Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete amesema uamuzi wa nani agombee urais kupitia chama hicho ulifanyika kwa pamoja na kufuata taratibu, hivyo anayetoka katika chama hicho kwa sasa ni kwa hiari na mapenzi yake.
Akizungumza na wajumbe wa Baraza Kuu la
Umoja wa Vijana wa CCM Dar es Salaam jana, Rais Kikwete alisema uamuzi
huo ulifanyika kwa mujibu wa Katiba ya CCM na ulipigiwa kura ndani ya
Halmashauri Kuu ya Taifa baada ya mjadala mrefu ambako uamuzi
ulichukuliwa kwa pamoja.
Kauli hiyo ya Rais Kikwete ni
majibu ya matamko ya hivi karibuni ya wanaCCM wanaotoka katika chama
hicho na kujiunga na vyama vinavyounda Ukawa, hasa Chadema, wakisema ni
kutokana na kuvunjwa utaratibu katika mchakato wa kumpata mgombea urais,
uliompitisha Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli.
Miongoni
waliotoka katika chama hicho tawala ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward
Lowassa pamoja na wenyeviti watatu wa mikoa ya Arusha, Singida na
Shinyanga; Onesmo Ole Nangole, Mgana Msindai na Hamis Mgeja.
Katika
majibu hayo, Rais Kikwete alisema hakuna haki iliyovunjwa katika
mchakato wa kutafuta mgombea urais wa CCM kwa sababu taratibu za chama
hicho zinajulikana wazi na ni zilezile.
Badala yake,
alisema mpango wa kukihama chama hicho ulikuwa umepangwa: “Ukweli ni
kwamba baadhi ya watu walikwishaamua kutoka CCM hata kabla ya vikao vya
Dodoma kuanza.”
Rais Kikwete aliwaambia vijana hao:
“Aliyetoka, katoka mwenyewe kwa uamuzi wake mwenyewe lakini pale
tuliamua wote. Maana pale tulipokubaliana kupiga kura, tulikubaliana
kupiga kura kwa majina yale matano, siyo uamuzi wangu pekee yangu, bali
ulikuwa uamuzi wa sote. Maana tulijadiliana na kukubaliana kwamba kwa
mujibu wa katiba yetu majina ni hayahaya. Tukapiga na kura yakaisha.”
Alisisitiza:
“Hivyo, anayetoka, anatoka kwa hiari yake mwenyewe kwa sababu pale
Dodoma sote tulikubaliana… na kwa kweli wote wanaotaka kutoka ndani ya
CCM wanatoka kwa hiari yao wenyewe na wala siyo kwa sababu ya kunyimwa
haki.
“Sasa mchakato umekwisha. Aliyepata kapata.
Aliyekosa kakosa. Mchakato huo haurudiwi tena, hatuwezi kuitisha tena
mkutano mkuu. Lililobakia sasa tunasubiri sasa Ndugu Magufuli arudishe
fomu na baada ya hapo ni Iyena Iyena na mambo yanakwenda. Haya ndiyo
mapenzi ya Mungu.”
Katika mchakato huo wa Dodoma, CCM
ilimteua Dk Magufuli kuwa mgombea urais na Lowassa ambaye jina lake
lilikatwa katika hatua za awali alihamia Chadema ambako pia chama hicho
kikishirikiana na vile vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),
kimempitisha kuwania urais.
Magufuli aanza vijembe
Katika
mkutano huo, Dk Magufuli alisema baadhi ya wapinzani ni waigizaji
wakubwa ambao wamesomea uigizaji na wataufanya Uchaguzi Mkuu wa mwaka
huu kutawaliwa na mbwembwe na maigizo mengi.
Alisema kazi kubwa ya CCM ni kukabiliana na mbwembwe na maigizo hayo ili kuyashinda.
Magufuli alisema CCM siyo watu wa matumaini, bali ni watu wa maendeleo na safari ya uhakika.
Alisema wapinzani wa CCM sasa wameanza kunukuu kila kitu hasa nyimbo za chama.
Aliwaambia
vijana hao: “Katika mchakato huu na katika uchaguzi wa mwaka huu kuna
mbwembwe nyingi, kuna mbinu nyingi na kuna maigizo mengi hasa kwa sababu
wako wengine walisomea maagizo. Kwa hiyo tuna wajibu wa pamoja
kuyashinda haya maigizo.”
0 comments:
Post a Comment