SERIKALI ya Awamu ya Tano imeanza utekelezaji wa bajeti yake ya kwanza ya Sh trilioni 29.5 ambayo kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, asilimia 40 ni fedha zilizotengwa kwa ajili ya maendeleo.
Huko nyuma kiasi kilichokuwa kinatengwa kwa ajili hiyo kilikuwa chini ya asilimia 30. Katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka huu, serikali imepanga kukusanya Sh trilioni 18.46 ambazo ni sawa na asilimia 62.5 ya bajeti yote zitatokana na mapato ya ndani yanayohusisha halmashauri.
Katika hizo Sh trilioni 18.46, serikali imepanga kukusanya mapato ya kodi ya jumla ya Sh trilioni 15.105 ambayo ni asilimia 82 ya mapato ya ndani. Ili kutekeleza bajeti hiyo, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewekewa lengo la kukusanya Sh trilioni 15.1 katika mwaka wa 2015/16. TRA ilivunja rekodi ya kukusanya mapato kwa asilimia 104 ya kiwango kilichowekwa cha makusanyo ya Sh trilioni 13.2.
HabariLeo imefanya mahojiano na Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo kujua mikakati ya ukusanyaji kodi katika kuisaidia utekelezaji wa bajeti ya serikali.
Swali: TRA imejipangaje kuhakikisha inakusanya kiwango ilichopangiwa?
Majibu: TRA imepewa lengo la kukusanya Sh trilioni 15.1 mwaka huu wa fedha. Hili ni lengo kubwa, na kama mnavyofahamu serikali imeongeza bajeti ya maendeleo hadi kufika asilimia 40 kwa nia ya kuleta maendeleo ya nchi.
Kwanza kabisa tumeshakaa sisi (TRA), idara kwa idara na kupanga mkakati wa kiidara, kiwilaya na kimkoa. Katika mikakati hiyo tunalenga kuhakikisha kila kodi inayostahili kukusanywa inakusanywa kikamilifu na hakuna uvujaji wa mapato. Katika kutimiza azma hiyo tumejipanga kufanywa kazi kwa pamoja na viongozi wa juu wa serikali katika ngazi ya wizara mbalimba, mikoa na wilaya.
Tungependa kushukuru viongozi wa juu wa serikali kutupa hamasa na msukumo katika azma hii, maana rais na waziri mkuu wamekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza azma hii. Hata katika ngazi ya mikoa suala la ukusanyaji mapato ni sehemu ya ajenda. Maneneja wa mikoa wanatakiwa kukutana na viongozi wa mikoa na wilaya kusaidiana katika kukusanya mapato na kukabiliana na changamoto zinazofanya mapato yasikusanywe.
TRA tumejipanga kuhakikisha wafanyabiashara wote ambao hawajasajili, kampuni. Kuboresha huduma za ulipaji wa kodi na kuwezesha gharama za ulipaji wa kodi uwe wa nafuu. Kama kweli yupo mtu anafanya biashara anatakiwa aonekane kama hayupo na kama hayupo tutafuta hizo TIN na tubakize TIN zilizohai.
Katika kutekeleza hilo tumeanza na Dar es Salaam ambapo tumetenga maeneo maalumu ambayo kwa Wilaya ya Kinondoni ni jengo la LAPF-Kijitonyama na Kibo Complex, Tegeta, Ilala ni Shaurimoyo na jengo liitwalo 14 Rays lililoko Gerezani na katika wilaya ya Temeke ni Uwanja wa Taifa.
Swali: Kuna watu ambao wanashindwa kulipa kodi kutokana na kutokuwapo mazingira rafiki, hili mtalifanyaje?
Majibu: TRA inatambua hilo na wakati mwingine ugumu huo unachangiwa na kuzifikia ofisi za TRA. Tumetambua hili kwani wakati mwingine wanashindwa kulipa kodi kutokana na ugumu wa kufikia kwa ofisi zetu na msongamano hasa nyakati za kulipa kodi za makadiliko. Sasa tanatafuta ofisi sehemu mbalimbali mwafaka ili kuwawezesha wafanyabiashara kulipa kodi kwa wakati bila usimbufu wa msongamano.
Tumejipanga kuhakikisha tunaimarisha mifumo ya kulipia kodi. Mifumo ikiimarishwa wafanyabiashara wataweza kulipa kodi kwa njia mbalimbali za mitandao, benki, simu ya kigajani, mawakala; mfano MaxMalipo, bila kulazimika kuja ofisi za TRA wakiwa na fedha. Hatua hii itampunguzia muda mfanyabiashara wakati wa kulipa kodi na kukaa kwenye foleni.
