UMOJA wa Mataifa nchini Tanzania umetia saini mkataba na ubalozi wa Norway wa Sh bilioni 6. 9 (dola za Marekani milioni 3.1) kusaidia masuala mbalimbali nchini Tanzania. Masuala hayo ni ya wakimbizi, utawala bora, haki za binadamu na ushirikiano na watu wa Zanzibar.
Mkataba huo umetiwa saini kati ya balozi wa Norway nchini Tanzania Hanne-Marie Kaarstad na Mratibu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa Alvaro Rodriguez. Akizungumza baada ya kutiwa saini Hanne-Marie Kaarstad alisema Tanzania ni moja ya mfano bora wa mashirika ya Umoja wa Mataifa yakifanya kazi kwa pamoja kwa umakini mkubwa.
“Umoja wa Mataifa umekuwa ni mshirika mkubwa wa Norway katika Nyanja mbalimbali za maendeleo,“ alisema na kuongeza kwamba ni matumaini yake kwamba malengo endelevu ya maendeleo ambayo yatapitishwa septemba mwaka huu yatahitaji maandalizi mazuri na usimamizi wa karibu.
Alisema kutokana na mazingira hayo Norway itaendelea kushirikiana na Umoja wa Mataifa katika kufanikisha majukumu yake nchini Tanzania ya kusaidia kuleta maendeleo endelevu. Naye Mratibu wa Umoja wa Mataifa nchini, Alvaro Rodriguez alishukuru serikali ya Norway kwa kuwa mshiriki wa karibu wa shughuli za Umoja wa Mataifa.
Norway amekuwa mshiriki mkubwa wa maendeleo ya Tanzania kupitia Umoja wa Mataifa na kwamba katika mpango wa UNDAP 2011-2016 kuanzia Desemba 14, 2011 umeshatoa Krona za Norway milioni 111.
0 comments:
Post a Comment