
Mkurugenzi
Idara ya Huduma za Kisheria wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Bw.
Emmanuel Kawishe akitoa ufafanuzi kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya
Wasichana ya Songe nje kidogo ya mji wa Musoma juu ya majukumu na
utendaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kama ilivyoainishwa kwenye
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa uzinduzi wa programu
endelevu ya utoaji wa elimu ya mpiga kura kwa kuyafikia makundi
mbalimbali nchini.

Mkurugenzi
wa Idara ya TEHAMA wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Mhandisi Manyiri Isaya
akitoa ufafanuzi kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya
Songe nje kidogo ya mji wa Musoma juu ya daftari la wapiga kura na namna
taarifa za wapiga kura zinavyotumika kwenye chaguzi mbalimbali. Kulia
ni Mkurugenzi Idara ya Huduma za Kisheria wa NEC, Bw. Emmanuel Kawishe.

Mkuu wa
Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga kura wa NEC, Bi. Giveness Aswile
akiwaeleza wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Songe Musoma
mfumo unaotumiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) katika kuwawezesha
watu walio katika makundi maalum hasa watu wenye ulemavu wenye sifa
kupiga kura kupitia karatasi maalum.

Wanafunzi
wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Songe iliyoko nje kidogo ya mji
wa Musoma wakionesha vipeperushi na machapisho mbalimbali waliyopewa na
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa lengo la kuwawezesha kuongeza uelewa
juu ya majukumu ya Tume wakati wa uzinduzi wa program endelevu ya
utoaji wa elimu ya mpiga kura mjini Musoma.

Mwanafunzi
wa kidato cha Sita wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Songe, Musoma
akiwauliza swali Maofisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (hawapo pichani)
juu ya matumizi ya TEHAMA katika kuwabaini wananchi waliojiandikisha
kwenye kituo cha kupigia kura zaidi ya kimoja.

Baadhi
ya wananfunzi wa shule ya Sekondari ya wasichana na Songe nje kidogo ya
mji wa Musoma, wakifuatilia kwa makini elimu ya Mpiga kura iliyokuwa
ikitolewa na Maofisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) katika shule
hiyo wakati wa uzinduzi wa program ya utoaji wa elimu ya mpiga kura kwa
wananchi.

