METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, September 16, 2016

Shilingi bilioni 6.6 zatumika kunufaisha kaya maskini Dar es Salaam

taw
Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam Theresia Mmbando

Na. Abushehe Nondo & Frank Shija

JUMLA ya kaya 26,248 zimenufaika na mpango wa kunusuru kaya maskini (TASAF III) kwa kupatiwa jumla ya shilingi Bilioni 6.6 katika mkoa wa Dar es Salaam.
Hayo yamebainishwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam Theresia Mmbando wakati akiongea na waandishi wa habari jana Jijini Dar es Salaam.

Mmbando amesema kuwa utambuzi wa kaya maskini ulianza mwezi Januari 2015 kwa kushirikisha wilaya za Kinondoni, Temeke na Ilala ambapo jumla ya kaya 26,248 zilizoandikishwa na kupokea ruzuku  kila baada ya miezi miwili kwa kuzingatia mzunguko wa malipo.

Aliongeza kuwa wanufaika wa mpango huo wamepatikana kutokana na ushirikishwaji wa jamii husika ambapo jamii yenyewe ilibainisha majina ya walengwa katika maeneo yao.

Aidha Mmbando amesema kuwa pamoja na mafanikio hayo kuna baadhi ya changamoto zilizojitokeza katika kutekeleza mpango huo ikiwemo baadhi ya kaya zilizokidhi vigezo kukataa kuandikishwa, kuandikishwa kwa kaya zisizokuwa na sifa, pamoja na kupokea ruzuku pungufu.

Katika kukabiliana na changamoto hizo, Mmbando amesema mpaka sasa jumla ya kaya 609 zimeondolewa katika kwenye mpango huo ikiwemo kaya 141 (Ilala), kaya 296 (Kinondoni) na kaya 172 (Temeke).

Kwa upande wake Mratibu wa TASAF Mkoa wa Dar es Salaam, Esterine Sephania amesema kuwa suala la udanganyifu wa kuandikishwa kwa walengwa wasiokuwa na sifa linaanzia katika ngazi ya serikali za mitaa ambapo huko ndiko wanaleta majina.

Aliongeza kuwa kutokana na udanganyifu uliojitokeza katika zoezi hilo takribani shilingi milioni 2.2 zimepotea kupitia udanganyifu uliotokana na uandikishwaji kwa watu wasiokuwa na vigezo.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com