Wakurugenzi wazuiwa kujipangia tozo kwa wafugaji wa ng’ombe
SERIKALI imesema ni marufuku kwa mkurugenzi yeyote wa halmashauri kujipangia kiasi cha fedha cha kuwatoza wafugaji wa ng’ombe kwa ajili ya wanyama hao kupigwa chapa bila ya kuwashirikisha wafugaji na kwamba, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) anatarajiwa kuwasilisha marekebisho ya sheria bungeni kwa ajili ya kuondoa tozo zote za kodi zisizo na tija.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene pamoja na Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Ole Nasha wakati wakichangia mjadala wa kuhitimisha hoja ya makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2017/18.
Akizungumza bungeni hapo, Simbachawene alisema Serikali za Mitaa zimejipanga kuhakikisha zinawajengea uwezo wananchi ili waishi maisha bora kwa kuwawekea maisha wezeshi ya kufanya biashara zao.
“Tumegundua kuna tatizo la kodi kutozwa mara mbili kwa jambo moja, tozo kufanana, tozo kutozwa kwenye mitaji badala ya faida, na tayari Rais John Magufuli alisisitiza juu ya muhimu wa tozo zinazowakandamiza masikini kuondolewa,” alisema.
Alisema kuanzia sasa ushuru au tozo zisizozingatia mazingira ya uzalishaji zinazolenga kunufaisha wachache na zisizo na tija kwa taifa zitaondolewa kupitia marekebisho hayo ya sheria.
“Haya yote tumeyazingatia, AG ataleta mabadiliko ya sheria, nawahakikishia tumepitia tozo zote na zile zisizofaa zitaletwa hapa, zitabadilishwa,” alisisitiza. Alitoa mfano kuwa tozo kama zile zinazowakandamiza wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo nazo zitaangaliwa na ikibidi kufutwa kama zilivyofutwa tozo 108 katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.
0 comments:
Post a Comment