HIVI karibuni, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Rais John Magufuli akizungumza Ofisi ndogo ya Chama hicho iliyopo Lumumba mkoani Dar es Salaam, alisema anataka kuona CCM mpya na kwamba anataka kukirudisha chama katika maadili kama kilivyoachwa na Mwalimu Julius Nyerere.
Watu wengi wanajiuliza kama Mwenyekiti huyu mpya ataweza kutokana na hali halisi iliyopo ndani ya chama hicho ambacho kwa miaka kadhaa kimeacha kuangalia kanuni zake na kujiingiza katika misingi ya uchumi mchanganyiko na hivyo kuchipua kundi la matajiri ambalo lilienda kushika chama na taratibu kukifanya kionekane kama cha watu wenye nacho.
Pamoja na maswali wanayojiuliza wananchi mbalimbali na hasa wanaojua udhaifu wa watu wanyonge na ubabe wa watu wenye nacho waliomo ndani ya CCM katika nafasi mbalimbali za maamuzi kuanzia ngazi ya shina hadi taifa, CCM inajinasibu mashine yake inavyoweza kujitanabaisha katika kujiendesha. Uchumi mchanganyiko ulioruhusu ukuaji wa makabaila na mabepari umeenda kinyume na dhamira ya CCM iliyorithiwa kutoka Tanu na ASP ya kujenga misingi ya uchumi wa kijamaa na viongozi wake kukemea unyonyaji wa mtu na mtu.
Siasa za ndani za chama hicho kikongwe nchini zilizotokana na kutaka kuondokana na uchumi wa kikoloni uliowatenga wananchi na kuwafanya wananchi wawe na uchumi duni na maisha ya kusikitisha, zilikuwa zinaelekea kuliko kusikotakiwa. Baada ya huru, chama kilichukua hatua kadhaa za kuanzisha mfumo imara wa uchumi uliozingatia mambo mengi yakiwemo maadili ya viongozi, kubwa likiwa ni kujilimbikizia.
Inaelezwa kwamba, baada ya uhuru, watawala viongozi walitaka kuvaa vya wakoloni, yaani kutumia nafasi zao kufaidi wao tu keki ya taifa dhidi ya wanyonge na ndipo kukawa na haja kubwa ya kuwa na Azimio la Arusha. Kwa sasa viongozi wengi baada ya Azimio la Zanzibar wamekuwa mstari wa mbele kujilimbikizia mali wakisema waziwazi kwamba kuwa na mali si dhambi na hivyo kurudi alikokuwa anakupiga vita Mwalimu.
Huhitaji kuwa na shahada ya chuo kikuu kuelewa kwamba kiongozi (aliyeingia madarakani akiwa hana mali), hawezi kuwa tajiri bila kukanyaga maadili. Mwaka 1967 Chama cha Tanu (kilichowezesha uhuru wa Tanganyika) kilitangaza Azimio la Arusha, kikaamua kujenga ujamaa na kueleza dhahiri azma yake ya kujenga nchi ya ujamaa ambamo unyonyaji wa mtu na mtu utakuwa umetokomezwa.
Kikasma uchumi wa taifa utamilikiwa na kudhibitiwa na umma wa wakulima na wafanyakazi na uhusiano wa watu katika jamii kuwa wa kindugu, wakishirikiana kwa maendeleo ya wote. Miaka 20 baada ya kutangazwa kwa Azimio la Arusha, taifa lilipiga hatua kubwa katika kujenga msingi wa uchumi wenye mwelekeo wa kujengwa kwa nchi ya ujamaa.
Katika maelekezo ya chama kuhusu maendeleo ya uchumi na jamii katika kipindi cha 1987-1992, yaliyopitishwa na mkutano mkuu wa tatu wa kawaida wa taifa uliofanyika Kizota Dodoma, Oktoba 22 hadi 31,1987 iliandikwa kwamba hatua hizo ni pamoja na kutaifishwa kwa benki, viwanda, kampuni za biashara, bima, viwanda na huduma mbalimbali. Maelekezo hayo yalisema kwamba hatua hizo zilibadili dira ya maendeleo ya taifa na hasa kuwezesha rasilimali za taifa kutumika kwa makusudi ya kuendeleza uchumi wa taifa na hasa katika kutosheleza mahitaji ya taifa.
Aidha maelekezo hayo yalijinasibu kwamba hatua hizo zimesaidia kupunguza kwa kiwango kikubwa tofauti za mapato baina ya watu na hasa mapato ya mishahara. Kufanikisha mambo yaliyojenga matarajio makubwa ya wananchi kulitengenezwa mwongozo wa Chama wa mwaka 1971, Mwongozo wa 1981 lakini baada ya mabadiliko ya kisiasa na kung’atuka kwa Mwalimu Nyerere katika siasa za ndani za CCM mabadliko makubwa ya kiutendaji na kiuendeshaji yalifuata na shinikizo la maendeleo kwa msimamo wa Magharibi viliingia.
Ikawa taifa lililotaka kujenga misingi imara ya taifa linalojitegemea na viongozi wanaojali watu masikini, yaani wavuja jasho wa nchi hii, likafa. Huwezi kudharau mchango wa Azimio la Arusha kubana viongozi kujilimbikizia mali na kutafuta uongozi kwa kutumia fedha na kuweka msingi imara ya taifa linaloheshimu madaraka, mamlaka na ustawi wa jamii.
