Na Mathias Canal,
WEST-Dar es salaam
Serikali imeweka bayana
dhaira yake ya kuchukua hatua kali za uwajibikaji kwa Maafisa Elimu wa Mikoa,
Wilaya, Walimu na maafisa wengine wote wakiwemo askari ambao wamepewa jukumu la
kusimamia mitihani.
Hatua hizo dhidi ya
wasimamizi hao wa mitihani zitahusisha kusimamishwa kazi, kufukuzwa pamoja na
kufikishwa mahakamani ili wafungwe jela.
Waziri wa Elimu, Sayansi
na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda (Mb) ameyasema hayo leo tarehe 5 Disemba
2022 wakati akizungumza na uongozi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi
Muhimbili kampasi ya Mlongazila katika Wilaya ya Ubungo Mkoani Dar es salaam
alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja.
Amesema kuwa ili
kuimarisha sekta ya elimu lazima kushughulika na watu wanaofanya udanganyifu
ikiwemo kuwachukulia hatua kali na kuwajibika huko sio tu kufukuzwa kazi kama
ilivyozoeleka au kupewa onyo pekee bali wafungwe jela ili iwe fundisho kwa
wengine.
Waziri Mkenda amesema
kuwa Baraza la Mitihani Tanzania (NACTE) limeongeza mikakati ya kupambana na
watu ambao wanafanya udanganyifu kwenye vituo vya mitihani ambapo serikali
imewakamata na kuwachukulia hatua wasimamizi wote kwa kushirikiana kufanya
ubadhilifu wa mitihani.
Amesema kuwa serikali
imechunguza na kubaini kuwa watumishi wa serikali na watumishi wa sekta binafsi
wamehusika kwenye udanganyifu wa elimu na kuwachukulia hatua.
"Sasa nisisitize kuna kauli inasema ukitaka kuuwa Taifa basi uwa elimu, sasa tunafanya mageuzi ya elimu nchini kwenye sera na mitaala lakini haiondoi jukumu la kusimamia elimu tunayoitoa sasa hivi inatolewa kwa taratibu zinazokubalika" Amesisitiza Waziri Mkenda
Waziri Mkenda amesema
kuwa udanganyifu katika mitihani una madhara ya kumuwezesha mtu kufaulu ambaye
hakustahili kufaulu kwani akiwa daktari ataleta athari kubwa katika jamii.
"Hasara mojawapo
kubwa kwa Taifa letu ya kuvujisha mitihani ni kuwafundisha watoto katika umri
mdogo kwamba ili uendelee ni lazima ufanye udanganyifu, tunaanza kujenga rushwa
mapema mno na serikali haitakubali kitu kama hicho" Amekaririwa Waziri
Mkenda
"Wale waliohusika
hasa watumishi wa serikali, Maafisa elimu na watu wote waliohusika mahali pao
kwa kweli ni jela, tunaongea na mamlaka husika kwamba tusije tukawafukuza tu
kazi, wanachokifanya ni jinai, ukiangalia gharama za kuendesha mitihani ni
kubwa sana kwahiyo mtu anayevuruga mitihani ashitakiwe mahakamani wahukumiwe na
waende jela" Amesisitiza Waziri Mkenda
Waziri Mkenda ameeleza
kuwa serikali itapitia sheria ili kama kuna mwanya wa kuwawezesha watu kufanya
udanganyifu na wakatoka bila kuchukuliwa hatua yoyote kuwe na namna ya kufanya
mabadiliko.
Amesema anayechezea
mtihani afungwe jela na ametoa onyo kwa wote wanaofanya hivyo kuacha mara moja
udanganyifu huo.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment