Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu akiwasilisha mtazamo wa namna ambavyo anataka Wilayahiyo iwe
Wakuu wa Idara na vitengo, Maafisa Tarafa, Watendaji wa Kata, Vijiji, na Wenyeviti wa Vijiji wakifatilia mafunzo kutoka kwa wawasilishaji
Afisa utumishi wa Wilaya ya Ikungi Evodius Buberwa
akifafanua na kutofautisha majukumu ya watendaji wote ngazi ya Wilaya, Tarafa,
Kata na Vijiji
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu akisisitiza
umuhimu wa kuchangia maabara kwa ajili ya kuwanusuru wanafunzi wanaotaka kusoma
masomo ya sayansi lakini kikwaza inakuwa maabara
Kutoka Kushoto ni Mustafa Mtopo kaimu Afisa usalama wa Taifa
Wilaya ya Ikungi, Fortunatus Ndalama Mshauri wa Mgambo Wilaya ya Ikungi,
Dijovson Ntangeki Kaimu Katibu Tawala Wilaya ya Ikungi, Mkuu wa Wilaya ya
Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya
ikungi Rustika Turuka, na Mkuu wa poiisi Wilaya ya Ikungi Milton Nkyalu
wakifatilia mafunzo kutoka kwa wawasilishaji waliotoka ofisi ya Mkurugenzi
Mtendaji wa Wilaya hiyo
Mkurugenzi
Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya ikungi Rustika Turuka aliyesimama
akizungumza na Wakuu wa Idara na vitengo, Maafisa Tarafa, Watendaji wa Kata,
Vijiji, na Wenyeviti wa Vijiji wakati wa kikao hicho cha kazi
Afisa utumishi wa Wilaya ya Ikungi Ahmed Mussa akiwasilisha madawakati wa mafunzo hayo
Kaimu
katibu Tawala wa Wilaya ya Ikungi Dijovson Ntangeki akielezea ratiba ilivyo ya
mafunzo hayo
Na Mathias Canal,
Singida
Wakuu wa Idara na vitengo, Maafisa Tarafa, Watendaji
wa Kata, Watendaji wa vijiji na wenyeviti wa vijiji 101 vilivyopo Wilayani
Ikungi Mkoani Singida hii leo wamepatiwa mafunzo ya kutambua mipaka ya majukumu
yao kiutendaji katika kikao cha kazi kilichofanyika katika ukumbi wa shule ya
sekondari Ikungi.
Mafunzo hayo yameandaliwa na uongozi wa Halmashauri
ya Wilaya hiyo kutokana na kubainika kuwa asilimia kubwa ya watendaji hususani
wenyeviti wa vijiji na vitongoji wamekuwa wakiingilia katika majukumu ya
kiutendaji.
Akifungua mafunzo hayo yaliyodumu kwa zaidi ya masaa
matano yaliyojikita zaidi kutoa ufafanuzi juu ya majukumu ya watendaji wa Kata,
Wenyeviti wa Vijiji na Watendaji wa Vijiji, Mkuu wa Wilaya hiyo Miraji Jumanne Mtaturu amebainisha kuwa
pamoja na mafunzo kwa ajili ya ufahamu wa majukumu ya watendaji hao lakini amesema
kuwa Wilaya ya Ikungi ipo nyuma kielimu kutokana na shule kuwa mbali na maeneo
ya watu, wanafunzi wa kike kuachishwa shule na kuolewa, baadhi ya viongozi na
wataalamu kutotimiza wajibu wao na wakati mwingine uzembe wa baadhi ya
watumishi wa serikali katika kutatua kadhia za wananchi.
Pamoja na hayo pia DC Mtaturu amesema kuwa kuna baaadhi ya maeneo kuna shule ambazo
zina majengo mazuri na Hosteli kwa ajili ya wanafunzi lakini wazazi wanakataa
kuwapeleka wanafunzi shuleni ikiwa ni pamoja na shule ya Sekondari Mkinya
iliyopo Kata ya Dung’unyi, Shule ya Sekondari Mtunduru, Shule ya Sekondari
Mwaru na Wembere , huku shule ya Sekondari Issuna ikiwa na Majengo na Hosteli
nzuri lakini wanafunzi wanaosoma hapo ni wale wanaotoka Wilaya nyingine huku
wenyeji wakiwa wamejichimbia ndani.
Dc
Mtaturu amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya
Wilaya hiyo kwa kushirikiana na Polisi kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua baadhi
ya Watendaji wa Kata, Waratibu wa elimu wa Kata, Wenyeviti wa Vijiji na
Watendaji wa Vijiji wanaoshirikiana na baadhi ya wazazi kuwaachisha wanafunzi
shule ili wakaolewe ambapo amebaini kuwa katika Kata ya Mwaru na baadhi ya Kata
zinazozunguka katika Kata hiyo viongozi wake kwa kushirikiana na Waratibu elimu
Kata wamekuwa wakifanya biashara ya kuruhusu wanafunzi kuolewa kwa kupewa
Ng’ombe.
