Ndugu zangu,
Mada niliyoianzisha jana imezua mjadala mkubwa. Nimefutilia kila kilichoandikwa na wajumbe. Ningependa kufanya hapa majumuisho.
Kuna moja kubwa nililolibaini, kuwa wengi waliochangia hawakujihangaisha sana kutaka kuyajua ya jana kwa maana ya historia.
Wengi wamechangia bila kujibu hoja za msingi za Profesa Lipumba, ambazo kimsingi ni nzito na hazina majibu mepesi.
Binafsi
ningelipenda sana kuisoma michango ya Wanachama wa CUF, maana, hili la
Profesa ni mgogoro wa ndani ya CUF na unahusu Katiba ya chama hicho pia.
Nyongeza hapa ni ukweli kuwa kuna kinachoitwa ' Siasa za CUF'. Hizi
zina tofauti sana na za CCM, Chadema na wengineo. Kuzijua hizi ni lazima
urudi nyuma hadi kwenye matukio ya walau 1984 ili upate mwanga.
Naam, kwa
kuyafuatilia yanayoendelea ndani ya CUf, na kama viongozi wakuu wa CUf
wasipotanguliza busara, nauona mpasuko mkubwa wa CUf- Bara na CUF-
Visiwani.
Haiwezekani
leo ikawa rahisi kumweka kando Profesa Lipumba kama ilivyokuwa kwa
Mwenyekiti wa kwanza wa Chama hicho James Mapalala. Na hata ilivyokuwa
rahisi kwa Musobi Mageni kukaa pembeni na kumpisha Profesa Lipumba
kwenye uenyekiti.
Profesa
Lipumba ana uungwaji mkono na wafuasi wa kutosha kuimega CUF wakitokea
Bara. Ndani yake kuna wenye majina na wafuasi nyuma yao. Ni watu wa aina
ya Magdalena Sakaya, Nachuma na Kambaya. Miongoni mwao ni wabunge.
Kumekuwa
na manung'uniko ya CUF Bara kuwa CUF kama chama kinaendeshwa kwa msukumo
na mashinikizo ya upande wa pili kwa maana ya visiwani. Maalim Seif pia
anatupiwa lawama za moja kwa moja na wenye kumuunga mkono Profesa na
hususan walio bara.
Hakuna namna nyingine iliyo bora ya kuinusuru CUF isimeguke bila kufanyika jitihada za kufanyika juhudi za upatanisho hata kwenye kuutafuta mwisho wa mafahari wawili kukaa zizi moja.
Profesa
Lipumba, katika hali ya sasa, na kwa hoja alizoweka mezani, anaonekana
dhahiri yuko katika matayarisho ya juu kabisa ya mapambano ya kisiasa.
Ni jukumu
pia la Msajili wa vyama vya siasa ambaye pia ni mlezi wa vyama vya
siasa, kuandaa mazingira ya upatinishi kuepuka mpasuko ndani ya CUF
ambao unaweza kupelekea uhasama usio na tija kwa taifa miongoni mwa
makundi yanayoibuka katika mgogoro huu wa ndani ya CUF.
Tumeshaziona ishara,
Maggid Mjengwa.
No comments:
Post a Comment