Tumeweka kituo cha huduma kwa wateja ambacho kitamsaidia mfanyabiashara kuuliza swali au kupata ufafanuzi wa jambo lolote na kuelimishwa. Namba za kupiga ni 0800780078 au 0800750075 au barua pepe ya huduma@tra. go.tz. Huduma hii ni kuanzia saa mbili asubuhi mpaka saa 11 jioni na mteja atajibiwa kwa wakati.
Swali: Je, upande wa uingizaji bidhaa kutoka nje, utasaidiaje ukusanyaji wa kodi?
Majibu: Katika kitengo hiki TRA ina mfumo wa forodha wa Tascis ambao umemrahisishia mfanyabiashara kuweza kuleta mzigo wake na ukashughulikiwa kwa haraka kadiri inavyowezekana. Na kwa bahati nzuri mfumo huu tumekuwa tukiuboresha siku hadi siku kwa kuunganisha na taasisi mbalimbali zinazohusika katika kushughulikia mizigo ili kupunguza muda unaotumika kutafuta vibali mbalimbali, mfano kutoka TBS (Shirika la Viwango Tanzania) na TFDA (Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania).
Pia inamwezesha mfanyabiashara kuanza kushughulikia mzigo wake mapema hata kabla ya mzigo kufika na zinabaki zile taratibu ambazo zinatakiwa kufanywa mzigo unapokuwa umefika. Sambamba na hilo tumepunguza sana wizi au udanganyifu upande wa mzigo ya Transit ambayo kwa namna moja au nyingine kulikuwa na udanganyifu fulani kwa baadhi ya wafanyabiashara kudai mzigo unakwenda nchi fulani kumbe inatumika ndani ya nchi hii, hivyo kuikosesha serikali mapato.
Udanganyifu huu tumeupunguza kupitia uwepo lakiri ya kielektroniki katika magari na mizigo inayokwenda nje ya nchi kutoka Bandari ya Dar es Salaam ili kuhakikisha mizigo hiyo inafuatiliwa kwa njia ya mtandao tangu inapotoka bandarini hadi inapofika mpakani. Hili limesaidia kufuatilia mzigo ukiwa njiani na muda wa gari inaotumia ikiwa njiani, jambo ambalo limesaidia kudhibiti baadhi ya mizigo hiyo kuuzwa ndani ya nchi na kuinyima serikali mapato.
Kwa mizigo inayokwenda nchi za Afrika Mashariki kama Rwanda na pia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, mizigo hiyo inalipiwa kodi katika nchi husika kabla mizigo haijaondoka bandari ya Dar es Salaam. Na tumelidhibiti hili ili kuhakikisha mianya inazibwa na kuondoka kabisa.
Hatua nyingine tutakayoifanya ni kuweka usimamizi na kuziba mianya ambayo imekuwa ikitumika kuingiza mizigo ya magendo, Hili tunalifanya kwa kuimarisha kitengo chetu cha kupambana na biashara za magendo kwa kukiwezesha kwa kukipa vitendea kazi kama magari ambayo yatafanya doria maeneo mbalimbali ambayo mianya hii ipo. Mfano ukanda wa pwani kutoka Mtwara hadi Tanga na maeneo ya mipaka.
Na pia tunawatumia wananchi kutupa taarifa ambazo zinaweza kutusaidia kufuatilia mienendo ya watu hao wanaofanya udanganyifu. Sambamba na hilo pia tunatumia vyombo vya dola kufanya doria nchi kavu na pia kuimarisha mipaka yote kwa kushirikiana na nchi jirani tuizopakana nazo.
Swali: Je, kwa upande wa utoaji risiti mikakati ikoje?
Majibu: Katika hili TRA imeweka mkazo katika utoaji risiti kwa kuongeza kasi ya ugawaji na uuzaji wa mashine za kielektroniki (EFD) kwa wafanyabiashara ambao hawana sambamba na kutoa elimu kwa wafanyabiashara. Ili kuhakikisha kuwa changamoto zilizopo katika mashine hizo zinatatuliwa mara moja, tumewalazimisha mawakala wote kufungua ofisi eneo la Kariakoo kwa sababu pale pana wafanyabiashara wengi ili kupunguza muda unaotumika kutengeneza mashine zinapokuwa na tatizo, na kuwapa muda wa kuwaelimisha wafanyabiashara.
Katika hili pia tumewalazimisha kuwa na ofisi katika mikoa mbalimbali na pia kunakuwa na mikataba kati ya wakala na wasambazaji. Tumeweka mkazo upande wa wateja wanaonunua bidhaa kwa kuwataka wadai risiti na kuhakiki taarifa za risisti hizo kama ni sahihi na gharama iliyoandikwa ni ile iliyotolewa. Bahati nzuri, serikali imelitungia sheria ya fedha ya mwaka 2016 kwa kuweka adhabu kwa mteja ambaye hatodai risiti ya EFDs ambapo anaweza kupewa faini ya kati ya Sh 30,000 hadi Shmilioni 1.5 kulingana na thamani ya bidhaa.
