KITENDAWILI cha Chama cha Wananchi (CUF) kuridhia hoja ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kusimamisha mgombea mmoja wa nafasi ya urais kwa upande wa vyama vya upinzani, kinatarajiwa kuteguliwa Jumamosi ya wiki ijayo, ambapo Baraza Kuu la Uongozi wa Taifa wa chama hicho litakaa kujadili na kutoa uamuzi.
Hii ina maana kwamba, kama Baraza Kuu likipinga, itakuwa rasmi kwamba ndoto za vyama vya upinzani kusimamisha mgombea mmoja zitafutika.
Hayo yalibainishwa jana Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu Bara wa CUF, Magdalena Sakaya alipokuwa akizungumzia ushiriki wao kwenye Ukawa pamoja na kutohudhuria kwao juzi kwenye kikao cha Ukawa kujadili majimbo ya uchaguzi na kumtaja mgombea nafasi ya urais kupitia kundi hilo.
Sakaya alisema CUF ni sehemu ya Ukawa na wanaendelea kushiriki kwenye vikao vya kuafikiana maamuzi kwa hoja mbalimbali na kwamba hawajajitoa kwenye Ukawa kama ambavyo baadhi ya mitandao na vyombo vya habari vimeripoti. “Hatujajitoa Ukawa, sisi ni sehemu ya Ukawa na hatuwezi kusaliti kitu tulichokiasisi wenyewe,” alisema Sakaya.
Na kuongeza, taharuki iliyopo mitaani kwamba CUF wamejitoa inachangiwa na baadhi ya vyombo vya habari ambavyo siku chache zilizopita vimekuwa vikiripoti kwamba Ukawa imeshamteua mgombea nafasi ya urais, jambo ambalo limezua taharuki kwa wanachama wa CUF, kwa kuwa hawajatoa ridhaa hiyo.
Alisema kutokana na taharuki hiyo, wanachama wameingiwa na hofu ya jambo hilo kwa kuwa hakuna ridhaa iliyoafikiwa na vikao vya maamuzi, na kwamba hali hiyo imeifanya chama hicho kuitisha kikao cha Baraza Kuu la Uongozi, chombo ambacho ndicho chenye maamuzi ya kutoa ridhaa hiyo.
“Baada ya kuona habari hizo kwenye baadhi ya vyombo vya habari na mitandaoni, wanachama wetu wameingiwa na hofu ya ushirikishwaji na tumeitisha Baraza Kuu la Uongozi litakutana Julai 25, mwaka huu, tutajalidi na kutoa uamuzi wetu,” alisema Sakaya.
Kuhusu kushirikishwa kwao ndani ya Ukawa, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF, Abdul Kambaya alisema kwa mfano kikao cha juzi kilichofanyikia hoteli ya Colosseum, Dar es Salaam, walipata taarifa baada ya kikao kuanza, hivyo walishindwa kuhudhuria kwa kuwa walikuwa kwenye kikao cha dharura cha wanachama wao.
“Hizo taarifa za kikao cha Ukawa cha kumtangaza mgombea na kuzungumzia majimbo ya uchaguzi mapya, mwenyekiti wetu alipata taarifa mara baada ya kikao kuanza majira ya saa nne asubuhi, baada ya kuonekana hayuko, hakuweza kuhudhuria kwa kuwa tulikuwa kwenye kikao kingine cha wanachama wetu”, alisema Kambaya.
Aliongeza kuwa, kikao hicho cha jana taarifa za uwepo wake hazikuwa wazi mapema na kwamba mwakilishi wao aliyehudhuria ni wa ngazi ya wataalamu na sio ngazi ya viongozi wakuu, ambao ndio wenye maamuzi.
Kutokana na hali hiyo, alisema mkutano wa Julai 25 ndio utakaotoka na maamuzi ya ama kukubali maridhiano ya Ukawa ya kusimamisha mgombea mmoja au vinginevyo.
“Tunaomba tusubiri baraza la maamuzi likae, sisi tunafanya kazi kwa kushirikisha wanachama wetu na baraza hilo, litakuja na maamuzi ya masuala yote ya uchaguzi na mengineyo,” alisema Kambaya.
Juzi, katika kikao cha Ukawa kilichofanyika hoteli ya Colosseum kilihudhuriwa na viongozi wa juu wa vyama vinavyounda kundi hilo, isipokuwa kiongozi wa CUF, na kilipangwa kumtaja mgombea mmoja wa urais kupitia kundi hilo atakayechuana na wagombea wengine, akiwemo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli.
Hata hivyo katika kikao hicho kilichokaa hadi usiku saa tatu, hakikumtaja mgombea wa nafasi hiyo na badala yake kilisema jina la mgombea wanalo na kwamba watalitangaza ndani ya siku saba.
0 comments:
Post a Comment