METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, August 23, 2016

AGRA inavyoimarisha kilimo kama msingi wa maendeleo ya uchumi


IBARA ya 78 ya Mwongozo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa mwaka 1981 inaweka bayana nafasi ya kilimo kwa maendeleo ya uchumi na kijamii ya taifa la Tanzania.
Mwongozo huo ulisema: “Msingi wa uchumi wa nchi yetu ni kilimo.” Asilimia zaidi ya sabini ya Watanzania wanaishi kwa kutegemea kilimo, biashara yetu na nchi za kigeni inategemea zaidi mazao tunayozalisha katika kilimo; viwanda vichache tulivyonavyo nchini vinategemea mazao ya kilimo; uwezekano wa kuzalisha ziada itakayowezesha nchi kugharamia mapinduzi ya viwanda (kugharamia kuanzishwa kwa viwanda mama na viwanda vya madawa) upo katika sekta ya kilimo.
Mwongozo huo umetumika katika Programu ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 1987 hadi mwaka 2002 iliyotengenezwa kwa malengo ya kujenga misingi imara ya uchumi wa kijamaa wa taifa linalojitegemea, kabla ya kuingia kwa vyama vingi mwaka 1992 ambapo ulibakisha nakshi tu katika juhudi nzima za kujenga taifa linalojitegemea. Kutokana na mwongozo huo, chama tawala kilielekeza kubadili kilimo kilichokuwa cha kinyonge cha kutegemea mvua na kuingia katika kilimo cha umwagiliaji na matumizi ya teknolojia na kanuni za kilimo chenye tija.
Miaka 25 baada ya maamuzi hayo, Taasisi ya Mapinduzi ya Kijani Barani Afrika (AGRA), iliingia Tanzania kutoa msaada kwa wakulima wadogo ili waweze kutumia teknolojia katika kilimo chao na hivyo kuwawezesha wakulima wadogo kuwa na uhakika na usalama wa chakula huku wakiingiza ziada katika soko. Taasisi hiyo ilianza kazi nchini kwa kutambua umuhimu wake mwaka 2006 na tangu mwaka huo imekuwa ikifanya shughuli moja hadi nyingine, ikiwa na lengo la kubadili kilimo cha wakulima wadogo nchini Tanzania ambao ni tegemeo kwa taifa.
Mtendaji wa taasisi hiyo nchini, Dk Mary Mgonja anasema msaada wanaoutoa umelenga kuweka hai matumaini makubwa ya kilimo ya kujenga msingi wa uchumi imara wa Tanzania kwa kuongeza matumizi zaidi ya teknolojia kama njia pekee ya kuwainua mamilioni ya wakulima wadogo kutoka katika lindi la umaskini.
“Tanzania kuanzia mwaka 2006 imekuwa ikipewa kipaumbele na AGRA na tayari miradi 96 imepewa ruzuku inayofikia dola za Marekani milioni 51,” anasema katika mahojiano na kuongeza kwamba ruzuku hiyo ililenga kutoa mchango kwa serikali katika kukabiliana na changamoto za wakulima wadogo katika mnyororo wa thamani wa shughuli zao kuanzia masuala ya mbegu, udongo, soko, sera hadi fedha.
Ukiangalia mchango huo na mabadiliko yanayoonekana sasa hasa katika upatikanaji wa mbegu bora na sera ya mbegu nchini Tanzania, juhudi za AGRA zimekuwa chachu katika kufanikisha mabadiliko kwa wale waliotumika kufanya maonesho na sasa wengine wanaweza kuwaiga na kuendeleza kilimo. Matunda hayo katika uendelezaji wa teknolojia yanaonekana katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na upatikanaji wa mbegu zinazofaa katika mazingira ya sasa.
Aidha ushawishi pia unaendelea wa wananchi kutumia mbegu hizo mpya ambazo zinachuana na mabadiliko ya tabianchi. AGRA kupitia ruzuku zake imewezesha kupatikana kwa aina tofauti za mbegu zilizoboreshwa ili kukabiliana na hali za maeneo; matumizi sahihi ya mbolea; utunzaji baada ya mavuno; teknolojia ya hifadhi za nafaka na ubunifu wa upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kuinua kilimo.
