Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa
maelekezo kwa mkandarasi Nyanza Road Construction inayojenga barabara ya
Furahisha hadi Pasiansi KM 2.8 wakati alipokagua ujenzi wa barabara
hiyo, jijini Mwanza.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amemtaka
Mkandarasi wa kampuni ya Beijing Construction Engineering Group
anayejenga uwanja wa ndege wa Mwanza kumaliza kazi ya upanuzi wa uwanja
huo ifikapo mwezi Februari Mwakani.
Profesa
Mbarawa ametoa kauli hiyo alipokuwa akikagua kazi ya ujenzi na upanuzi
wa uwanja wa ndege wa Mwanza pamoja na daraja la watembea kwa miguu
lililopo maeneo ya furahisha, jijini Mwanza.
Profesa
Mbarawa amesema kuwa kukamilika kwa ujenzi na upanuzi wa uwanja huo
kutaimarisha hali ya usafiri wa anga kwa wakazi wa Mwanza na mikoa
mingine na hivyo kukuza shughuli za kibiashara nchini.
“Hakikisheni
upanuzi wa uwanja wa ndege huu unakamilika haraka ili kurahisisha na
kuboresha huduma za usafirishaji kiwanjani hapa”, alisema Waziri Mbarawa.
Aidha,
Profesa Mbarawa amemtaka mkandarasi wa kampuni ya Nyanza Road
Construction kumaliza kwa wakati upanuzi wa barabara ya ‘Mwanza-Airport’
eneo linaloanzia Ghana Quarters hadi Uwanja wa Ndege wa Mwanza KM 9.15
pamoja na daraja la watembea kwa miguu la furahisha ili kukuza uchumi na
kupunguza kero ya msongamano wa magari katika jiji la Mwanza.
Katika
hatua nyingine Prof. Mbarawa amewataka wananchi wa Mwanza kutoharibu
miundombinu ya barabara na madaraja ambayo Serikali inatumia gharama
kubwa katika utengenezaji wake.
“Naomba muitunze na kuithamini miundombinu hii kwani Serikali inatumia gharama kubwa katika kutengeneza na kukarabati”, alisisitiza Prof. Mbarawa.
Ujenzi
wa uwanja wa ndege wa Mwanza ni mkakati wa Serikali kuhakikisha ujenzi
wa uwanja huo unaboreshwa kuwa wa kisasa na wa kimataifa ili kuwezesha
ndege kubwa kutua kwa wingi na kuwa kiungo muhimu kwa mikoa 10 ya kanda
ya Ziwa na Kati.
Mkandarasi
wa kampuni ya Nyanza Road Construction inayojenga barabara ya Furahisha
hadi Pasiansi akitoa maelezo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa wakati alipokagua ujenzi wa barabara
hiyo jijini Mwanza.
0 comments:
Post a Comment