Rais wa
Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo Joseph Kabila ahudhuria sherehe ya
kutia saini mpango wa amani, usalama na ushirikiano wa Congo na mataifa
yenye maziwa makuu jijini Addis Ababa.
Marekani
imeonya kutokea kwa ghasia zaidi katika jamhuri ya kidemokrasia ya Congo
iwapo rais Joseph Kabila atasalia katika uongozi baada ya kukamilika
kwa hatamu yake mnamo mwezi Desemba.
Jamhuri
ya kidemokrasia ya Congo imesema kuwa ghasia zitaendelea kushuhudiwa
nchini humo iwapo mataifa ya kigeni yataendelea kuingilia kati masuala
ya ndani ya nchi hiyo. Kwa muda wa miezi kadhaa sasa Marekani imekuwa
ikifuatilia kwa karibu hali katika Jamhuri hiyo ya Kidemokrasia ya Congo
ambapo taharuki inazidi kutanda kabla ya makataa ya tarehe 20 Desemba
ya kukamilika kwa kipindi cha pili cha kuhudumu kwa rais wa nchi hiyo
Joseph Kabila.
Mnamo
mwezi Mei, mahakama ya kikatiba iliamua kuwa Kabila aliyechukuwa uongozi
baada ya babake kuuawa mnamo mwaka 2001 kabla ya kuchaguliwa mwaka 2006
na 2011, anaweza kukaimu wadhifa huo iwapo uchaguzi hautaandaliwa
kufikia tarehe 19 mwezi Septemba kulingana na katiba inayohitaji kura
kuandaliwa siku 90 kabla ya kukamilika kwa kipindi cha kuhudumu kwa
rais.
Hali nchini Congo
Lakini
kulingana na Anthony Gambino aliyekuwa mkuu wa taasisi ya Marekani ya
maendeleo ya kimataifa, hali nchini Congo tayari imesambaratika.
Aliongeza kuwa kufikia leo imesalia muda wa mwezi mmoja kwa nchi hiyo
kuwa na mzozo kamili wa kikatiba .
Rais wa
Marekani Barrack Obama pia ameshinikiza kuweko kwa ubadilishanaji
mamlaka kwa njia ya kidemokrasia barani Afrika . Mnamo mwaka 2015 katika
makao makuu ya Umoja wa Afrika jijini Addis Ababa alisema,´´Maendeleo
ya kidemokrasia nchini Afrika pia yamo hatarini iwapo viongozi watakaa
kungatuka mamlakani baada ya kukamilika kwa hatamu zao za uongozi ´´.
Ghasia za hivi punde
Haya yote
yanajiri baada ya watu watatu ikiwa ni pamoja na afisa mmoja wa polisi
kuuawa hapo jana kwenya makabiliano katika mji mmoja Mashariki mwa
Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo baada ya ghasia zilizotokana na madai
ya kushindwa kwa serikali hiyo kushughulikia maswala ya usalama .
Mamia ya
watu pia waliandamana katika barabara za Beni baada ya kukamilika kwa
siku tatu za maombolezo zilizoitishwa na makundi ya kijamii kuhusiana na
mauaji ya mamia ya watu siku ya Jumamosi usiku. Mauaji hayo yalitokea
siku tatu tu baada ya rais Kabila kuzuru eneo hilo na kuahidi kufanya
kila awezalo kuhakikisha kudumishwa kwa amani na usalama katika eneo
hilo.
DW
0 comments:
Post a Comment