METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, September 10, 2016

Kwanini Prof. Lipumba Ni Mjadala Mkubwa?


Ndugu zangu,

Mada niliyoianzisha jana imezua mjadala mkubwa. Nimefutilia kila kilichoandikwa na wajumbe. Ningependa kufanya hapa majumuisho.

Kuna moja kubwa nililolibaini, kuwa wengi waliochangia hawakujihangaisha sana kutaka kuyajua ya jana kwa maana ya historia.

Wengi wamechangia bila kujibu hoja za msingi za Profesa Lipumba, ambazo kimsingi ni nzito na hazina majibu mepesi.

Binafsi ningelipenda sana kuisoma michango ya Wanachama wa CUF, maana, hili la Profesa ni mgogoro wa ndani ya CUF na unahusu Katiba ya chama hicho pia. Nyongeza hapa ni ukweli kuwa kuna kinachoitwa ' Siasa za CUF'. Hizi zina tofauti sana na za CCM, Chadema na wengineo. Kuzijua hizi ni lazima urudi nyuma hadi kwenye matukio ya walau 1984 ili upate mwanga.

Naam, kwa kuyafuatilia yanayoendelea ndani ya CUf, na kama viongozi wakuu wa CUf wasipotanguliza busara, nauona mpasuko mkubwa wa CUf- Bara na CUF- Visiwani.

Haiwezekani leo ikawa rahisi kumweka kando Profesa Lipumba kama ilivyokuwa kwa Mwenyekiti wa kwanza wa Chama hicho James Mapalala. Na hata ilivyokuwa rahisi kwa Musobi Mageni kukaa pembeni na kumpisha Profesa Lipumba kwenye uenyekiti.

Profesa Lipumba ana uungwaji mkono na wafuasi wa kutosha kuimega CUF wakitokea Bara. Ndani yake kuna wenye majina na wafuasi nyuma yao. Ni watu wa aina ya Magdalena Sakaya, Nachuma na Kambaya. Miongoni mwao ni wabunge.

Kumekuwa na manung'uniko ya CUF Bara kuwa CUF kama chama kinaendeshwa kwa msukumo na mashinikizo ya upande wa pili kwa maana ya visiwani. Maalim Seif pia anatupiwa lawama za moja kwa moja na wenye kumuunga mkono Profesa na hususan walio bara.
 
Hakuna namna nyingine iliyo bora ya kuinusuru CUF isimeguke bila kufanyika jitihada za kufanyika juhudi za upatanisho hata kwenye kuutafuta mwisho wa mafahari wawili kukaa zizi moja.

Profesa Lipumba, katika hali ya sasa, na kwa hoja alizoweka mezani, anaonekana dhahiri yuko katika matayarisho ya juu kabisa ya mapambano ya kisiasa.

Ni jukumu pia la Msajili wa vyama vya siasa ambaye pia ni mlezi wa vyama vya siasa, kuandaa mazingira ya upatinishi kuepuka mpasuko ndani ya CUF ambao unaweza kupelekea uhasama usio na tija kwa taifa miongoni mwa makundi yanayoibuka katika mgogoro huu wa ndani ya CUF.

Tumeshaziona ishara,
Maggid Mjengwa.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com