METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, August 5, 2024

MBOLEA KUWAFIKIA WAKULIMA HADI NGAZI ZA VIJIJI- CLAUDIA KIMAKO




Na Saida Issa, Dodoma 

IMEELEZWA kuwa kiwanda cha Mbolea cha Itracom kilichopo Nala jijini Dodoma, kimeweka Mkakati wa kuwafikia wakulima wote hadi ngazi ya kijiji kwa kusambaza mbolea lengo likiwa ni  kuwapunguzia mzigo wakulima.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Maendeleo  ya biashara  na masoko wa kiwanda hicho Claudia Kimako jijini Dodoma  wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Kimako alisema kuwa Mkulima hatakuwa na haja ya kusafiri  kwenda Wilayani kwaajili ya kununua mbolea kwani tayari wameandaa mikakati ya kuwafikia walipo. 

Alisema kwa mkakati huo wakulima wengi wataweza kutumia mbolea hiyo na ongezeko la watumiaji litakuwa kubwa kutokana na ubora wake na wao kama kiwanda watahakikisha kwamba kila mkulima anafikiwa.

"Sisi kama kiwanda cha itracom kinachozalisha mbolea hapa nchini na mbolea yetu ni mchanganyiko wa asili na chumvi chumvi tunapenda kuwasihi wakulima kutumie mbolea hizi ili warudishe rutuba kwenye ardhi yao,"alisema.

Kiwanda hicho kina aina tatu za mbolea kinachozalisha ikiwemo mbolea ya kupandia,mbolea ya kukuzia pamoja na mbolea ya kukuzia mazao yenye asili ya mizizi.

Akitoa taarifa ya  kiwanda hicho Kimako alisema Kiwanda hicho  kina viwanda vitatu,viwanda viwili tayari vimeanza uzalishaji na vinauwezo wa kuzalisha tani laki mbili kwa kila kiwanda, ambapo kwa uzalishaji wa viwanda hivyo ni tani laki 4 kwa mwaka pia, kuna kiwanda kimoja ambacho kipo katika majaribio nacho kinauwezo wa kuzalisha tani laki mbili.

"Pia kuna viwanda viwili vinavyomaliziwa kufungwa kwahiyo tunategemea hadi mwisho wa mwaka Disemba 2024 tutakuwa na uwezo wa kuzalisha kiasi cha tani milioni moja kwa mwaka,"alisema.

Akizungumzia hali ya usambazaji wa mbolea hizo alisema kuwa mbolea hizo zinasambazwa nchini na nchi jirani.

"Tumeshafanikisha kupeleka mbolea yetu Nchini Kenya pia Burundi ambapo ndio asilia ya hiki kiwanda na kwa hapa Tanzania tayari tumeshaifikia mikoa 21 na katika maeneo yote mbolea yetu ilipofika matokeo ni mazuri,"alisema.

Kadhalika alisema kuwa, changamoto wanayokumbana nayo nikwamba mbolea hiyo bado mpya kwani jamii bado hawajaifahamu hivyo wanaendelea kuandaa mashamba darasa kwa wakulima ili waweze kuifahamu mbolea hiyo.

Hata hivyo Kimako  alielezea kuhusu suala la ajira kuwa mpaka sasa Watanzania 610 wamepata ajira katika kiwanda cha itracom huku warundi wakiwa ni 236.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com