Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda ameipongeza Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kwa hatua mbalimbali za kimaendeleo na kiteknolojia ambazo imepiga kwa kipindi kifupi tangu apewe dhamana ya kuongoza Wizara hiyo.
Prof. Mkenda amesema hayo leo katika Mahafali ya 16 ya taasisi hiyo alipokuwa mgeni rasmi ambapo ameikumbusha DIT kuwa Serikali inawategemea wanasayansi na wahandisi katika azma yake ya kuwa nchi ya uchumi wa viwanda na DIT imepewa jukumu la kimkakati katika kuhakikisha inazalisha wataalamu katika fani ya sayansi na uhandisi.
"Ni kweli nimefika hapa mara kadhaa na ninakumbuka maelekezo yangu ya kwanza kwenu nilipowatembelea mwezi Januari, 2022 niliwataka kuanzisha kiwanda cha kutengeneza vipuri vya vyombo vya moto. Nilifika tena hapa tarehe 28 Julai, 2022 nikaona hatua mliyokuwa mmepiga katika utekelezaji wa maelekezo yangu, nilifarijika kwa hatua hiyo," amesema.
Katika mahafali hayo jumla ya wahitimu ni 1040, kati yao wakiume ni 782 na wakike ni 258 wametunukiwa tuzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Stashahada 503, Shahada ya kwanza 510 na 27 wa Shahada ya Uzamili.
Waziri Prof. Mkenda amesema Wizara yake inatambua kuwa DIT ni kiwanda cha kuzalisha wataalam wenye weledi wanaotarajiwa kuchachua sekta ya viwanda na kwamba maendeleo makubwa ya kiuchumi yanatokana na matumizi mazuri ya elimu ya ufundi, sayansi na teknolojia.
Prof. Mkenda ameipongez pia DIT kwa kuimarisha ushirikiano na mataifa kupitia makubaliano mbalimbali ambayo imeingia ya kitaifa na kimataifa.
"Nilipata fursa ya kutembelea kule Uingereza katika Chuo Kikuu cha Northampton na kukutana na Watumishi wawili wa DIT wanaosoma kule, kwenye hili nawapongeza sana na kuwataka kuwa inapotokea fursa ya kupeleka watumishi nje ya nchi basi iwe ni katika vyuo vikubwa vya aina hiyo ili kuendana na azma ya Serikali kuwapatia Watanzania elimu itakayotuwezesha kukidhi mahitaji ya Kikanda na Kimataifa," amesema.
Aidha, kwa upande wa Wizara amesema itaendelea kusimamia uendelezaji wa masuala ya sayansi, teknolojia na ubunifu ili kutoa fursa kwa wabunifu na wagunduzi mbalimbali kujitokeza, kuonesha bunifu na gunduzi zao kupewa fursa ya kuzitumia kusaidia jamii yetu na kuwaendeleza ili kufikia hatua ya kuzibiasharisha katika soko.
Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam, Prof. Preksedis Ndomba amesema mwaka huu idadi ya wahitimu wa kike ni sawa na asilimia 25, asilimia hiyo ni sawa na ile ya wahitimu wa kike kwa mwaka uliopita.
Prof. Ndomba amesema wahitimu hao ni wanufaika wa mfumo mpya wa ufundishaji kwa vitendo ambapo wameshiriki kutatua changamoto mbalimbali zilizokuwa zikisumbua mfano ndani ya taasisi.
"Tumekua na changamoto mbalimbali na hawa vijana wamesaidia kuzitatua mfano karabati wa bweni namba 1 kwa kuweka mfumo mpya wa umeme kazi iliyofanywa na wanafunzi wa uhandisi umeme pamoja na kazi ya kugawa vyumba (patitioning) katika bweni hilo hilo iliyofanywa na wanafunzi wa idara ya uhandisi ujenzi," amesema.
Amesema baadhi ya wahitimu walipata fursa ya kwenda nje ya nchi kwa mafunzo mbalimbali katika teknolojia za kisasa na katika ubunifu pia miongoni mwao wamebuni teknolojia mbalimbali na zipo katika hatua za mwisho za ubiasharishaji zinazosimamiwa na Kampuni Tanzu ya Taasisi (DIT Co. Ltd).
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam, Dkt. Richard Masika amesema
DIT imejipambanua kama kiongozi katika kuchachua maendeleo ya viwanda hapa nchini kwa kupitia ukuzaji wa teknolojia na ubunifu.
Baraza la Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam limefanikiwa kuboresha miongozo mbalimbali inayohusu ustawi na maendeleo ya wafanyakazi na pia tumeweka mazingira mazuri kwa wahitimu wetu kuweza kupata fursa ya kujitolea kufanya kazi katika taasisi kwa nia na lengo la kupata uzoefu unaohitajika na soko la ajira.
Kama unavyofahamu kuwa mafunzo ya ufundi hukamilika vyema zaidi pale mwanafunzi anaposhiriki mafunzo kwa vitendo viwandani au katika mnyororo wa uzalishaji. Lakini, tunakabaliliwa na uhaba wa nafasi za mafunzo kwa vitendo viwandani kukana na utayari mdogo wa viwanda kutoa nafasi za mafunzo hayo kwa wanafunzi wetu
Pongezi nyingi kwa wahitimu wetu kwa kumaliza safari yao ndefu ya kitaaluma katika Taasisi yetu kwa mafanikio. Hatua ambayo vijana hawa wamepiga katika maisha yao ni kubwa, na ninaamini wameiva vizuri katika elimu ya darasani pamoja na mafunzo waliyopata kwa vitendo. Hawa wote ni watendaji wazuri na wako tayari kuwahudumia Watanzania. Ni imani yangu kwamba watakuwa mabalozi wazuri wa Taasisi yetu na Taifa letu.
Mwisho
0 comments:
Post a Comment