Hata hivyo pia amewaagiza Watendaji wa Kata ya
Makilawa na Iyumbu kumpatia taarifa ya kamati ya maendeleo ya Kata (WDC) ili
kubaini mpango wa mikakati katika kujenga shule za Sekondari katika Kata hizo
mbili ambazo zimesalia ilihali Kata 28 tayari zina shule za sekondari kati ya
Kata 30 zilizopo katika Wilaya hiyo.
Katika shule 28 ni shule 3 tu zenye maabara, shule
ya Sekondari ya Puma na Wembere ambao nao walijenga maabara baada ya kupata
msaada kutoka Benki ya dunia Mwaka 2013, shule ya Sekondari Mkinya ina maabara
2 ambazo zilijengwa kwa msaada wa SADC mwaka 2009 hivyo kupelekea Wilaya nzima
ya Ikungi kuwa na Maabara 4 pekee zilizojengwa kwa msaada wa wahisani ambapo
hakuna hata maabara moja iliyojengwa na wananchi ikakamilika kutokana na zuio
la kuchangia walilolipata wananchi kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Singida
Mashariki Tundu Lissu.
Sawia na hayo pia Mkuu huyo wa Wilaya amewaagiza
Watendaji wa Kata na Vijiji kwa kushirikiana na Wabunge, Madiwani na Wenyeviti
wa Vijiji kuwaelimisha wananchi kukaa vikao na kupitisha maadhimio ya kuendelea
kuchangisha michango ya ujenzi wa maabara kwa mujibu wa waraka wa Elimu namba 6
wa mwaka 2015 wa elimu msingi bila malipo.
Hata hivyo agizo limetolewa pia kwa Wazazi/Walezi
pamoja na wanafunzi wenyewe kuchukuliwa hatua kali za kisheria kutokana na
utoro wa wanafunzi shuleni jambo ambalo linapelekea kuwa na ufaulu duni wa
wanafunzi Wilayani humo.
Dc Mtaturu pia amemuagiza Afisa Mtendaji wa Katana
Afisa Mtendaji wa Tarafa kutumia siku 14 kuhakikisha madawati yanafika katika
shule zenye uhaba wa madawati ili kuondokana na adha ambayo inaendelea
kuwakumba wanafunzi shuleni ilihali madawati tayari yamepatikana.
Aidha ndani ya siku tano viongozi hao wameagizwa
kuhakikisha kuwa Masoko pamoja na stendi zinaenda katika maeneo yaliyopangiwa
ili ushuru upatikane kwa wakati na kwa kiasi kilichokusudiwa.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya
Ikungi Rustika Turuka amewashukuru
Watendaji wa Kata, Wenyeviti wa Vijiji na Watendaji wa Vijiji kwa kujitokeza
kwa wingi katika mafunzo hayo jambo ambalo limeonyesha kuwa wananchi hao wana
imani na serikali ya awamu ya nne hivyo amewaomba kuachana na siasa na kufanya
kazi kwa moyo na nguvu zaidi.
Amewataka viongozi wote wa ngazi ya Wilaya, Tarafa,
Kata, Vijiji na vitongoji kutekeleza maagizo yote yanayotolewa na serikali kwa
haraka na kwa ukamilifu.
Turuka
amesema kuwa kila kiongozi anapaswa Kutatua kero za wananchi kwa kutenda haki, kutofanya
kazi kwa mazoea, kutoa majawabu sahihi ya wananchi na kama hawafahamu wanapaswa
kuuliza sehemu husika ili kutozungumza jambo wasilokuwa na uhakika nalo.
Kupitia kikao hicho kilichoitishwa na mkuu huyo wa
Wilaya kilichokuwa na dhumuni la kufahamiana na kukumbushana majukumu na wajibu
wa viongozi na kueleza mtazamo wa Ikungi mpya inavyotakiwa kuwa Afisa utumishi
wa Wilaya sawia na Mkuu wa Polisi Wilaya wamepewa nafasi ya kuelezea majukumu
na wajibu wa kila mmoja katika maeneo yao.
Kwa upande wao baadhi ya Watendaji wa Kata, Vijiji na
wenyeviti wa vijiji 101 vilivyopo Wilayani humo wamesema kuwa mafunzo
waliyoyapata watayatumia vyema kuwa mabalozi wazuri kwa wananchi na
kuwaelimisha zaidi ili kutambua mipaka yao na majukumu yao katika kuishauri
serikali.
Aidha Maafisa Tarafa, Watendaji wa Kata, Watendaji
wa vijiji na wenyeviti wa vijiji wote ambao hawajahudhuria kikao hicho cha kazi
wametakiwa kuandika barua za maelezo kwanini wameshindwa kuhudhuria na
zimetakiwa kupitia kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Ikungi hadi kufikia
tarehe 10 ya mwezi huu wa nane.
0 comments:
Post a Comment