Moja ya sifa kubwa ya AGRA katika kusaidia mabadiliko katika kilimo cha Tanzania ni ruzuku yake na ufuatiliaji katika kuhakikisha kwamba kunakuwa na mazingira mazuri ya biashara ya mbegu kupitia mradi wa Micro Reforms for African Agribusiness (MIRA). Mradi huu ulizaa matunda mema kwani kuanzia Juni 2016, kumekuwepo na sera mpya ya mbegu. Mbegu ni moja ya tatizo kubwa kwa wakulima.
Wakulima hawa walizoea mbegu za asili ambazo zinatoa mazao haba, hivyo wamekuwa wakihitaji kubadilishwa fikira na kuletewa mbegu mpya zitakazoshindana na mazingira ya sasa na pia kutoa tija kubwa. Mkurugenzi Mtendaji Tanzania Seeds Trade Association (Tasta), Baldwin Shuma, anaeleza kufurahishwa na sera hiyo inayoruhusu sasa makampuni ya mbegu kuzalisha mbegu ambazo zilifanyiwa utafiti na taasisi za umma.
Awali kukosekana kwa sera hiyo kulifanya iwe vigumu kwa makampuni ya mbegu kuzalisha mbegu hizo kwa wingi baada ya kukamilishwa kwa utafiti ambao umekuwa ukifanywa na taasisi za umma. Hapakuwepo na miongozo, sheria wala kanuni kwa kuzingatia sera iliyopo, hivyo kuwepo kwa sera baada ya juhudi kubwa ya AGRA kumesaidia kuwepo kwa uhakika wa mbegu nyingi kuzalishwa na kumfikia mkulima na hivyo kuondoa tatizo la mbegu bora.
Dk Matilda Kalumuna wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo ya Mlingano –Tanga, akizungumzia manufaa ya ruzuku za AGRA kubadili kilimo cha Tanzania, anasema taasisi yake imefaidika kwa kuweza kuimarisha mifumo yake ya kuangalia ubora wa mbolea. Taasisi hiyo ilipata ruzuku ya dola za Marekani 400,000 kusaidia kuimarisha mifumo yake ya kuangalia ubora wa mbolea kwa kutoa mafunzo na vifaa.
“Kupitia mradi huu taasisi ilifundisha wakaguzi wa mbolea 100; wachambuzi 15 wauzaji pembejeo wenye uelewa 338 na wadau 8000,” anasema Dk kalumuna. Anasema kutokana na mradi huo makampuni mbalimbali na wauzaji wa pembejeo za kilimo waliamua kwa hiari yao kujisajili kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Ubora wa Mbolea Tanzania (TFRA) iliyo chini ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Ni kwa mantiki hiyo sasa mbolea iliyoko sokoni inasajiliwa, kukaguliwa na kuchambuliwa kwa lengo la kuona mbolea zisizokidhi viwango zinajulikana na kuondolewa sokoni. Mbolea hafifu na wakati mwingine feki ilikuwa inaingia kwa wakulima na kuwapoteza lengo lao wakidhani wamepata mbolea kumbe wajanja walikuwa wakiwabambikia. Tatizo hili kwa sasa limepunguzwa kutokana na kuwapo na mfumo wa ukaguzi na wakaguzi unaofanywa na TFRA.
Kuwepo kwa wakaguzi hao kunasaidia kutekeleza sheria ya mbolea na hivyo wakulima sasa wanapata kile wanachohitaji bila udanganyifu na wakidanganywa inakuwa rahisi kwao kubaini kwa kuwaita wataalamu hao ambao hukagua mbolea hiyo. Kupatikana kwa mbegu na mbolea sahihi kumechangia kuongezeka kwa mazao ya mkakati kama mahindi katika kanda ya nyanda za juu.
Na kiukweli hifadhi ilianza kuwa tatizo kiasi cha AGRA kulazimika kutoa ruzuku nyingine tena ili kuwezesha wakulima kujua namna ya kuhifadhi mazao yao kwa kutumia mifuko maalumu na vihenge na wale wenye uwezo mkubwa kununua vifukofuko. Pamoja na wakulima kuwa na hamu ya kupata teknolojia hiyo mpya ambayo imeboreshwa kwani hata zamani walikuwa na vihenge, hawakuwa na fedha za kunulia teknolojia hiyo na hivyo AGRA ikaingia katika juhudi nyingine kwa kuzungumza na mabenki mbalimbali na kufikia mapatano na Benki ya Equity.
