METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, February 14, 2024

TANZANIA KUWA NCHI YA 22 AFRIKA KUFANYA UTAFITI WA GHARAMA ZA UTAPIAMLO NCHINI-MHE UMMY NDERIANANGA


Na Mathias Canal, Dodoma

Tanzania itakuwa nchi ya 22 barani Afrika kufanya utafiti wa gharama za utapiamlo nchini pindi utakapokamilika. 

Mwaka 2024, takribani nchi 6 (ikiwemo Tanzania) zimeonesha utayari wa kufanya utafiti huo ili kuwezesha nchi kupanga malengo ya kupunguza upotevu wa pato ghafi itokanayo na utapiamlo na kuwekeza katika maeneo ya maendeleo. 

Hayo yamebainishwa leo tarehe 14 Februari 2024 na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) wakati akizindua zoezi la utafiti wa gharama za utapiamlo nchini.

Mhe Nderiananga amesema kuwa tafiti hizo zinazofanyika hapa nchini ni moja ya jitihada za kutafuta shahidi za kisayansi zinazoweza kuisaidia Serikali kuboresha harakati zake za kuondokana na athari za utapiamlo (hasa udumavu kwa watoto pamoja na uzito uliozidi au kiribatumbo kwa watu wenye miaka 15-49). 

“Hivyo basi, ni jukumu letu sote kama Serikali na wadau kuhakikisha tunafanya tafiti nyingi zinazogusa changamoto zilizo katika jamii zetu. Lengo ni kupata taarifa sahihi zitakazochagiza harakati za kuelekea maendeleo endelevu na kuimarisha ustawi wa Taifa letu kupitia nguvukazi ya watu wenye afya njema, ufahamu mzuri na wenye uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za kiuchumi” Amesisitiza Mhe Nderiananga

Amesema kuwa ameridhika na taarifa zote zilizotolewa kuhusu chimbuko, msingi na umuhimu wa kufanya zoezi la utafiti huu pamoja na maelezo ya jinsi ilivyopangwa kulitekeleza. 

Mhe Ummy amewashukuru wataalamu wa Chakula na Lishe kwa kuishauri vyema Serikali juu ya umuhimu wa utafiti huo katika nchi inapokwenda kuandaa Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050. 

Kadhalika amewashukru wadau wakiwemo Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) ambao tayari wameshatoa fedha ambazo zitasaidia katika hatua muhimu za utafiti huo. 

“Kwa mujibu wa maelezo ya utangulizi huu ni utekelezaji wa maazimio ya viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kupitia mpango ujulikanao kama “The Cost of Hunger Study in Africa – COHA” ambapo Mheshimiwa DKt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameridhia ufanyike” Amesisitiza na kuongeza kuwa

“Hii inatokana na nia yake ya dhati ya kuondoa utapiamlo nchini. Lengo la utafiti ni kubainisha makadirio ya gharama zinazosababishwa na matatizo ya lishe duni/utapiamlo; kijamii na kiuchumi na hususan katika nyanja za sekta ya afya, elimu na nguvu kazi”

MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com