEA KWA MOTO

BWENI la wanafunzi wasichana katika shule ya sekondari ya Moreto iliyopo tarafa ya Msoga wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, baada ya kuungua kwa moto na kusababisha mali zote za wanafunzi hao kuteketea kwa moto. (Picha na Mwamvua Mwinyi)
Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo


MBUNGE wa jimbo la Chalinze, mkoani Pwani, Ridhiwani Kikwete, ametoa magodoro 50, yenye thamani ya sh.mil 2.225 kwa wanafunzi wa kike wa shule ya Sekondari Moreto, waliounguliwa na bweni lao na kusababisha mali zote kuteketea kwa moto.

Wanafunzi hao wapatao196, katika shule hiyo iliyopo kata ya Lugoba tarafa ya Msoga, wilaya ya Bagamoyo, wamenusurika kifo baada ya bweni hilo kuteketea kwa moto siku ya oktoba 5.

Moto huo umeteketeza mali zote zilizokuwemo ambazo hadi sasa hazijajulikana thamani yake.

Kufuatia kutokea kwa tukio hilo, Ridhiwani alifika shuleni hapo kutembelea na kutoa pole kwa kutokea janga hilo.

Alisema wakumshukuru ni mungu kwani pamoja na kutokea kwa hasara ya kuteketea kwa mali lakini hakuna madhara kwa wanafunzi yaliyotokea.

Ridhiwani aliwapa pole walimu na wanafunzi kijumla na kuwaomba wadau wengine kujitokeza kwenda kusaidia pale watakapojaaliwa.

Kwa mujibu wa mwalimu mkuu wa shule ya sekondari Moreto, Justine Lyamuya alielezea kuwa, tukio hilo limetokea oktoba 5,majira ya asubuhi ambapo walianza kuona moshi mzito katika bweni mojawapo wanaloishi wasichana wa shule hiyo.

Alisema wakati moto huo unazuka wanafunzi hao walikuwa kwenye masomo yao darasani.
"Tulifuatilia na kukuta moto umeshashika kwenye bweni hilo na jitihada za kuuzima zilishindikana"alisema mwalimu Lyamuya.

Lyamuya alisema mali zote za wanafunzi wanaolala kwenye bweni hilo zimeteketea kwa moto hivyo kwa sasa wanafanya tathmini kujua gharama zilizopotea.

Katika hatua nyingine jeshi la polisi mkoani Pwani linafanya uchunguzi wa tukio hilo ili kubaini chanzo cha moto.

Kamanda wa polisi mkoani Pwani, Boniventure Mushongi, alielezea kuwa mazingira ya jengo hilo ni yenye kutumia nishati ya solar power hivyo ni lazima kufanya uchunguzi wa kina kujua kiini cha kuzuka kwa moto huo.

Alisema bweni hilo linakadiriwa kuwa na wanafunzi 196.
Kamanda Mushongi alisema thamani za mali za wanafunzi katika moto huo bado hazijafahamika.

Mwisho
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com