Baadhi ya
wananfunzi wa shule ya Sekondari ya wasichana na Songe, Musoma
wakipitia machapisho mbalimbali ya elimu ya Mpiga kura yaliyotolewa na
Maofisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) katika shule hiyo wakati wa
uzinduzi wa program ya utoaji wa elimu ya mpiga kura kwa wananchi.
Na Aron Msigwa – NEC, Musoma
Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (NEC) imezindua rasmi programu ya utoaji wa Elimu
endelevu ya mpiga kura nchini kwa kutoa elimu hiyo kwa wanafunzi wa
shule ya Sekondari ya wasichana ya Songe iliyoko nje kidogo ya Manispaa
ya Musoma mkoani Mara.
Uzinduzi
wa programu hiyo ni kuanza rasmi kwa mkakati wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata elimu ya mpiga kura ili
kujenga uelewa kuhusu majukumu ya Tume , utendaji wake na uelewa wa
chaguzi mbalimbali zinazofanyika nchini.
Akizungumza
na walimu na wanafunzi wa shule hiyo wakati wa uzinduzi wa program
hiyo, Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Kisheria wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) Bw. Emmanuel Kawishe amesema kuwa NEC imeamua kuwafikia
moja kwa moja wanachi ili iwapatie elimu kuhusu haki na wajibu walio nao
kikatiba pia kuwajengea uelewa wa kutosha kuhusu taratibu zinazosimamia
chaguzi nchini.
Amesema
kuwa programu hiyo imezinduliwa kwa lengo la kuwaelimisha wananchi
kuhusu utendaji wa Tume na kazi za Tume ili kuongeza uelewa miongoni mwa
jamii pia kuiwezesha Tume hiyo kupokea ushauri na maoni ya wananchi.
Bw.
Kawishe ameeleza kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inalojukumu la
kutoa elimu ya mpiga kura kwa mujibu wa Sheria kama ilivyoanishwa katika
kifungu Na 4 (c) cha Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 1985 na kuongeza kuwa
imeanza kuwafikishia elimu ya mpiga wananchi kura moja kwa moja katika
maeneo yao.
Amesisitiza
kuwa NEC imezindua programu hiyo katika shule ya Sekondari ya wasichana
ya Songe ili kuwapatia fursa vijana waliotimiza umri wa kupiga kura na
wale ambao bado hawajatimiza umri huo kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu
chaguzi zijazo.
Aidha,
amewaeleza wanafunzi hao kuwa ili mwananchi aweze kupiga kura lazima
awe amekidhi sifa na vigezo vilivyoainishwa kisheria ikiwemo kutimiza
umri wa miaka 18 na kuendelea, kupiga kura katika kituo
alichojiandikishia kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi kifungu cha 63, kuwa
na utimamu wa akili, kuwa na uraia wa Tanzania na vigezo vingine
vilivyoainishwa kisheria.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi
Mhandisi Manyiri Isaya akitoa ufafanuzi kuhusu matumizi ya TEHAMA katika
kuhifadhi na kutoa taarifa za wapiga kura waliojiandikisha katika
daftari la kudumu la wapiga kura ameeleza kuwa matumizi ya TEHAMA
yamerahisisha utunzaji wa taarifa za wapiga kura na kufafanua kuwa
mwananchi aliyejiandikisha kwenye kituo kimoja cha kupigia kura hawezi
kwenda kupiga kura katika kituo kingine.
“Napenda
ifahamike kwamba kujiandikisha kwenye kituo zaidi ya kimoja kwa lengo la
kupigia kura mara nyingi ni kosa kisheria na mtu huyo anashitakiwa kwa
mujibu wa sheria, Tume tuna daftari la kudumu la wapiga kura
tunapochakata taarifa za wapiga kura huwa tunagundua watu
waliojiandikisha zaidi ya kituo kimoja, tunachofanya sisi tunachukua
taarifa za kituo cha mwisho mtu alichojiandikisha” Amesisitiza.
Mhandisi
Manyiri amefafanua kuwa karatasi za kupigia kura hutolewa kulingana na
idadi ya wapiga kura waliojiandikisha katika kituo husika hivyo hakuna
namna ambayo mwananchi anaweza kupiga kura kwenye kituo zaidi ya kimoja.
Naye Mkuu
wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga kura Bi. Giveness Aswile akitoa
ufafanuzi kuhusu wajibu wa Tume katika kushughulikia watu wenye mahitaji
maalum hasa watu wenye ulemavu ambao wanaokidhi sifa za kupiga kura
amesema kuwa Tume imekuwa ikiweka mazingira rafiki ya kuwawezesha kupiga
kura.
Amesema
kuwa katika uchaguzi uliofanyika Oktoba, 2015 Tume ya Taifa ya Uchaguzi
iliandaa karatasi maalum za kupigia kura na maeneo wezeshi ya kupigia
kura ili kuwawezesha wananchi hao kutumia haki yao ya Kikatiba
kuwachagua viongozi wanaowataka.
“ Tume ya
Taifa ya Uchaguzi katika uchaguzi uliopita tuliweka mazingira mazuri
kwa watu wenye ulemavu, na wale wasioona ambao wana uwezo wa kusoma na
kuandika tukawawekea vifaa na karatasi maalum zenye nukta nundu ambazo
zina majina ya wagombea wa vyama vyote ili kuwawezesha kupiga kura wao
wenyewe bila msaada wa mtu yeyote” Amesisitiza Bi. Aswile.
Ameongeza
kuwa NEC imekuwa ikitoa kipaumbele kwa makundi mengine hasa ya wazee,
mama wajawazito kupata huduma haraka katika vituo vya kujiandikishia na
kupiga kura bila kupanga mstari kama ilivyo kwa wananchi wengine.
Kwa
upande wao walimu na wanafunzi wa shule hiyo wakizungumza kwa nyakati
tofauti kuhusu uzinduzi wa program hiyo katika shule yao wameishukuru
Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuichagua shule hiyo kuwa ya kwanza kupata
elimu ya mpiga kura.
Wamesema
kuwa elimu ya mpiga kura waliyoipata kupitia kwa maofisa wa Tume na
majibu ya maswali waliyouliza imewaongezea ufahamu na kuwajengea uwezo
wa kuwaelimisha vijana wengine kuhusu majukumu ya Tume ya Taifa ya
Uchaguzi na wajibu wao katika kushiriki kwenye chaguzi zijazo.
0 comments:
Post a Comment