Raia wa
Afrika Kusini wanapiga kura katika chaguzi za serikali za mitaa ambazo
huenda zikawa pigo kwa chama cha ANC ambacho kimeiongoza nchi hiyo tangu
kumalizika kwa enzi ya ubaguzi wa rangi miaka 22 iliyopita.
Jana saa
moja asubuhi Wapiga kura walianza kupanga foleni katika vituo vya
kupigia kura kukiwa na hali ya baridi kali. Takriban wapiga kura milioni
26.3 wamesajiliwa kushiriki katika chaguzi hizo.
Kulingana
na kura za maoni, chama cha ANC kiko katika hatari ya kupoteza viti
katika miji muhimu nchini humo ukiwemo mji mkuu Pretoria, mji mkuu wa
kibiashara Johannesburg na mji wa pwani wa Port Elizabeth ujulikanao pia
kama Nelson Mandela Bay.
Maendeleo
nchini Afrika Kusini yamekuwa sio ya kasi iliyotarajiwa tangu Hayati
Nelson Mandela aliposhinda katika uchaguzi wa kihistoria mwaka 1994
ambapo enzi ya ubaguzi rangi ilikoma nchini humo. Bado raia wengi weusi
hawana maakazi mazuri, elimu bora na nafasi za ajira.
Je ANC kitastahimili kishindo?
Benki kuu
nchini humo imesema uchumi utatuwama kwa asilimia sufuri mwaka huu na
vyama vya upinzani Democratic Alliance na Economic Freedom Fighters EFF
kinachoongozwa na Julius Malema vimeishutumu serikali ya Rais Jacob Zuma
kwa kuurejesha nyuma uchumi wa taifa hilo imara zaidi kiuchumi barani
Afrika. Upinzani umeahidi kuuboresha uchumi iwapo utashinda katika
chaguzi hizo.
Kiongozi
wa kwanza mweusi wa chama cha DA Mmusi Maimane amesema Afrika Kuisni iko
katika nafasi ya kujipatia kitu cha kipekee na cha kihistoria katika
chaguzi hizo akikitaja chama tawala cha ANC kuwa fisadi, badhirifu na
kuondoka kutoka ndoto waliyokuwa nayo waafrika Kusini ya demokrasia.
Rais Zuma
ana uungwaji mkono mkubwa nchini humo hasa katika maeneo ya vijijini na
ANC kimekita mizizi miongoni mwa raia wa nchi hiyo na kina fedha za
kuwashawishi wapiga kura ili kiendelee kuwa na wingi wa viti 278 vya
mameya na madiwani.
Uchaguzi kipimo cha umaarufu wa Zuma
Lakini
umaarufu wa Zuma umeingia dowa kutokana na kashfa chungu nzima za
ufisadi, kesi mahakamani, kuzorota kwa uchumi wakati wa uongozi wake na
viwango vya wasio na kazi vikiwa asilimia 27. Kati ya watu wanne nchini
humo, mmoja hana kazi.
Mlungiseleli
Kwanini mwenye umri wa miaka 60 ambaye anafanya vibarua katika mji wa
Port Elizabeth amesema ANC kimeshindwa vibaya katika kuteleza ahadi zake
ilizotoa kilipoingia madarakani 1994 na kinachoshuhudiwa ni ukosefu wa
ajira, viwango vya juu vya uhalifu na ufisadi na ukosefu wa huduma
muhimu kama maji na umeme.
Matokeo
ya chaguzi hizo zinazotajwa kuwa kipimo cha umaarufu wa Rais Zuma
yanatarajiwa siku ya Alhamisi na huenda yakaongeza shinikizo kwa
kiongozi huyo kujiuzulu kabla ya muhula wake kukamilika mwaka 2019.
Zuma hata
hivyo amesema ana imani watashinda viti vingi. Mchambuzi wa masuala ya
kisiasa Afrika Kusini Judith February amesema iwapo ANC kitashindwa
katika mabaraza muhimu, yaliyo na watu weusi wengi kama Johannesburg na
Nelson Mandela Bay, itamaanisha hali ngumu kwa Rais Zuma.
Hata hivyo
February ameongeza kuwa ANC huenda kikawashangaza wengi matokeo
yatakapotangazwa.DW
0 comments:
Post a Comment