Hii litafanya kila mwananchi kuwa na mwako wa kudai risiti. Kwa muda mrefu kumekuwa na msukumo kwa upande wa wauzaji lakini hakukuwa na msukumo wa kipekee kwa wanunuaji hasa ukizingatia haikuwa desturi yetu kudai risiti tunapofanya manunuzi ya bidhaa, baadhi tu ndio walikuwa wakifanya hivyo. Kwa waliokuwa na utamaduni wa kudai risiti, wapo ambao wamekuwa hawako makini kukagua risiti walizopewa kwa kuangalia kama taarifa ni sahihi.
Zaidi ya utekelezaji wa sheria, tunataka mwananchi aangalie taarifa za kwenye risiti ni sahihi. Mfano; kuangalia kama risiti ni ya TRA, nembo na TIN, kiwango sahihi cha pesa alizolipa na tarehe ni ya siku husika, kwani kiwango kikiwa si sahihi kitapunguza kiwango cha kodi ambacho kilikuwa kiingie serikalini. Napenda kuchukua fursa hii kuwakumbusha wananchi ifikapo Septemba 1 mwaka huu wawe wakijua kwamba vituo vyote vya mafuta vitafungwa mashine za EFD.
Pia wananchi wajue kwamba tumebadilisha tarehe ya kuwasilisha marejesho ya VAT kutoka tarehe 27 hadi 20 ya mwezi unaofuata ili kusaidia TRA kukusanya mapato kwa wakati husika.
Swali: Je, mtatekelezaje agizo la Waziri Mkuu la kudhibiti wafanyakazi wa TRA wasio waaminifu na kuboresha tathimini ya kodi ili kuwatendea haki wananchi?
Majibu: Kwa upande wa watumishi tumejikita kuwawajibisha wale watakaoshindwa kufanya kazi kwa maadili na weledi na tunasisitiza tathimini ya kodi isiwe ya kumkomoa mtu ili kutengeneza mwanya wa mazungumzo yanayopelekea rushwa. Katika kujenga nidhamu ya uwajibikaji, tumeweka mifumo ya kuhakikisha kazi hizi zinafanyika kwa uadilifu na uangalifu mzuri, kuheshimu walipa kodi na kuwatendea haki pale wanapokuwa na hukumu bila kumuonea mtu.
Uongozi wa TRA unalitekeleza hili kwa vitendo, na lina kwenda sambamba na kuwajengea uwezo wafanyakazi kwa upande wa kiutawala na kwa vitendo katika ukusanyaji mapato. Niwasihi wananchi kutumia haki yao ya msingi ya kukataa makadirio kama wanaona hayako sawa sawa na hayaendani na mapato yao ili waweze kukadiriwa kile wanachotakiwa kukadiriwa.
Wanaweza kukata rufaa kwa Kamishna wa Kodi husika au Kamishna Mkuu wa TRA na Baraza la Rufaa la Kodi na akasikilizwa na kupata haki zao. Uongozi wa TRA unatekeleza hili kwa vitendo ili kuhakikisha hakuna mfanyabiashara anayeonewa maana nia yetu ni kuhakikisha mfanyabiashara analipa kodi sahihi na kwa wakati.
Swali: Je, mnao watumishi wa kutosha kutekeleza majukumu yenu pamoja na suala zima la elimu kwa mlipa kodi?
Majibu:Tumeongeza watumishi 150. Pia tunatarajia kuajiri wengine wapatao 300 ambao wako mafunzoni ili kuziba pengo la wafanyakazi waliostaafu au kuachishwa kazi. TRA inatumia kila fursa iliyopo katika kuelimisha wananchi umuhimu wa kushiriki katika kulipa kodi, sambamba na kuwajengea uelewa wanafunzi katika ngazi za sekondari na vyuo kwa kuanzisha klabu za kodi.
Mwanafunzi ndio mlipakodi, mwajiri au mwajiriwa mtarajiwa, hivyo tumeanzisha klabu za kodi katika vyuo vya IFM na Chuo cha Kodi na tutaendelea na hili katika vyuo vingine pale mwaka mpya wa masomo utakapoanza.
Swali: Una mwito gani kwa jamii au serikali?
Majibu: Natoa mwito kwa jamii kuwa Serikali inapoongeza usimamizi wa kodi wasijisikie vibaya na kuona wanaonewa bali wanatakiwa kujua hii ni njia ambayo Serikali inawatumia wananchi wake katika kuleta maendeleo.
0 comments:
Post a Comment