Madereva kikaangoni
SERIKALI imeanza rasmi kutumia mfumo wa nukta katika leseni za udereva kwa kudhibiti madereva wazembe, wanaosababisha ajali za barabarani.
Mfumo wa nukta ni mfumo ambao utatumika kupunguza nukta katika leseni za madereva, ambao watakutwa na makosa mbalimbali ikiwemo ulevi na uzembe, hatua ambayo baadaye itamfanya dereva kunyang’anywa leseni yake.
Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam jana na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusufu Masauni wakati wa uzinduzi wa Mkakati wa Kukabiliana na Ajali za Barabarani nchini.
Alisema mfumo huo, utakuwa na nukta 15 na dereva atakayebainika kutenda kosa la usalama barabarani, atapunguziwa nukta 10 kati ya 15 za leseni yake.
Alisema mkakati huo uliozinduliwa jana, ambao utadumu kwa kipindi cha miezi sita, umelenga kudhibiti makosa yanayosababisha madhara makubwa, likiwemo ongezeko la ajali za barabarani zinazowasababishia watu wasio na hatia vifo na ulemavu.
Aliongeza kuwa mambo yaliyolengwa katika mkakati huo ni pamoja na kudhibiti madereva walevi na ambao wanaendesha kwa uzembe.
Alisema dereva ambaye atakamatwa kwa sasa akiendesha kwa uzembe au ulevi, atapelekwa mahabusu kwa saa 24, ndipo atapelekwa mahakamani kwani wamegundua wapo madereva wanaoendesha kwa uzembe, wakiamini kuwa wakikamatwa watatozwa faini ambazo wanaweza kuzimudu.
Pia alisema mkakati huo, unalenga kudhibiti mwendo kasi kwa madereva na wamiliki wa magari na kuhakikisha kunakuwepo na madereva wawili kwa safari za masafa marefu.
“Hatuwezi kuendelea kuona ajali za barabarani zikiongezeka na kupoteza maisha ya watu ambao wengi ni tegemezi matokeo yake watoto wanabaki yatima, naamini dereva akibaki na nukta tano sijui atafanya nini na leseni yake,” alisema Masauni.
Masauni aliongeza kuwa mkakati huo, pia utawalenga madereva ambao hawana sifa pamoja na wale waliochukua leseni kwa njia ambazo si sahihi, lengo likiwa ni kuwabaini madereva ambao hawana viwango, ambao kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakichangia ajali za barabarani.
Aidha alisema mkakati huo, pia utalenga kudhibiti ajali za pikipiki na bajaji, ikiwemo kutoa elimu katika vituo vya pikipiki na bajaji, lengo likiwa ni madereva wa vyombo hivyo kupata elimu itakayowaepusha na madhara ya ajali ambazo nyingi zimekuwa ni mbaya.
“Niseme tu baada ya elimu hii kutolewa dereva atakayevunja sheria ikiwemo kutovaa kofia ngumu, kutoheshimu taa nyekundu pamoja na kupakia abiria mishikaki atachukuliwa hatua kali ikiwemo kupelekwa mahabusu na baadaye mahakamani,” alisema Masauni.
Alisema mkakati huo, pia utawalenga abiria ambapo kila abiria atatakiwa kufunga mkanda wa usalama, anapotumia vyombo vya usafiri na kwamba wanaandaa mchakato wa kubadilisha sheria, ambayo itawataka abiria kufunga mikanda na ambaye atakiuka atachukuliwa hatua kali.
Aliongeza kuwa mkakati huo pia utadhibiti rushwa na kuwaadhibu watoaji na wapokeaji rushwa katika barabara zote nchini.
“Najua wapo askari wa Usalama Barabarani wanaopokea rushwa na wengine hata wanatoa rushwa lakini niseme sasa tutaweka mitego ili kuwakamata watoaji na wapokeaji.
“Pia tutaandaa motisha kwa ajili ya askari wetu watakaofanya vizuri ili kuleta morali kwa wale ambao hawafanyi kazi zao kwa weledi,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Meneja Usalama Barabarani na Mazingira wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), Geofrey Silanda, akizungumzia suala la kutumia siku mbili kwa safari za masafa marefu, alisema mamlaka hiyo imejipanga na tayari wameboresha ratiba ambayo inatarajiwa kuanza kufanya kazi muda wowote.
Takwimu za ajali za barabarani Akiwasilisha taarifa ya Serikali bungeni hivi karibuni, Masauni alisema Jiji la Dar es Salaam linaongoza kwa kuwa na ajali nyingi za barabarani kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2013 hadi 2015, zilizosababisha vifo vya watu pamoja na majeruhi. Kwa mujibu wa Masauni, Jiji la Dar es Salaam limeongoza kwa kuwa na ajali 18,506 kati ya ajali 46,539 zilizotokea nchi nzima kwa kipindi hicho.
“Takwimu za nchi nzima zinaonesha kuwa mwaka 2013 zilitokea ajali 23,842 zilizosababisha vifo 4,002 na majeruhi 20,689. Mwaka 2014 zilitokea ajali 14,360 zilizosababisha vifo 3,760 na majeruhi 14,530 na mwaka 2015 zilitokea ajali 8,337 zilizosababisha vifo 3,468 na majeruhi 9,383,” alisema Masauni.
Masauni alieleza kuwa kwa mwaka 2013, Mkoa wa Kipolisi Kinondoni uliongoza kwa kuwa na ajali zipatazo 6,589 ukifuatiwa na Mkoa wa Kipolisi Ilala uliokuwa na ajali 3,464 wakati mikoa ya Simiyu na Tanga ilikuwa na ajali chache, ambapo Simiyu zilitokea ajali 67 na Tanga ajali 96.
Mwaka 2014 Kinondoni na Ilala ziliongoza tena, ambapo ajali 3,086 zilitokea Kinondoni na Ilala ajali 2,516. Mikoa iliyokuwa na ajali chache ni Simiyu ajali 55 na Kagera ajali 29.
Alisema kuwa mwaka 2015 Mkoa wa Kipolisi Ilala, uliongoza kwa kuwa na ajali nyingi za barabarani, ambapo ajali 2,516 zilitokea mkoani humo, ukifuatiwa na Temeke uliokuwa na ajali 1,420 wakati mikoa ya Rukwa na Arusha ilikuwa na ajali chache.
Alibainisha kuwa mfumo endelevu wa wazi uliopo wa kutoa takwimu hizo ni kupitia taarifa za mwaka za Jeshi la Polisi (Polisi Annual Report), ambapo kila Mtanzania anaweza kupata taarifa hizo za ajali.
0 comments:
Post a Comment