Shabaha na madhumuni ya Viongozi na Azimio la Arusha kwangu mimi ni ufafanuzi wa aina ya chama kinachojengwa na siasa zake, hivyo kuondoka kwa vyote hivyo kulileta aina mpya ya viongozi ambao wanataka mali na kutumia mamlaka waliyonayo kujilimbikizia mali, si kwa ajili ya umma bali wao wenyewe. Hata zamani machifu walikuwa na mali lakini walizitumia kwa ajili ya watu wao si kizazi hiki cha baada ya Azimio la Arusha kuuawa, wao wanajilimbikizia mali kuwa waungu watu na kutumia udhaifu uliopo kufanya wanavyotaka.
Si ajabu Rais Magufuli anapotaka wanachama wa chama hicho kumvumilia wakati atakapokuwa akifanya kazi ya kukirudisha kwenye maadili, kwani katika kuifanya kazi hiyo kuna mahali atakapoamua kunyoosha, atanyooshea hapo hapo. Wafanyabiashara waliingia ndani ya Chama wakafanya vitu vyao, ikawa shida kwelikweli kuwaondoa kwa kuzingatia kwamba wao ndio waliotengeneza na kuingiza watu katika serikali.
Kama alivyowahi kusema Mwalimu Nyerere, Chama legelege kikazaa wakati huo serikali legelege na dhamira ya kujenga msingi wa uchumi wa kijamaa ikawa ndoto. “Chama Cha Mapinduzi tumepanga tuanze kujisahihisha, kwa sababu chama ninachokipenda nimekulia humu, kilikuwa kimeanza kupoteza dira na hili lazima niliseme wazi bila unafiki,” alisema Rais Magufuli.
Kiukweli kukosekana kwa dira hiyo kumetokana na viongozi kushindwa kutofautisha dhana ya kipindi cha mpito kuelekea ujamaa na dhana ya uchumi mchanganyiko ambapo inawezekana kufikia ujamaa kwa kutokomeza ubepari na unyonyaji. Tukiwa hatuna sekta ya dola, sekta ya ubepari, sekta ya wananchi wavuja jasho binafsi na ushirika kama ilivyokusudiwa katika dhana ya kujenga ujamaa kupitia uchumi mchanganyiko, taifa lilikosa mwelekeo baada ya kuvunjwa kwa Azimio la Arusha na viongozi kuacha kuwajibika kufuata miiko ya uongozi.
Kwa mujibu wa Azimio la Arusha ni mwiko kwa kiongozi wa chama au serikali kuwa bepari au kabaila, kuwa na nyumba ya kupangisha, kuwa mkurugenzi wa kampuni ya kibepari na kuwa na mishahara zaidi ya mmoja. Katiba ya CCM ya sasa inataka mwanaCCM kuheshimu miiko hiyo ya kutotumia nafasi yako kujilimbikiza mali. MwanaCCM ni kiongozi. Kiukweli suala la miiko ya viongozi kwa wanachama na hata viongozi katika chama cha kijamaa ni muhimu na haiwezekani chama kiimbe ujamaa na viongozi wake wanatekeleza sera za kibepari na unyonyaji.
Kutokana na hili Rais Magufuli anaweza kusafisha sana eneo hili na ikawa tabu sana ingawa inajulikana tangu wakati wa Mwalimu Nyerere kwamba mwanachama wa CCM ni lazima awe mkulima (mvuja jasho) au mfanyakazi kwani haiwezekani katu mtu kulinda na kutetea maslahi yao ya ubepari na wakati huo huo kuwa mjamaa. Kutokuwa makini kumeifikisha CCM katika hali mbaya kwani hata Azimio la Arusha lilisema Tanzania si nchi ya Ujamaa kamili.
Bado ina ubepari na vishawishi vyake na ilipolegezwa ikawa balaa na ndio maana Magufuli atakuwa na kazi kubwa kuimarisha kazi ya chama ndani ya umma ili chama chake ambacho bado kinaungwa mkono na Watanzania wengi kiendelee kuongoza nchi huku kikiwa na picha halisi kuwa ni cha kutetea wanyonge. Katika hali ya sasa ambapo CCM ilikuwa imeanza kugeuka kuwa chama cha matajiri, ilifika mahali kama mtu ni masikini akiomba uongozi ilikuwa ni vigumu kuupata kama vile mtu kupita kwenye tundu la sindano na hilo alijionea mwenyewe wakati anagombea urais.
Magufuli amesisitiza kwamba mwaka ujao chama chake kitafanya uchaguzi wa nafasi mbalimbali, hivyo yeyote mwenye uwezo wa kuongoza aombe nafasi na atakayeomba na kutaka kutumia rushwa, atambue kuwa jina lake halitarudi, kwani hata yeye amechaguliwa bila kutumia hata senti. Kama kweli Rais Magufuli anataka heshima ya CCM irejee dhana ya kazi ya chama ndani ya umma ina maana kubwa ikiwamo ya kueleweka misimamo na kuzingatia inachosimamia katika kufanikisha maisha ya walio wanyonge.
Na katika hili CCM bado haijasema kwamba ni chama cha kibepari, bado ni cha kijamaa, hivyo makada wake lazima waamini katika hilo ili kushawishi umma kuwaunga mkono. Na katika hili utaona kuna kila sababu ya yeye kuondokana na mafisadi ndani ya chama hicho ili kibaki kuwa kipya na chenye maadili kama kilivyoachwa na Mwalimu Nyerere.
0 comments:
Post a Comment