Akizungumza katika maonesho ya Nanenane yaliyoisha hivi karibuni katika viwanja vya John Mwakangale, Mbeya, Mkuu wa biashara ya kilimo wa Benki ya Equity, Enesto Josephat alisema kwamba kwa sasa wamekubaliana na AGRA kuendesha mradi huo wa majaribio katika mikoa mitatu ya Njombe, Morogoro na Iringa. “Benki ya Equity Tanzania imeingia ubia na AGRA kuanzisha mfuko ambao utasaidia kununuliwa kwa vifaa vya hifadhi ya nafaka.
Katika mradi wa majaribio Njombe, Morogoro na Iringa, tutatoa mikopo ya kuanzia Sh milioni 5 hadi 30 ili kununua mifuko maalumu ya kuhifadhia nafaka; vihenge vya chuma na vifukofuko (cocoons), kuanzia mwezi huu,“ anasema. Ni dhahiri mifuko maalumu ni rahisi lakini vihenge vya chuma na vifukofuko vinahitaji zaidi fedha na mazao yanayowekwa kiushirika kwani inaweza kukaa hadi miaka mitano hivyo teknolojia hii itasaidia sana usalama wa chakula katika maeneo ya vijijini.
Kuhusu umuhimu wa ruzuku ya AGRA katika upande wa utafiti, Mtaalamu wa viazi mviringo, Owekisha Kwigizile, kutoka kituo cha utafiti wa viazi cha SAGCOT anasema: “Hapa nchini Tanzania tuna aina tatu viazi mviringo zinazotambuliwa kisheria pamoja na kwamba viazi mviringo ni chakula kikuu nchini. SAGCOT na wadau wengine wa AGRA tunafanya juhudi kuongeza vipando bora zaidi ambavyo vitatoa tija kubwa na kuongeza mavuno.”
Ni dhahiri kuwa AGRA imetumbukiza fedha nyingi kuimarisha ndoto ya kuwa na rasrimali za kutosha kuweza kuwa na msingi wa viwanda vya kusindika mazao mbalimbali nchini lakini kilichobaki ni wataalamu wa ugani kuhimiza matumizi ya teknolojia katika kubadilisha maisha ya wakulima wetu kwanza kuwa na usalama wa chakula na pia kuongeza kipato chao. Kama alivyosema Mtendaji wa AGRA nchini, Dk Mary Mgonja suala lililobaki ni kuongeza matumizi ya teknolojia hizi.
“Ninatoa mwito kwa wakulima kukumbatia njia mpya za teknolojia katika kilimo ili kupata tija zaidi; kuanzia matumizi ya mbegu bora zilizoboreshwa mashambani hadi kwenye matumizi ya teknolojia mpya ya kuhifadhi mavuno. Njia hizo kama zitatumika vyema zitaongeza uzalishaji na kupunguza upotevu wa mavuno. Mambo hayo ni muhimu ili wakulima wadogo wajinasue kiuchumi,” alisema Dk Mgonja.
Dk Mgonja anatoa pongeza kwa serikali kutokana na kuboresha sera ya kilimo yenye lengo la kukabiliana na changamoto za wadau mbalimbali katika sekta ya kilimo na kusema Maonesho ya Nanenane yanasaidia kutambua na kuona tafiti mbalimbali na uwezo wa wakulima kuingia katika mabadiliko. Anasema maonesho hayo ya Nanenane ni sehemu ya shamba darasa muhimu ambapo wakulima mbalimbali wanaangalia na kupata maarifa mapya na pia kupata nafasi ya kubadilishana uzoefu katika kilimo ili kiwe cha kisasa zaidi badala ya kuwa kile kile kila msimu.
Hapa nchini AGRA inafanya kazi na serikali pamoja na mashirika mengine yapatayo 10, ikiwa ni pamoja na Tanzania Seeds Trade Association (Tasta), CSDI, Equity Bank, Unyiha Associates, Briten, Rudi, Agroz na taasisi za umma za ARI Uyole, Chollima AGRO, ARI Mlingano na kituo cha SAGCOT. Lengo kuu ni Tanzania kusonga mbele katika kilimo, jambo ambalo inawezekana.
“AGRA itaendelea kushirikiana na wizara ya kilimo, mifugo na uvuvi kuhakikisha kwamba shughuli zake nchini zinakwenda sambamba na juhudi za serikali ya Tanzania katika kuboresha kilimo,” anasema Dk Mgonja.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com