Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa (katikati) ,akizungumza Oktoba 10, 2023 na viongozi na watumishi wa sekta ya ardhi Mkoa wa Singida akiwa kwenye ziara yake ya kikazi ya siku moja ya kufuatilia utekelezaji wa maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusu utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975. Kulia ni Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Singida, Shamim Hoza na Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Mkoa wa Singida, Judith Mwalongo.
Na Dotto Mwaibale, Singida
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa amesema kuanzia
sasa mtumishi yeyote wa wizara hiyo atakaye kiuka miiko na maadili ya kazi
hatavumiliwa.
Silaa aliyasema hayo Oktoba 10, 2023 wakati akizungumza na viongozi na
watumishi wa sekta ya ardhi Mkoa wa Singida akiwa kwenye ziara yake ya kikazi
ya siku moja ya kufuatilia utekelezaji wa maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusu
utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975.
Alisema kuna migogoro ya ardhi ambayo inatatulika na mingi inasababishwa na
utendaji mbovu wa baadhi ya waliopewa kusimamia kazi hiyo na wanapofanya makosa
wamekuwa wakihamishwa kutoka sehemu alipofanyia kosa na kupelekwa kituo kingine
cha kazi jambo ambalo katika kipindi atakachokuwepo kwenye wizara hiyo
hatakiendekeza.
“Mfanyakazi atakayefanya kosa nitamalizana naye papo hapo sitahitaji
kumpeleka kwingine,” alisema Silaa ingawa hakufafanua atamalizana naye kivipi
mfanyakazi huyo atakayebainika kutenda kosa.
Silaa aliwataka wafanyakazi wa wizara hiyo kufanya kazi zao kwa kufuata
sheria na haki akiamini kuwa ni wanataaluma na si vinginevyo.
Aidha, alirudia tena kwa kuwaelekeza watendaji wa sekta ya Ardhi nchini
kuhakikisha ndani ya siku mia moja kuanzia Septemba 4, 2023 wanatatua migogoro
ya ardhi ili kuwafanya wananchi wawe na imani na Serikali yao na kuifurahia
wizara hiyo.
Alisema hatapenda kuona wananchi wakiinua mabango pale viongozi wakitaifa
wanapokuwa kwenye ziara katika maeneo mbalimbali wakilalamikia migogoro ya
ardhi.
Hata hivyo alipongeza ofisi ya Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Singida kwa
umahiri na ustadi wa utendaji katika zana pana ya kushughulikia migogoro
mbalimbali ya ardhi sambamba na hatua nzuri za upimaji, umilikishaji na
usimamizi wa matumizi bora ya ardhi mkoani hapa.
Aidha, pia alipongeza Shirika la Nyumba
la Taifa (NHC) kwa ukusanyaji madhubuti wa mapato na ufanisi wa kiutendaji huku
akiwataka watendaji kuendelea kuchapa kazi wakati Serikali inaangalia namna ya
kutatua changamoto zilizopo.
Hata hivyo Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Singida, Shamim Hoza pamoja na kumshukuru waziri kwa
ziara hiyo alimuhakikishia kwamba wafanyakazi watazingatia maagizo yote
yaliyotolewa kwa tija, ukuaji na mstakabari mzuri wa sekta nzima ya ardhi ndani
ya Mkoa wa Singida.
Pia Hoza alishauri uwepo wa dhana ya ushirikishwaji baina ya watumishi wa
sekta ya ardhi katika kutekeleza majukumu mbalimbali ili kuondoa migongano ambayo
huathiri utendaji ndani ya sekta hiyo.
Akizungumzia mafanikio alisema ofisi yao kwa mwaka 2021 imefanikiwa kuandaa
michoro 61 kwenye viwanja 19,620 na kueleza kuwa idadi hiyo inapanda kadri
wanavyoendelea kutoa elimu kwa wananchi na kuwa changamoto kubwa waliyonayo ni
uhaba wa watumishi katika kada zote, kuwa na gari moja na ufinyu wa bajeti.
Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Mkoa wa Singida, Judith Mwalongo
alisema mkoa huo una jumla ya viwanja 105, ambapo vilivyoendelezwa ni 38 na
ambavyo bado havijaendelezwa ni 67 na kuwa vipo katika maeneo tofauti tofauti.
Alisema Mkoa wa Singida una jumla ya majengo 39 yakiwa na jumla ya nyumba
(units) 171, ambapo asilimia 90 ya nyumba hizo zipo katikati ya mji wa Singida.
Hata hivyo Mwalongo alisisitiza kuwa shirika hilo limefanikiwa kukusanya mapato
mara dufu zaidi ya matarajio yaliyowekwa.
Alisema Mkoa wa Singida kwa mwaka 2022/2023 umeweza kuongeza mapato kwa
kuongeza kiwango cha bili ya mwezi kwa asilimia 20 na kuanzia Julai 2023 mpaka
Septemba kwa asilimia 6 ambapo kwa mwezi Juni 2022 walikusanya Sh. 45,850,630
na Juni 2023 walikusanya Sh.54,978,984 sawa na asilimia 20.
Alisema kwa Julai 2023 walikusanya Sh. 54,985,358.78 na Septemba 2023 walikusanya Sh.58,071,718.78.
Mwalongo akizungumzia makusanyo ya kodi alisema kwa mwaka wa fedha
2022/2023 mkoa ulitakiwa kukusanya jumla ya Sh.611,456,618.56 (pamoja na VAT)
na mpaka wanafunga mwaka huo wa fedha wamefanikiwa kukusanya jumla ya
Sh.756,618,432.60 (pamoja na VAT) ambayo ni sawa na 123.7 asilimia.
Alisema mwaka huu wa fedha kwa kipindi cha Julai mpaka Septemba 2023
walitakiwa kukusanya Sh.186,304,138.45 (pamoja na VAT) mpaka sasa wamekusanya
jumla ya Sh.239,538,125.4.
Mwalongo alisema Mkoa wa Singida utaendelea kuhakikisha unatekeleza
majukumu yake ikiwemo kuhakikisha kodi inakusanywa kikamilifu pamoja na kuhakikisha
madeni hayoongezeki bali yanapungua.
Aidha, alisema mkoa utaendelea kulishirikisha shirika juu ya fursa zilizopo mkoani Singida (uwepo wa viwanja vya wazi, uwepo wa viwanja vyenye majengo chakavu katika maeneo ya kimkakati na uhitaji wa nyumba za makazi na biashara) ili waweze kuzitumia kikamilifu katika kuhakikisha wanaongeza mapato ya mkoa na shirika kwa ujumla.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa, akisalimiana na Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Singida, Shamim Hoza mara alipowasili ofisi za Ardhi Mkoa wa Singida wakati wa ziara hiyo. Katikati ni Mpima ardhi Mkoa wa Singida, Sesaria Williams na kushoto ni Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi Wilaya ya Singida, Bahati Colex.
0 comments:
Post a Comment