Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema ujenzi wa Gati Jipya la Abiria katika Bandari ya Kigoma utakuwa chachu ya kukuza biashara na kuimarisha usafiri kwa njka ya maji katika ukanda wa Ziwa Tanganyika
Prof. Mbarawa ameyasema hayo wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa gati hilo, ambalo linajengwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Japan kupitia ruzuku, huku ujenzi wake ukiwa umeanza tangu Juni,2025
Amesema mradi huo wenye thamani ya Shilingi bil. 53, utakapokamilika utaimarisha usafirishaji wa abiria na mizigo, kuongeza usalama wa huduma za usafiri kwa njia ya maji na kuchochea shughuli za kiuchumi katika mikoa ya Kigoma, Katavi, Rukwa, pamoja na nchi jirani
“Tunajenga meli, tunakabati bandari na tunajenga reli ili kuhakikisha mifumo yote ya uchukuzi inaunganishwa na kuleta tija kiuchumi,” amesema Prof. Mbarawa
Gati hilo litakuwa na urefu wa mita 130, upana mita 50, Mradi huo pia utahusisha ujenzi wa barabara yenye urefu wa mita 481 kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma hadi eneo la gati
Prof. Mbarawa amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya uchukuzi ili kuifanya Kigoma kuwa lango muhimu la biashara na shughuli za kiuchumi katika Ukanda wa Ziwa Tanganyika na Ukanda wa Maziwa Makuu
Kwa upande wake, Meneja wa Bandari za Ziwa Tanganyika, Bw. Ernest Mabula, amesema kukamilika kwa gati hilo kutaboresha ufanisi na usalama wa huduma za usafiri kwa njia ya maji, kuongeza usafirishaji wa abiria na mizigo na kukuza biashara katika ukanda huo
Naye Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Dkt. Rashid Chuachua, ameishukuru Serikali kwa uwekezaji huo, akisema gati hilo litachochea ukuaji wa uchumi, kuongeza fursa za biashara na kuboresha huduma za usafiri kwa wananchi.







0 comments:
Post a Comment